Kijana anayedaiwa kuvamia Kanisa la RC Geita aburuzwa kortini

Jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita. Picha na Rehema Matowo

Muktasari:

Kijana Elpidius Edward (22), mkazi wa Mtaa wa Katundu Wilaya ya Geita anadaiwa kuvamia na kufanya uharibifu kwenye maeneo takatifu na mali yenye thamani ya Sh48.2 milioni ndani ya Kanisa Kuu la Kiaskofu Jimbo Katoliki Geita katika tukio lililotokea Saa 8:00 usiku wa kuamkia Februari 26, 2023.

Geita. Kijana Elpidius Edward (22), mkazi wa Mtaa wa Katundu Wilaya ya Geita anayedaiwa kuvamia na kufanya uharibifu katika Kanisa Kuu la Kiaskofu Jimbo Katoliki la Geita amefikishwa mahakamani akikabiliwa na makosa mawili ya kuharibu mali.

Mshtakiwa huyo aliyefikishwa mahakamani jana Jumatatu Machi 6, 2023 anayedaiwa kutenda makosa hayo Februari 26, 2023 baada ya kuvunja na kuingia kwenye jengo la Kanisa hilo kinyume na kifungu namba 261 (1) na kifungu cha pili cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Mbele ya Hakimu Mkazi, Nyakato Bigirwa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, mshtakiwa huyo anadaiwa kuharibu mali ya Kanisa katoliki Jimbo la Geita yenye thamani ya Sh48.2 milioni.

Akisoma hati ya mashtaka katika shauri hilo namba 62/2023, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Winfrida Ernest ameiambia mahakama kuwa bila uhalali, alisababisha uharibifu wa mali za Kanisa zenye thamani ya Sh 48.2 kinyume cha kifungu namba 326 kifungu kidogo cha kwanza cha Sheria na Kanuni ya Adhabu.

“Februari 26, 2023 katika Kanisa Katoliki Jimbo la Geita, mshatakiwa alivunja na kuingia kwenye Kanisa Katoliki Jimbo la Geita akiwa na dhumuni la kufanya kosa na kuharibu mali kinyume cha kifungu namba 326 kifungu kidogo cha kwanza cha Sheria na Kanuni ya Adhabu,” amesema Mwendesha Mashtaka akisoma maelezo ya mashtaka

Mshtakiwa amekana mashtaka dhidi yake na amepelekwa mahabusu baada ya kukosa dhamana hadi Machi 20, 2023 shauri hilo litakapotajwa tena.

Tukio lilivyotokea

Tukio la uvamizi Kaanisa Kuu Jimbo la Geita lilitokea Saa 8:00 usiku wa kuamkia Jumapili Februari 26, 2023 ambapo kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, kijana aliyehusika ni muumini wa kanisa hilo ambaye pia amewahi kuwa mmoja wa wahudumu kanisani hapo.

Pamoja na kufanya uharibifu katika eneo mimbari (altare), kijana huyo anayedaiwa kuingia kanisani hapo kwa kuvunja kioo cha lango kuu pia anadaiwa kuvunja kiti cha Kiaskofu, misalaba, sanamu za kiimani na vyombo vya kuhifadhia ya maji ya baraka ambayo pia aliyamwaga.