Kikwete ataka kuondoshwa vizuizi ili kilimo kistawi Afrika

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete akihutubia katika Mkutano wa saba ALF unaofanyika jijini Accra, Ghana. 

Muktasari:

  • Rais huyo Mstaafu amekiri kuwa serikali za Afrika zimekuwa zikifanya juhudi mbali mbali kwa ajili ya wakulima wadogo, lakini pia wadau wengine ili kubadilisha hali ya kilimo barani Afrika na kwamba tayari kuna maendeleo makubwa yaliyofikiwa na mafanikio mengi yamepatikana.

Accra. Rais Mstaafu Jakaya Kikwete amesema sekta ya kilimo barani Afrika, haijafanya vizuri kutokana na vizuizi vingi, huku akitoa wito kwa wadau kuwa mjadala ambao utafungua uwezo wake na hivyo kuondokana na upungufu wa chakula, njaa na umaskini.

Akizungumza katika Mkutano huo wa Uongozi wa Afrika (ALF) ambao umeanza jana Mei 24 2023, Kikwete ambaye ni Mlezi wa taasisi hiyo, amesema, sekta hiyo inachangia sehemu kubwa ya pato la Taifa na mapato ya fedha za kigeni kwa barani Afrika.

“Hakuna sekta inayoajiri watu wengi kama kilimo, lakini bado haijafikia uwezo wake timilifu, kwahiyo; kujadili jinsi ya kufungua uwezo wake ni jambo sahihi kufanya. Hii itasaidia nchi za Afrika kuunganisha nguvu ili kuondokana na umasikini, upungufu wa chakula na njaa,” amesema.

Rais huyo Mstaafu amekiri kuwa serikali za Afrika zimekuwa zikifanya juhudi mbali mbali kwa ajili ya wakulima wadogo, lakini pia wadau wengine ili kubadilisha hali ya kilimo barani Afrika na kwamba tayari kuna maendeleo makubwa yaliyofikiwa na mafanikio mengi yamepatikana.

"Hata hivyo, kuna mengi zaidi yanahitajika kufanywa ili kilimo kiweze kuchangia kikamilifu katika ukuaji na maendeleo ya mataifa ya Afrika, ikiwa ni pamoja na ustawi na utajiri wa Waafrika,” amesema na kuongeza;

"Mpaka sasa mambo yamekwenda vizuri lakini bado hayatoshi kama inavyothibitishwa na kiwango cha umasikini katika maeneo mengi ya vijijini ambapo watu wetu wengi wanaishi na ripoti zisizoisha za watu kusumbuliwa na ukosefu wa chakula na njaa barani Afrika." alisema.

Kikwete hafurahishwi na ripoti zenye kuonyesha Afrika inatumia kiasi kikubwa cha fedha za kigeni kununua chakula, na kwamba bado Afrika inauza malighafi za kilimo kwa nchi zilizoendelea kisha kununua bidhaa zilizotengenezwa kutokana na malighafi hizo.

"Tunahitajika kuwekezaji kwa watu wetu hasa wakulima wadogo na vijana wetu, uwekezaji katika taasisi na miundombinu yetu ili kuhakikisha mazingira mazuri ya kufanya biashara yanapatikana na kulitumia Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) kama sehemu ya Afrika kujitanua kiuchumi,” ameshauri Mlezi huyo wa ALF.

Awali akifungua mkutano huo, Rais wa Ghana, Nana Addo Dankwa Akufo-Addo, amesema biashara ndani ya Afrika ni moja ya mambo yalicho chini katika eneo hilo na kwamba inachangiwa na uwezo mdogo wa uzalishaji.

"Kuna nguvu katika umoja. Ikiwa nchi zote 54 zenye watu bilioni 1.3 na Pato la Taifa la dola trilioni 3 zitashirikiana, hii ni fursa kubwa ya ukuaji na kukabiliana na ongezeko la bei na kutokuwa na uhakika wa yanayotokea kwenye masoko ya kimataifa." alisema.

Alisema kuwa kwa kuwa AfCFTA inatoa fursa kwa sekta binafsi, Serikali lazima ziwe na ujasiri lakini pia kuwa mikakati yenye lengo ili kuijengea thamani kubwa Zaidi.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa AfCFTA, Wamkele Mene, amebainisha kuwa Afrika bado ni bara linalonunua chakula kutoka nje kwa kiwango kikubwa, na gharama ya kununua chakula kutoka nje ilifika dola bilioni 80 kati ya mwaka 2015 na 2017.

"Tunahitaji kufungua uwezo wa jamii zetu za vijijini ili kuwa sehemu ya mnyororo wa thamani wa kimataifa na kuwezesha wakulima wadogo kuwa sehemu ya biashara ya kimataifa. Kwa kutambua jukumu la sekta binafsi na biashara zinazomilikiwa na wanawake, AfCFTA imetoa kipaumbele kwa kilimo na usindikaji." alisema.

Akitoa muktadha wa kikao cha jumla, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekele alisema soko la kilimo la Afrika bado limegawanyika na kusambaa.

Aliomba taasisi za kifedha kushirikiana katika soko kama sehemu ya suluhisho la upatikanaji wa fedha za kusaidia mifumo ya kilimo barani Afrika

Viongozi na washiriki wengine walibainisha kuwa Afrika ina ardhi ya kutosha kwa kilimo ambayo inaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji na maendeleo ya bara hilo, ikishikilia zaidi ya nusu ya ardhi ya kilimo duniani na rasilimali kubwa za maji zenye uwezo wa kutosha kwa umwagiliaji.

Viongozi wengine wa Kiafrika waliohudhuria ni pamoja na Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, Rais wa zamani wa Tunisia Dr Mohamed Marzouki, Rais wa zamani wa Nigeria Dr Goodluck Jonathan, Rais wa zamani wa Benin, Thomas Yayi.

Wengne ni Rais wa zamani wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia, Hailemariam Boshe, na Rais wa zamani wa Sierra Leone Dr Ernest Koroma.