Magufuli alivyosukuma Uwanja wa Ndege Chato

Miaka miwili tangu Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli alipoaga dunia, waandishi wanne wakongwe nchini—Absalom Kibanda, Ansbert Ngurumo, Neville Meena na Jesse Kwayu—wameandika na kuzindua kitabu kinachoangazia sehemu ya utawala wake, hasa jinsi miradi mikubwa ilivyojengwa Chato na kuchipua kwa kasi; na jinsi baadhi yake ilivyoanza kunyauka.

Kitabu hicho kilichopewa jina la 'I am the State: A President's Whisper from Chato' ambacho tafsiri isiyo rasmi 'Mimi ndiye Dola: Mnong'ono wa Rais kutoka Chato' kinachoonyesha sura ya kiongozi huyo na uwekezaji huo wa miaka mitano na miezi mitatu kabla hajafikwa na mauti.

Akizindua kitabu hicho Aprili 14 mwaka huu, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Dk Benson Bagonza alisema kinaonyesha namna fedha za umma zilivyotumika nje ya bajeti ya Serikali na kwamba, "mambo yaliyotajwa katika kitabu hiki yalitendeka nchi ikiwa gizani, watu walinyamazishwa na haya yaliyoandikwa ni sehemu ndogo ya yaliyotendeka nchi ikiwa gizani."

Katika sura ya kwanza ya kitabu hicho mengi yameandikwa na katika mapitio haya tutatazama tu baadhi ya mambo yaliyoguswa na kuyaacha yale mengine.

Katika aya ya kwanza ya sura hiyo, unakutana na sentensi moja fupi inayosomeka “Hukujua jambo hili”. Kwamba wazo la ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Chato lilibuniwa, likaibuliwa, likaendelezwa na kutekelezwa na Rais John Magufuli mwenyewe.

Kitabu kinasema Dk Magufuli aliingia madarakani Novemba 5, 2015 na miezi tisa tu baadaye, Agosti 31, 2016, Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ilisaini mkataba na Kampuni ya Mayanga Contractors Co. Ltd kujenga uwanja huo.

Uwanja mkubwa zaidi wa ndege nchini ni ule wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) uliopo Dar es Salaam, kinasema kitabu hicho, kwamba unafuatiwa na wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Uwanja wa Chato, au Geita kama unavyoitwa sasa, unatajwa na kitabu hicho kuwa ni wa tatu kwa ukubwa baada ya JNIA na KIA.

Kitabu kinabainisha kuwa viwanja vya ndege vya Mwanza na Arusha vilivyoshika nafasi ya tatu na nne baada ya JNIA na KIA katika kuhudumia abiria na mizigo, vina njia za kurukia ndege zenye urefu wa kilomita 3.0 (Mwanza) na 1.8 (Arusha) mtawalia; huku Chato iliyopo jirani na Uwanja wa Ndege wa Mwanza na isiyo na biashara wala rasilimali za kujivunia, nayo ina njia ya kurukia ndege yenye urefu wa kilomita 3.0.

KIA, yenye shughuli nyingi na hadhi ya kimataifa, ina njia ya kurukia ndege yenye urefu wa kilomita 3.6, ikiwa ni mita 600 tu kuizidi Chato.

Waandishi wa kitabu wanahoji, kwa nini viwanja vya ndege vya mikoani vilivyo na uwezo mkubwa na shughuli nyingi havikupewa umuhimu ukilinganisha na Chato, ambao hauhudumii shirika lolote la ndege zaidi ya Air Tanzania Corporation Limited (ATCL)?

Katika uchunguzi wao, waandishi hao wanasema waligundua kuwa ni viwanja vya ndege vichache kati ya 59 kote nchini vina njia za kutegemewa za kurukia ndege.

Wanasema mbali na viwanja vya JNIA, KIA, Mwanza na Songwe, ambavyo vinamudu kutua ndege kubwa kama Boeing 787-8 Dreamliner na Airbus A220-300, ni Uwanja wa Chato pekee ambao umejengwa na kuendelezwa ili uwe na uwezo wa kuhudumia ndege kama hizo, lakini sivyo ilivyo kwa viwanja vingine vilivyosalia.

