Kikwete mwenyekiti mpya tuzo za AFP

Kikwete mwenyekiti mpya tuzo za AFP

Muktasari:

  • Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete ametangazwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Tuzo ya Chakula Afrika (AFP) akipokea kijiti kutoka kwa Rais mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo aliyeiongoza taasisi hiyo tangu mwaka 2016.

Dar es Salaam. Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete ametangazwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Tuzo ya Chakula Afrika (AFP) akipokea kijiti kutoka kwa Rais mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo aliyeiongoza taasisi hiyo tangu mwaka 2016.

AFP ni tuzo inayowatambua wanawake, wanaume na taasisi zilizo mstari wa mbele na michango yao katika kilimo cha Kiafrika inaanzisha enzi mpya ya usalama endelevu wa chakula na fursa ya kiuchumi ambayo inawainua Waafrika wote.

Akitoa salamu za kumkaribisha mrithi wake leo Februari 17, Mwenyekiti anayemaliza muda wake, Obasanjo ameonyesha furaha akibainisha kwamba kupitia kazi yake, Kikwete ameonyesha ari ya dhati katika kuleta mageuzi ya kilimo barani Afrika.

 “Nampongeza Kikwete kwa kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa Tuzo ya Chakula Afrika. Kupitia uongozi wake, nina imani kuwa bara hili litaendelea kuchunguza na kutekeleza mikakati ya mifumo ya chakula ambayo itawaondoa watu kutoka kwenye umasikini kupitia ukuaji jumuishi na maendeleo endelevu,” amesema Obasanjo.

Dk Kikwete ana rekodi ya kuchangia katika mabadiliko ya mifumo ya chakula barani Afrika. Akiwa Rais wa Tanzania, aliongoza utekelezaji wa ‘Kilimo Kwanza’, mpango ambao ulifungua tija na faida kwa wakulima wadogo nchini.

Pia, aliongoza utekelezaji wa Ukanda wa Kukuza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi unaolenga kufungua uwekezaji zaidi wa sekta binafsi katika sekta ya kilimo nchini.

Alipostaafu na kupitia Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete, kiongozi huyo amekuwa akishirikiana na wakulima na watafiti kuandaa mipango na afua za kimkakati ili kuongeza mavuno na tija kwa wakulima wadogo na biashara ya kilimo.

Uteuzi wa Kikwete unakwenda sambamba na wito wa uteuzi wa Tuzo ya Chakula Afrika wa Dola za Marekani 100,000 kwa mwaka 2023.

Mwaka huu, Nestlé ilishirikiana na Tuzo ya Chakula Afrika na kuchangia Dola za Marekani 108,400 (sawa na Sh253.6 milioni) ambazo zitatolewa kwa ajili ya tuzo, hasa kipengele maalumu kinachozingatia ubunifu unaoendeleza mifumo ya uzalishaji wa chakula.

 “Tunafurahi kuona jinsi waombaji wa mwaka huu wa Tuzo ya Chakula Afrika wanavyoleta mabadiliko.

“Utafiti wao na juhudi za uvumbuzi zitasaidia kuleta mabadiliko ya kilimo katika bara la Afrika na tunajivunia kuunga mkono hili,” amesema Remy Ejel, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kanda ya Asia Oceania na Afrika wa taasisi ya Nestlé.