Kijana asimulia alivyofanya ujambazi kwa miaka 19

Kijana Hassan Ally maarufu kama Chiko akihesabu fedha kiasi cha Sh 170,000 alizochangiwa kama mtaji na Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mhandisi Hamad Masauni pamoja na viongozi wengine baada ya kukiri hadharani kuacha ujambazi na matukio mengine ya uhalifu aliyokuwa akiyafanya kwa kipindi cha miaka 19. Picha Hamida Shariff
Mikumi. Haikuwa kazi kwangu kuacha ujambazi, ukabaji, uuzaji wa bangi, gongo na matukio mengine ya uhalifu ilipofikia hatua ya Serikali kunifukuza ndani ya saa 24 katika eneo hili la Mikumi ilibidi nitafakari kwa kina na kulazimika kuacha kufanya matukio hayo ya uhalifu.
Hivi ndivyo Hassan Ally maarufu kama Chiko (54) alivyoanza kumsimulia Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni namna alivyojikuta akiingia kwenye kufanya matukio ya uhalifu ukiwemo ujambazi kwa zaidi miaka 19 na hivyo muda wake mwingi kuupoteza mahabusu na magereza ambako alikuwa akipelekwa kwa makosa mbalimbali.
Chiko ambaye alianza uharifu akiwa na umri wa miaka 20, aliamua kumsimulia Waziri Masauni ambaye juzi alifika eneo la Mikumi kwa lengo la kusikiliza kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Mikumi husasani za kiusalama na huduma zinazotolewa na taasisi zilizokuwa chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani.
Miongoni mwa wananchi waliojitokeza kueleza changamoto na kero zinazowakwaza ni pamoja na Chiko ambaye alidai kuwa amedhulumiwa fedha kiasi cha Sh200,000 na mtu ambay hakumtaja jina baada ya kushindwa kumlipa ujira wake kutokana na kazi ya kulima na kwamba madai hayo alishayafikisha kwa viongozi mbalimbali.
"Waziri Masauni mimi hapa Mikumi hakuna asiyenijua kuanzia wananchi, viongozi na hata polisi kutokana na shughuli zangu za ujambazi, ukabaji, nilikuwa nakata watu mapanga, uuzaji wa bangi, gongo na matukio mengine ya uhalifu niliyokuwa nayafanya miaka ya nyuma, sasa hivi nimeamua kuacha matukio haya, shughuli zangu kwa sasa ni kufanya vibarua vya kulima, kusafisha mitaro na kazi nyingine zinazofanana na hizo, lakini cha kusikitisha huyu jamaa kanidhulumu jasho langu," alisema Chiko.
Allisema kuwa baada ya kufukuzwa na Serikali ya Mikumi mwaka 2008 aliondoka kurudi kijijini kwao Wilaya ya Kilombero kwenye asili yake na akiwa huko aliishi maisha ya kuogopewa na kutengwa kwa kuwa tayari ndugu na majirani walishajua tabia yake. Hivyo aliamua kurudi tena Mikumi kuomba msamaha kwa viongozi wa Serikali na Jeshi la Polisi na kuahidi kutofanya tena matukio ya uhalifu. Hivyo baada ya kusamehewa na kukubaliwa kuendelea kuishi Mikumi aliamua kuacha kabisa vitendo hivyo vya uhalifu.
"Mimi sitaki kurudi kule kwenye yale matukio niliyokuwa nikiyafanya nikiyakumbuka naumia waziri, lakini baadhi ya watu hapa Mikumi wamekuwa wakinijaribu kwa kunidhulumu na wengine kutokuwa na imani nami," alisema Chiko.
Akieleza matukio ambalo aliyafanya huku akijutia kufanya ni matukio hayo ni pamoja na tukio na kumjeruhi mtu mmoja ambaye hamkumbuki jina ambapo baada ya kukamatwa na kufikishwa mahakamani na alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela.
"Tangu nilipoanza ujambazi mwaka 1989 na kuuza bangi na gongo mwaka 1999 mpaka nilipoamua kuacha nimefungwa mara moja kifungo cha mwaka mmoja lakini mahabusu na mahakamani ilikuwa ndio kama nyumbani nilikuwa napelekwa mara kwa mara na nilikuwa nakaa muda mrefu na baadaye naachiwa," alisema Chiko.
