Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kikwete asema wastaafu wameridhika na Dira 2050, amtaja Mbowe

Muktasari:

  • Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 itaivusha Tanzania kutoka kwenye uchumi wa kati wa chini na kuifikisha kwenye uchumi wa kati wa juu.

Dodoma. Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete, amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 itaitoa Tanzania kwenye uchumi wa kati wa chini na kuifikisha kwenye uchumi wa kati wa juu.

Kikwete amepongeza uzinduzi wa Dira 2050 akisema ni hatua kubwa katika historia ya maendeleo ya nchi na kwamba wastaafu, akiwemo yeye, wameridhika na dira hiyo.

Mstaafu huyo ametumia sehemu ya salamu zake kumtupia kijembe cha utani aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.

Kikwete amesema hayo leo Alhamisi, Julai 17, 2025, katika hafla ya uzinduzi wa Dira hiyo katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, ambapo mgeni rasmi ni Rais Samia Suluhu Hassan. Alikuwa akitoa salamu za viongozi wastaafu.

Kikwete amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo inayoishia mwaka huu imeitoa Tanzania kwenye orodha ya nchi maskini duniani na kuifikisha hapa tulipo.

Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2000 hadi 2025 iliyotengenezwa wakati wa Rais wa awamu ya tatu, hayati Benjamini Mkapa, iliitoa Tanzania kwenye kundi la nchi maskini zaidi duniani na kuifikisha kwenye uchumi wa kati wa chini.

"Ni matumaini yetu Dira ya mwaka 2050, ambayo ni dira ya Rais Samia Suluhu Hassan, itatufikisha kwenye kundi la nchi za uchumi wa kati daraja la juu kwa vigezo vinavyotambulika kimataifa, ambapo uchumi unatakiwa kufikia Dola za Marekani 4,500," amesema.

Kikwete amesema kundi la viongozi wastaafu nchini wanaona hilo linawezekana kutoka kwenye uchumi wa kati wa ngazi ya awali na kwenda kwenye uchumi wa kati kwenye ngazi ya juu.

Amesema kama wapo walioweza, basi na Watanzania wanaweza, na akahoji kwa nini ishindikane wakati kila kitu kipo cha kuwezesha hayo mambo, na kwamba ikifikia hapo, Tanzania itakuwa pazuri.

Amepongeza mpango wa kuandaa Dira ya 2050 sambamba na kuandaa mpango wa utekelezaji wake, akisema hatua hiyo ni muhimu, kwani itaharakisha utekelezaji na matumaini makubwa ya malengo, tofauti na ilivyokuwa kwenye dira ya mwaka 2000.

"Tunatoa pongezi nyingi kwako kwa uamuzi wa busara wa kutaka Tanzania kuwa na dira ya maendeleo ya miaka 25 kutoka mwaka 2025 hadi mwaka 2050.

Uamuzi huu umethibitishia wazi sisi wazee wastaafu, Watanzania wenzetu, na hata ulimwengu kwa ujumla kuwa wewe ni kiongozi makini mwenye maono ya mbali na mwenye mapenzi makubwa kwa nchi yako," amesema.

Ametaja kuwa mchakato wa kutayarisha Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050 ulivyoendeshwa umefanyika kwa weledi wa hali ya juu na ulikuwa shirikisho na jumuishi.

Katika hatua nyingine, Kikwete amegusia historia ya kisiasa ya Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Mipango na Uwekezaji, akisema: "Lakini labda niseme kitu kimoja, unajua huyu pengine aliteleza tu.

“Huyu Kitila Mkumbo alikuwa Mwenyekiti wa Vijana wa CCM Mkoa wa Singida, sijui Mbowe (Freeman Mbowe) alikuja kumdanganya nini yule pale. Kwa hiyo haya anayoyafanya sasa ni ya ki-CCM. CCM anakumbuka kule alikotokea.”

Kauli hiyo iliwafurahisha washiriki wa hafla hiyo, akiwemo Mbowe mwenyewe. Profesa Kitila aliwahi kuwa mwanachama wa Chadema kabla ya kuondoka kwenda ACT-Wazalendo na baadaye kurejea CCM.