HOJA ZA KARUGENDO: Mama Samia Rais wetu, ponya na karabati

HOJA ZA KARUGENDO: Mama Samia Rais wetu, ponya na karabati

Muktasari:

  • Wakati tunaendelea kumlilia na kumsindikiza kwenye nyumba yake ya milele Rais John Magufuli na kumkaribisha Mama yetu, Rais Samia Suluhu Hassan, nimuhimu kujikumbusha yaliyo mbele yetu. Nasema kukarabati ni muhimu bila kigugumizi kuwa huu ni wakati wa kuponya na kukarabati.

Wakati tunaendelea kumlilia na kumsindikiza kwenye nyumba yake ya milele Rais John Magufuli na kumkaribisha Mama yetu, Rais Samia Suluhu Hassan, nimuhimu kujikumbusha yaliyo mbele yetu. Nasema kukarabati ni muhimu bila kigugumizi kuwa huu ni wakati wa kuponya na kukarabati.

Rais Magufuli amefanya mambo mengi. Amefufua shirika letu la ndege, amejenga madaraja ya juu na ya chini, amejenga barabara na viwanja vya ndege, amejenga shule, hospitali na kuwawezesha wafanyabiashara wadogo maarufu ‘machinga’. Lakini pia amefanikiwa kuinua sekta ya madini na kuhakikisha inachangia pato la taifa na mengine mengi, lakini kwa bahati mbaya alishindwa kutengeneza mfumo wa utumbuaji, uponyaji na ukarabati ndani ya jamii yetu. Maoni yangu, tunataka tusitake Rais Maguguli ametufundisha umuhimu wa kuthaminiana kwa kufuata sheria na katiba ya nchi. Hili tumejifunza wote, wawe wale wa vyama vya siasa na viongozi wa serikali, kila Mtanzania mwenye kujitambua nasema atakuwa ameliona hili, hivyo ni lazima tulifanyie kazi bila kuchelewa.

Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema, Katiba yetu inampatia Rais madaraka makubwa sana. Ninafikiri hatukuelewa alikuwa akimaanisha nini wakati ule. Ila sasa baada ya utawala wa Rais Magufuli, tumelitambua hili na ni imani yangu tumejifunza. Kwa sababu tumeshuhudia utumbuaji wa majipu, mchakamchaka ndani ya serikali, tumeshuhudia makovu makubwa baada ya utumbuaji, tumeshuhudia wanaofurahi na kushangilia, lakini pia tumeshuhudia chuki na uhasama mkubwa.

Kwa vile kazi bado ni kubwa na Tanzania ni yetu sote, ni muhimu sasa Mama yetu, Rais Samia baada ya kumaliza msiba huu mzito, atakuwa na muda wa kuanza pia kutengeneze mfumo wa uponyaji na ukarabati.

Hapa ukarabati niusemao unamaanisha “Rehabilitation”. Mfano watu wanaotumia dawa za kulevya, wakifanikiwa kuachana na tabia hiyo, wanapelekwa vituo vya “Rehabilitation” ili kuwarudisha kwenye hali zao za kawaida. Mara nyingi uponyaji ni muhimu ukiambatana na ukarabati.

Ukweli ni kwamba, hadi sasa wale waliotumbuliwa ni wasomi wazuri, ni watu ambao taifa linawahitaji, ni watu ambao wakipokea uponyaji na kukarabatiwa bado wanaweza kutoa mchango wao mkubwa kwa Taifa. Uponyaji, sina maana ya wale wanaoponya kwa kuomba na kufukuza mapepo. Hapana! Uponyaji wa elimu, uponyaji wa kufundisha na kuamsha roho ya uzalendo.

Uponyaji wa kufanya mtu ajitambue yeye na kuitambua jamii inayomzunguka. Uponyaji wa kufanya mtu atambue kwamba duniani hapa sote tunapita, na jukumu letu ni kuhakikisha tunatengeneza dunia salama kwa kila mtu na kwamba mali zote zitabaki nyuma yetu.

Yawezekana haya yanafahamika kwa walio wengi, lakini kwa yale tunayoyashuhudia ni kwamba bado tunahitaji elimu na bado tunahitaji kuhimiza uzalendo. Hoja ninayoijenga hapa ni kwamba yote haya tunayoyashuhudia. Ukwepaji wa ushuru, rushwa, uchu wa madaraka, wizi mdogo na mkubwa ni dalili za mmomonyoko wa maadili.

Na bahati mbaya, hatuna mfumo wa kujenga maadili. Uzalendo umepotea, na hakuna mfumo wa kujenga tena uzalendo wetu.

Mwalimu Nyerere alikuwa ametengeneza mfumo wa kujenga uzalendo. Mfumo wa maadili ya Kitanzania. Marais waliofuata baada ya hapo, hawakuendeleza mifumo hiyo. Utumbuaji majipu wa uongozi wa awamu ya tano ni matokeo ya kutokuwa na mifumo ya kujenga uzalendo kwenye awamu ya pili, ya tatu na ya nne ya uongozi wa taifa letu. Tunampongeza sana kwa hatua hii. Lakini kwa vile kazi ya kulijenga taifa letu si ya mashindano, si kazi ya kumtafuta mshindi bali ni kazi ya kuleta amani, maendeleo na usalama kwa kila Mtanzania, ni muhimu sasa Rais Samia akatengeneza mifumo ambayo itaendelea kujenga amani na utulivu nchini. Ndiyo maana nimekuja na mapendekezo ya mfumo huu wa ‘uponyaji na ukarabati.’ Tumelelewa kwenye jamii inayowasujudu wenye fedha. Hata kama tunajua ni za wizi au za kuuza unga, mwenye mali ndiyo anaitwa “mwanaume”, hata kama jinsia ni mwanamke, akiwa na fedha anakuwa “mwanaume”.

Jipu la kuwatukuza wenye fedha na mali nyingi, ni kubwa na ni ugonjwa wa watu wengi katika jamii yetu.