Kitabu kinachambua kuwa viwanja vyote vikubwa nchini vilivyojengwa kati ya mwaka 1940 na 2012 viko katika makao makuu ya mikoa husika, isipokuwa wa Chato (Geita Airport) ulioko katika ngazi ya wilaya.

Kwanza, wanasema Tanroads kwa zaidi ya mwongo mmoja ilikuwa chini Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi; na kampuni ya ujenzi ya Mayanga Contractors Co. Ltd ilipewa zabuni nyingi katika miradi inayohusiana na Chato.

Kitabu kinamtaja kiongozi wa kampuni hiyo, kwamba alikuwa mwanafunzi mwenzake wa zamani Magufuli katika Shule ya Sekondari ya Lake, Mwanza (1977-78).

Waandishi wanachambua kwamba Chato ni kijiji alichozaliwa Rais Magufuli, kikiwa kitongoji kidogo katika mwambao wa Ziwa Victoria mkoani Geita, zaidi ya kilomita 120 kutoka jijini Mwanza.

Wameandika kuwa wakati viwanja vya ndege vikongwe na vyenye shughuli nyingi kama Kigoma, Tabora na Mwanza vikihangaika kupata ufadhili wa Serikali kuboresha njia zao za kurukia ndege na vifaa vingine, ule wa Chato ulipata fedha kwa kasi na ndani ya miaka mitatu kazi yote ya awali ilikuwa imekamilika.


Baraka za Bunge

Waandishi hao wanaeleza kwamba tatizo ni ule ukweli wa kwamba, kwanza, ujenzi wa uwanja wa Chato ulianza bila kupitishwa kibajeti na Bunge; pili, mkandarasi alichaguliwa na Rais kinyume cha sheria na taratibu za manunuzi; na tatu, ujenzi ulianza bila upembuzi yakinifu.

Kwa kutumia marejeo ya kumbukumbu za Bunge, waandishi wameandika jinsi mhimili huo ulivyoelezwa kuwa pamoja na kuwa Serikali kupanga kutumia Sh39 bilioni kwa ajili ya uwanja, Hazina ilitenga zaidi ya Sh50 bilioni hadi Machi 2018 bila kulihusisha Bunge.

Kitabu hicho pia kimetumia ripoti ya CAG kufafanua hoja kuhusu uwanja huo wa Chato. Kinasema miaka mitano baadaye, Ripoti ya CAG 2020/2021 ilibainisha kasoro kadhaa katika utekelezaji wa mradi huo; na kufichua kuwa upembuzi yakinifu wa mradi haukuwahi kufanywa kabla ya mradi kuanza.

Mbali na kasoro hizo, kitabu hicho kinabainisha kinachotajwa ni ushahidi wa kuwepo marufu ya matumizi mabaya katika ujenzi wa mradi huo.

Wametaja kuwapo “matumizi makubwa zaidi ya bajeti iliyoidhinishwa” kwa mradi husika, kwamba zilifikia Sh52.32 bilioni ikiwa ni mara tatu ya bajeti yake ya awali iliyoidhinishwa ya Sh17.79 bilioni, yaani ongezeko la asilimia 194.

Kitabu kinasema hata kama ATCL inayotumia uwanja huo, itajaribu kufufua biashara yake, njia ya Chato haionekani kuwa na manufaa makubwa, kikibainisha ni abiria wachache wa ndege wanaoingia na kutoka Chato wakijaribu kuulinganisha na Gbadolite wa Mobutu Sese Seko wa Zaire (sasa DRC), ambayo ilififia baada ya kifo chake.

Katika ulinganisho huo, wanasema, “wakati Mobutu aliwezesha kutua Concorde huko Gbadolite, Rais Magufuli aliwezesha Airbus A200-300 kutua Chato; Mobutu aliwaalika Papa John Paul II, Rais wa Ufaransa Valery Giscard d'Estaing na Mfalme wa Ubelgiji huko Gbadolite; Rais Magufuli alimkaribisha waziri wa mambo ya nje wa China na viongozi mbalimbali katika mji wake wa Chato.

Pia maeneo yote mawili, waandishi wanasema yalikaribia kuwa Ikulu za nchi husika.

Kesho tutaangalia Sura ya Pili inayoitwa ‘Chato: A Village that Almost Became Regional Headquarters’ (Chato: Kijiji kilichokaribia kuwa Makao Makuu ya Mkoa).