Rais Samia awashukuru wakazi wa Kagera kwa uokoaji

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amewashukuru wananchi wa Kagera kwa ujasiri, ushirikiano na jitihada walizofanya wakati wa kuwaokoa abiria waliokuwemo kwenye ndege ya Precision iliyoanguka katika Ziwa Victoria.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewashukuru wananchi wa Kagera kwa ujasiri, ushirikiano na jitihada walizofanya wakati wa kuwaokoa abiria waliokuwemo kwenye ndege ya Precision iliyoanguka katika Ziwa Victoria.

Ajali hiyo ya ndege imehusisha ndege aina ya ATR 42-500 ilikuwa ikitoka Dar es Salaam kwenda Bukoba na ilipotaka kutua katika uwanja wa ndege wa Bukoba iliangukia ziwani, mita 100 kutoka ulipo uwanja wa ndege.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Watu 19 wamekufa katika ajali hiyo huku wengine 26 wakiokolewa katika jitihada zilizofanywa na wananchi wa Bukoba wengi wao wakiwa wavuvi katika Ziwa Victoria pamoja na vyombo vingine vya uokoaji.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Novemba 7, 2022 na Mkurugenzi wa Mawasilaino ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus, Rais Samia amewapa pole wafiwa wote na majeruhi wa ajali hiyo ya aina yake iliyogharimu maisha ya watu.

“Rais amewashukuru wakazi wa Kagera kwa ujasiri, ushirikiano na jitihada walizofanya kuwaokoa abiria waliozama na ndege hiyo.

“Rais Samia anawatakiwa wanafamilia pamoja na Watanzania wote kwa ujumla subira katika kipindi hiki kigumu. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema peponi. Amin,” inaeleza taarifa hiyo ya Ikulu.

Tayari Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yuko mkoani Kagera na leo Novemba 7, 2022, ataongoza shughuli ya kuaga miili ya waliokufa kwenye ajali hiyo