Waliofariki ajali ya ndege Ziwa Victoria kuagwa leo

Muktasari:

  • Ajari hiyo ya ndege ilihusisha ndege aina ya ATR 42-500 ilikuwa ikitoka Dar es Salaam kwenda Bukoba na ilipotaka kutua katika uwanja wa ndege wa Bukoba iliangukia ziwani, mita 100 kutoka ulipo uwanja wa ndege.

Dar es Salaam. Miili ya watu 19 waliofariki dunia katika ajali ya ndege ya Precision Air iliyotokea jana Jumapili Novemba 7, 2022 inatarajiwa kuagwa leo.


Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albart Chalamila shughuli ya kuaga miili hiyo itaanza saa nne asubuhi katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Chalamila alisema kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ataongoza shughuli ya kuaga miili hiyo ambapo baada ya kumaliza kuaga, itakabidhiwa kwa ndugu zao kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Maandalizi ya sehemu ya kuweka majeneza yenye miili ya watu 19 waliofariki katika ajali ya ndege ya Precision Air katika Ziwa Victoria. Miili hiyo itaagwa katika uwanja wa Kaitaba. Picha na Alodia Dominick

Ndege hiyo iliyopata ajali ya kutumbukia Ziwa Victoria, mita 100 kabla ya kutua Uwanja wa Ndege wa Bukoba, Mkoa wa Kagera ilikuwa na abiria 43 ilikuwa ikitoka Dar es Salaam kwenda Bukoba.

Katika ajali hiyo, Watu 19 walikufa huku wengine 26 wakiokolewa katika jitihada zilizofanywa na wananchi wa Bukoba wengi wao wakiwa wavuvi katika Ziwa Victoria pamoja na vyombo vingine vya uokoaji.