Kilicho nyuma ya miradi Chato -3

Aprili 14 mwaka huu waandishi wanne nguli—Absalom Kibanda, Ansbert Ngurumo, Neville Meena na Jesse Kwayu walizindua kitabu chao walichokipa jina la 'I am the State: A President's Whisper from Chato'.

Leo tunafanya mapitio ya sura ya tatu ya kitabu hicho inayoitwa ‘The Dilemma of I am a State’, ambayo kwa tafsiri isiyo rasmi ni ‘Mtanziko wa 'Mimi Ndiye Dola'.

Kitabu kinaianza sura hiyo kwa kulinukuu gazeti la ‘The Citizen’ la Machi 19, 2021—ikiwa ni siku mbili baada ya tangazo la kifo cha Rais John Magufuli—liliandika makala yenye kichwa kilichosomeka: "Maisha Chato bila mwana mpendwa Magufuli."
Pamoja na mambo mengine mengi, makala hiyo iliyoandikwa na Peter Saramba na Rehema

Matowo iligusia hofu iliyowakumba wakazi wa Chato juu ya uwezekano wa kuporomoka kwa miradi mingi iliyoanza wakati wa utawala wa Rais Magufuli.

Katika sura hiyo, kitabu kinazungumzia kile kilichokiita “Historia ya wazimu wa miundombinu na ubinafsi wa Chato….”

Kinasema wazimu huo unaanzia enzi zile marehemu Magufuli alipoteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Miundombinu na Rais Benjamin Mkapa mwaka 1995.

Alipokuwa mbunge wa jimbo la Biharamulo Mashariki, alishiriki katika kubadilisha uamuzi wa Serikali kuhusu ujenzi wa barabara ya lami hadi jimbo jirani la Biharamulo Magharibi.
Barabara hiyo ilikusudiwa iende moja kwa moja hadi Biharamulo Magharibi, lakini iligeuzwa njia ili ipite katika mji wa Chato.

‘I am the State’ kinasema “kitendo hiki cha kuchukiza” ambacho kilipangwa na Magufuli wakati akiwa Waziri wa Ujenzi, kilizua tafrani iliyoongozwa na mbunge wa Biharamulo Magharibi, Anatory Choya.

Kwa kauli na matendo yake, Magufuli alitaka kuthibitisha kuwa watangulizi wake wanne walishindwa lilipokuja suala la kuifanya Chato kuwa eneo maarufu alikozaliwa rais, likiizidi Butiama ya Julius Nyerere (Musoma Vijijini), Lupaso ya Benjamin Mkapa (Masasi) na Msoga ya Jakaya Kikwete (Chalinze).

Kwa hakika, maeneo ya kuzaliwa kwa marais hao waliotajwa hapo juu yanafanana sana na vijiji vya kawaida vya Tanzania, lakini sivyo ilivyo kwa Chato ambayo miradi mingi ilifanyika katika kipindi kifupi alichokaa madarakani.

Pamoja na kwamba kuna eneo zimewekwa taa za barabarani za kuongozea magari, ni magari machache hupita eneo hilo na kinasema kitabu hicho kuwa nusu saa ambayo timu ya uchunguzi ilikaa barabarani ilipita bila kupita gari lolote.

Waandishi hao wakongwe kupitia kitabu chao wanaona kuwa taa za kuongozea magari kwenye makutano ya Barabara ya Mwanza-Bukoba kuelekea Chato mjini ni ubadhirifu mkubwa wa rasilimali kwa vile hakuna magari Chato yanayolazimu kuwapo kwa matumizi ya taa.

Wanasema Wilaya ya Chato ambayo kwa viwango vyote ni eneo jipya la utawala ina takriban kilomita 35 za barabara za lami, ambazo ni mbali zaidi ya makao makuu mapya ya mikoa kama Bariadi, Babati, Geita na Vwawa. Makao makuu ya mkoa wa Geita yana barabara za lami zenye urefu wa kilomita 22.

Waandishi hawa wanaandika kuwa utawala wa Rais Magufuli ulikuwa na ubavu wa kutumia mabilioni ya fedha za walipakodi katika miradi ambayo ingeitukuza tu Chato, lakini haikuwa na faida yoyote katika uwekezaji.

Hii inahusu pia stendi ya mabasi ya daladala yenye urefu wa mita 100 x 75 na inakadiriwa kuchukua hadi mabasi madogo 108, huku kumbukumbu zikionyesha kuwa chini ya mabasi 20 yanapita barabarani katika eneo hilo.

