Maisha Chato bila John Magufuli
Muktasari:
Ni jambo gumu kupokea na kulikubali. Lakini ndiyo hivyo Mungu ameamua kwamba kuanzia Machi 17, 2021, wakazi wa Kijiji cha Mlimani, mji na Wilaya ya Chato wataishi bila kijana, mpendwa, ndugu na shujaa wao John Magufuli.
Mwanza/Chato. Ni jambo gumu kupokea na kulikubali. Lakini ndiyo hivyo Mungu ameamua kwamba kuanzia Machi 17, 2021, wakazi wa Kijiji cha Mlimani, mji na Wilaya ya Chato wataishi bila kijana, mpendwa, ndugu na shujaa wao John Magufuli.
Kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, umaarufu wa Kijiji cha Mlimani, mji na Wilaya ya Chato ulikuwa wa kawaida kama vilivyo vijiji, miji na wilaya nyingine za pembezoni nchini.
Lakini baada ya John Magufuli kuingia madarakani, Kijiji cha Mlimani na Chato kwa ujumla siyo tu vimekuwa maarufu, bali pia vimebadilika na kuwa maeneo maalumu na muhimu kisiasa na kijamii.
Umaarufu huo umetokana na eneo hilo kuwa nyumbani kwa Rais John Magufuli na hivyo kupata fursa kadhaa kisiasa, kiuchumi, kijamii na kimaendeleo.
Miradi ya maendeleo
Katika kipindi cha miaka sita iliyopita Wilaya ya Chato imeshuhudia utekelezaji wa miradi kadhaa ya maendeleo ambayo haikuwahi kushuhudiwa hapo kabla.
Miongoni mwa miradi ambayo imeanzishwa au kukamilika na kuzungumzwa sana ni ujenzi wa Uwanja wa ndege, Hospitali ya Rufaa ya Kanda, Chuo cha ufundi (Veta), moberesho ya soko la dagaa Kasenda, ujenzi wa uwanja wa mpira, kituo kikuu cha mabasi, vibanda vya biashara kwa ajili ya wajasiriamali na minada ya mifugo.
Katika kipindi hicho, Chato pia imeshuhudia ununuzi na ujenzi wa vivuko vya Chato na Rubondo bila kusahahu kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato pamoja na shamba la miti la Silayo.
Wageni wa kitaifa, kimataifa
Katika kipindi cha uongozi wa Rais John Magufuli kijiji cha Mlimani, mji na Wilaya ya Chato imepata fursa ya kutembelewa na viongozi kadhaa wa kitaifa na kimataifa waliofika kwa mazungumzo na kiongozi huyo wakati wa likizo zake fupi alizokwenda nyumbani.
Ujio wa wageni hao si tu ulikuwa neema kwa Taifa, bali pia kwa wakazi wa Mlimani na Chato ambao uchumi wao ulichemshwa kwa kuwapo shughuli za kibiashara na ongezeko la mzunguko wa fedha.
Neema ya wageni ambayo bila kuwapo Rais Magufuli wasingekwenda Chato, ilihitimishwa na ziara za viongozi mbalimbali waliomtembelea Rais Magufuli nyumbani kwake mwanzoni mwa mwaka huu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, Wang Yi aliyefika Chato Januari 7, ni kati ya wageni wa Kimataifa waliofika kijiji cha Mlimani iliko Ikulu ndogo ya Chato.
Waziri Wang Yi aliyefanya ziara ya siku mbili nchini alipata fursa ya kushiriki shughuli kadhaa, ikiwamo kufungua chuo cha ufundi stadi (Veta) ambacho nchi yake iliahidi kuisaidia Tanzania kupata watu wenye ujuzi na stadi kufikia lengo la maendeleo ya sekta ya viwanda ifikapo 2025. China iliahidi kuchangia Sh350 milioni kusaidia chuo hicho.
Akiwa Chato, Waziri Wang Yi alitembelea mwalo wa samaki wa Chato ambako alitangaza neema kwa kuridhia Tanzania kuuza mabondo ya samaki aina ya sangara moja kwa moja China, tofauti na awali ambapo wafanyabiashara walilazimika kupitia jimbo la Hong Kong ambako bei ni ndogo ikilinganishwa na China.