Chiko alisema kupata kibanda ambacho kwa sasa anaishi na familia yake, ameoa na katika maisha yake amefanikiwa kupata watoto watano.
Mtoto wake wa kwanza wa kike anasomea udaktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, wa pili kaolewa, wa tatu yupo mtaani hana shughuli yoyote ya kumuingizia kipato, wa nne anasoma kidato cha pili na wa mwisho yupo darasa la nne.
Hata hivyo alisema kuwa watoto wake hao muda mwingi walikuwa wakilelewa na mama yao kwa kuwa yeye alikuwa mahabusu na magereza.
"Nimepoteza muda wangu mwingi mahabusu na magereza sasa hivi naishi maisha magumu sina kazi, biashara wala ujuzi wowote lakini naamini kama ningepata hela kidogo ningeweza kufufua baa yangu ndogo (glosari) niliyokuwa naimiliki, ambapo kwa sasa imekufa kutokana na kutokuwa na mtaji," alisema Chiko
Kufuatia simulizi yake hiyo Waziri Masauni ulimpongeza kijana huyo kwa kuamua kuacha ujambazi na matukio mengine ya uhalifu na kumsihi kutokufikiria kurudia tena matukio hayo licha ya kuwa na maisha magumu anayopitia alimtaka kijana huyo awe raia mwema na alisaidie Jeshi la Polisi kukemea vijana wenzake ambao bado wanajihusisha na vitendo vya uhalifu.
"Kuamua kuacha matukio haya ya kihalifu na kupata ujasiri ya kujitokeza mbele yangu na hadhara hii kwa lengo la kuthibitisha kuwa umeachana na matukio haya. Mimi nakupongeza kwa kuwa utakuwa mfano wa kuigwa kwa vijana wengine ambao mpaka sasa bado wanaendelea kujihusisha na vitengo vya uhalifu na kutusumbua huko mtaani," alisema Waziri Masauni.
Ili kumtia moyo na kumuwezesha kiuchumi Waziri Masauni na viongozi wengine akiwemo mbunge wa Jimbo la Mikumi Denis Londo na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilosa, Amer Mubarak waliamua kumchangia fedha kijana huyo ili ziweze kumsaidia kuanzisha biashara ndogondogo ili aweze kujikimu na kutoshawishika kurudi kwenye uhalifu ambapo kiasi cha Sh 170,000 zilipatikana na kumkabidhi.
Hata hivyo Waziri Masauni alimtaka kijana huyo kuachana kuendelea kumdai huyo mtu aliyedai kuwa anemdhulumu kwa kuwa taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa kijiji ilionyesha hakukuwa na ukweli wowote kuhusu deni hilo.
Baadhi wa wananchi wa Mikumi walieleza namna Chiko alivyokuwa tishio kwa wananchi wa maeneo hayo hata hivyo wanathibitisha kuwa kwa sasa ameacha kufanya matukio ya ujambazi huku wengine wakidai kuwa bado anaendelea na biashara ya kuuza bangi.
"Kwa kweli huyu jamaa kasumbua sana hapa Mikumi, alikuwa anakaba, anapora watu, anaiba mizigo kwenye malori ilifika mahali hatukutamani kumuona tena na ndipo Serikali ya Mikumi na polisi walipomuondoa kwa nguvu na kumpiga maarufu kuoneoana hapa Mikumi.
Kwa upande wake mmoja wa askari polisi ambaye hakutaka jina lake kutajwa, alisema Chiko aliwasumbua sana polisi kila linapotokea tukio la uhalifu miongoni kwa wahalifu wanaokamatwa ni pamoja na Chiko.
"Pamoja na kukiri kuacha matukio ya uhalifu lakini bado jeshi la polisi tunafuatilia kwa karibu mienendo na tabia yake ili kujiridhisha kama kweli ameacha kufanya matukio haya ama anadanganya kwa wananchi na viongozi,” alisema askari huyo.