Watatu wafariki, 28 waokolewa ajali ya ndege Ziwa Victoria

Muktasari:

Ndege ya Shirika la Ndege ya Precision Air iliyopata ajali ya kutumbukia Ziwa Victoria, mita 100 kabla ya kutua Uwanja wa Ndege wa Bukoba, Mkoa wa Kagera imesababisha vifo vya watu watatu na majeruhi.

Bukoba. Watu watatu wamefariki dunia katika ajali ya ndege ya Shirika la Ndege la Precision Air iliyotokea asubuhi ya leo Jumapili, Novemba 6, 2022.

Ni kutokana na ndege hiyo kushindwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba, Mkoa wa Kagera na kutumbukia Ziwa Victoria ambalo lipo karibu na uwanja huo.

Ndege hiyo ilikuwa na watu 43, kati yao 39 wakiwa abiria, marubani wawili na wahudumu wawili ambapo tayari 28 wameokolewa.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Issessanda Kaniki amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo akisema wanaume ni wawili na mwanamke mmoja.

kati ya abiria hao 39 waliokuwa kwenye ndege, watu wazima wapo 38 na mtoto mmoja.

Naye Mkuu wa Mkoa huo, Albert Chalamila amesema Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassimu Majaliwa atawasili Bukoba muda wowote.

Ndege iliyopata ajali ni Precision Air ATR 42 SH PWF iliyokuwa ikitoka jijini Dar es Salaam kwenda Bukoba.

Taarifa ya shirika hilo la ndege imesema, kati ya abiria hao 39, watu wazima ni 38 na mmoja ni mtoto mchanga.

“Timu ya uchunguzi inayojumuisha wafanyakazi wa kiufundi wa Precision Air na TAA (Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania) imeondoa na kujiunga na timu ya uokoaji eneo la ajali,” imesema taarifa ya shirika hilo.


Endelea kufuatilia mitandao yetu kwa habari zaidi