Ziara ya waziri huyo haikuwa tu na lengo la kuishia Chato, bali kiongozi huyo alishuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa kipande cha Reli ya Kisasa (SGR) kati ya Mwanza na Isaka, chenye urefu wa kilomita 341, mradi unaotekelezwa kupitia kampuni mbili za China kwa gharama ya zaidi ya Sh3.067 trilioni.
Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi naye alifanya ziara Januari 11, 2021 wilayani Chato kuonana na Rais Magufuli, alipata fursa ya kuweka jiwe la msingi la Hospitali ya Kanda ya Chato itakayohudumia zaidi ya watu 14 milioni kutoka mikoa ya Tabora, Kagera, Shinyanga, Kigoma, Mwanza, Rukwa na Geita.
Rais wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde naye amefika Chato katika ziara yake ya Januari 25, ambapo aliahidi Ethiopia kushirikiana na Tanzania kibiashara na uwekezaji huku Tanzania ikipata fursa ya kufundisha lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Adis Ababa.
Januari 14 wananchi wa Chato walipata ugeni mwingine mkubwa wa kitaifa wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Dk Hussein Mwinyi, aliyeambatana na Makamu wake wa Kwanza, Hayati Maalim Seif Sharif Hamad kumtembelea na kufanya mazungumzo ya faragha na Rais Magufuli.
Uwepo wa Rais Magufuli katika mapumziko nyumbani kwake Chato haukuwanufaisha wenyeji kwa ujio wa wageni wa kimataifa na kitaifa pekee, bali pia kuchangamka kwa shughuli za kibiashara na kiuchumi kutokana ongezeko la watu wenye uwezo wa manunuzi.
Wafanyabiashara waliuza bidhaa na huduma na hivyo kuongeza kipato chao. Faida ambazo sasa huenda zikakoma au kupungua baada ya kiongozi huyo kufariki dunia.
Elias Kaswahili, mmoja wa watu waliosoma pamoja na Rais Magufuli enzi ya utoto wao, ni kati ya wakazi wa Chato wenye huzuni na majonzi makubwa kwa kifo hicho.
“Kifo cha Magufuli ni pigo kwa wana Chato. Kiatu chake hakiwezi kumtosha mtu mwingine. Jambo pekee tulilobaki nalo ni kumwomba Mungu atupe utulivu,” anasema Kaswahili, aliyefahamiana na Magufuli tangu mwaka 1964 wakati wakisoma Shule ya Msingi Chato.
“Tuna masikitiko makubwa. Tumepata taharuki wakati Makamu wa Rais akihutubia, mji huu ulisikika sauti za vilio kila eneo. Magufuli ameinyanyua Chato, ameifanya ijulikane. Kilikuwa kijiji lakini sasa ni wilaya yenye mafanikio na maendeleo,” anasema.
Maisha Chato bila Magufuli
Ni kutokana na mafanikio hayo, Samuel Bigambo, mwenyekiti wa Baraza la Wazee Wilaya ya Chato anawasihi viongozi, hasa mrithi kiti cha Urais, Samia Suluhu Hassan kumuenzi mtangulizi wake kwa kuendeleza miradi na mipango yote ya maendeleo ya Chato.
“Tunaomba miradi ya maendeleo, ikiwamo ujenzi wa hospitali ya Kanda, uwanja wa ndege Chato na mengine katika sekta za elimu, afya na barabara iendelezwe kama njia ya kumuenzi Hayati Rais Magufuli,” amesema Bigambo.
Mwendesha pikipiki ya abiria mjini Chato, Emmanuel John amesema kifo hicho kimeacha simanzi na kufifisha nuru ya matumaini miongoni mwa wana Chato ambao wameingiwa hofu ya kukwama kwa miradi ya maendeleo iliyoanzishwa na kiongozi huyo.
“Tunamuachia Mungu, kwani ndiye anayejua yajayo. Lakini daima Chato tutamkumbuka Magufuli kwa yote tangu akiwa mbunge hadi Rais,” amesema John.