Kikokotoo chavuruga mkutano CWT, PSSSF

Muktasari:

  • Wajumbe wataka mjadala urudishwe mezani.

Dodoma. Mkutano kati ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma (PSSSF) umevunjika baada ya kuibuka kwa hali ya kutoelewana.

Sababu za kuvunjika kwa mkutano huo ni kikokotoo ambacho baadhi ya wajumbe wa CWT walitaka mjadala urudi upya mezani katika sheria ya Bunge, ili kurudisha asilimia 50, huku wengine wakitaja uongozi wa juu wa walimu kushindwa kuendesha mkutano.

Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho walimnyooshea kidole Kaimu Rais wa CWT, Dinah Mathamani kwamba ameshindwa kuendesha mkutano, ingawa yeye mwenyewe alipinga jambo hilo.

Mmoja wa wenyeviti wa mikoa ya Kaskazini alisema kikao kiliwagomea viongozi wao hata kabla ya kuwasikiliza wataalamu hao kutokana na kutokuwa na imani nao hasa kwenye suala la matumizi ya ofisi.

“Ni kweli tunatiliana shaka, labla mkutano wa Desemba tuje tusemane kwanza, lakini vinginevyo CWT bado haina mchungaji kwa kweli. Tunahitaji kumaliza tofauti zetu,” alisema mwenyekiti huo akiomba kutotajwa jina.

Kaimu Rais wa CWT, Dinah Mathaman alikiri kuwepo na mkutano huo kwa lengo la PSSSF kutoa elimu lakini wajumbe walipinga.

Alisema katika kikao na Rais Samia Suluhu Hassan walikuabaliana viongozi wa vyama kuendelea kutoa elimu juu ya asilimia 33 ya sera ya kikokotoo iliyofikiwa, ili wanachama wapate uelewa.

“Baada ya kufungua mkutano nilitaja ajenda, niliwaambia kubwa ni kuhusu sera ya kikokotoo. Nikawaambia kabla ya kuhoji inabidi tupate elimu kwanza ndio tuendelee na mkutano, hapo ndipo watu walianza kuguna,” alisema Mathamani.

Alisema waliamua kuahirisha mkutano huku wajumbe wakimshinikiza kutoa tamko kwenye vyombo vya habari kushinikiza asilimia 50 badala ya 33 ambayo imefikiwa kwa makubaliano ya serikali na vyama vya wafanyakazi.

Mmoja wa maofisa wa PSSSF waliotajwa kuwepo alikiri kutokea hali hiyo lakini akasema haikuwahusu wao kwani waliitwa na CWT na walipoona hakuna maelewano wakaondoka.