Vibanda vingi vya biashara vilivyojengwa karibu na jengo hilo havikaliwi, kwani wateja watarajiwa wanalalamika kwamba hakukuwa na biashara ya kuwawezesha kulipa kodi ya Sh50,000 kwa mwezi kwa kila duka.

Kati ya vibanda 50 ni 19 pekee vilivyokuwa na wapangaji kufikia Novemba 2022. Muundo wa kituo kikuu cha mabasi ni mita 200 x 150 na inakadiriwa kuchukua mabasi 130 yote katika Chato.

Asili ya ufumbo wa Rais Magufuli inaweza kulinganishwa na Mfalme Luis wa 16 aliyetawala Ufaransa hadi kilele chake cha kutawala katika mamlaka kamili, kwa kuinuliwa: ‘L'etat c'est moi' kumaanisha 'Mimi ni Dola’ au “Dola ni Mimi.”

Wazo la kuanzisha Chato kuwa mkoa mpya lilijitokeza katika kipindi cha miaka miwili au mitatu iliyopita kabla ya kifo cha Magufuli.

Mkoa wa Chato ulikusudiwa kuunda wilaya za Chato, Bukombe na Kakonko kutoka mkoa wa sasa wa Geita na wilaya nyingine mbili za Biharamulo na Ngara kutoka Mkoa wa Kagera.

Kitabu hicho kinakosoa pia hatua ya Rais Magufuli kujenga lango kuzunguka Pori la Akiba la Burigi ambalo sasa linaitwa Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato huko Chato wakati kijiografia, Burigi iko Biharamulo. Wanakosoa pia ujenzi wa ofisi kuu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kituo "maridadi" cha mabasi, mnada wa mifugo na machinjio, hospitali ya kanda na miradi mingine ndani ya takriban kilomita 120 kati ya Chato na makao makuu ya mkoa wa Mwanza.

Kwa kutazama yote hayo, waandishi wa kitabu cha ‘I am a State’ wanajikuta wakihitimisha wakisema hivi: “Huu ni ubadhirifu.”

Hata hivyo, kitabu kimewamwagia sifa za shukrani Profesa Anna Tibaijuka, Askofu Dk Benson Bagonza na Askofu Severine Niwemugizi waliojitokeza hadharani wakati Rais Magufuli na wafuasi wake walipotoka na wazo la kuipandisha hadhi ya Wilaya ya Chato kuwa ya Mkoa.

Askofu Bagonza aliufananisha uamuzi huo na mimba iliyotungwa nje ya kizazi ambayo inatishia maisha ya mtoto mchanga na mama yake.

Askofu Niwemugizi alisema pendekezo hilo linazingatia matakwa ya watawala na si ya watawaliwa. Kwa upande wake, Profesa Tibaijuka aliweka bayana zaidi aliposema pamoja na takwimu kwamba Chato haikukidhi hata mahitaji ya chini kabisa ya kupandishwa kwake hadi hadhi ya mkoa.

Hatimaye wazo hilo halikufanikiwa. Utafiti wa kitabu hicho ulibaini kuwa takriban miaka miwili baada ya kifo cha Magufuli, Oktoba 2022, Baraza la Ushauri la Mkoa wa Geita (RCC) liliamua kwamba maombi ya Wilaya ya Geita ya kutaka kuwa mkoa wa kiutawala yalitolewa kabla ya wakati wake na hayana nguvu.

Uamuzi huo wa RCC ulikuwa mwiba kwa azma ya Magufuli ya muda mrefu, na ni uthibitisho kwamba hiyo ilikuwa ni dhamira binafsi iliyonyauka na kufa bila kutarajiwa.

Pamoja na hayo yote, kitabu hicho kinasema gharama ya miradi ya Chato bado ni mzigo kwa Serikali ya Samia Suluhu Hassan kwa sababu utekelezaji wa miradi mingine unaendelea.

Kitabu hicho kinatolea mfano kuwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule alipotembelea soko la mnada wa mifugo katika Kijiji cha Buzilayombo Chato Mei 2022, alisema tayari Serikali imetumia Sh3.1 bilioni kati ya Sh4.8 bilioni 4.8 kukamilisha ujenzi wa awamu ya kwanza.

Kisha inakuja sura ya nne ya kitabu inayoitwa ‘The Chato Referral Hospital: Where patients can’t easily access’ (Hospitali ya Rufaa ya Chato: Eneo gumu kufikiwa na wagonjwa).
Tukutane kesho kuendelea na mapitio ya sura hiyo.