Chato: Kijiji kilichokaribia kuwa makao makuu ya mkoa-2
Katika mfululizo wa mapitio ya kitabu, 'I am the State: A President's Whisper from Chato' (Mimi ni Dola: Mnong'ono wa Rais kutoka Chato) leo tunaangazia sura yake ya pili inayozungumzia Chato kama kijiji ambacho kilikaribia kuwa makao makuu ya mkoa.
Kitabu kinaanza kwa kuelezea kulivyokuwa na mdororo wa uchumi nchini kote, uliosababishwa na mazingira mabaya ya biashara kati ya 2015 na 2020. Kwa miaka mitatu mfululizo (2016-2018), karibu biashara 4,640 zilifungwa kutokana na mazingira yasiyo rafiki ya biashara yanayotokana na sera mbaya, uwezo mdogo wa kibiashara kati ya wafanyabiashara wadogo na wa kati na ukosefu wa motisha.
Kelele za kupungua na hatimaye kufungwa kwa biashara kote nchini zilitolewa mara kadhaa na wabunge, ingawa Serikali haikuwahi kukiri jambo hilo.
Waandishi wa kitabu hicho miongoni mwa vyanzo walivyotumia, kimojawapo kimesema fedha kwenye mzunguko zilipungua kutoka asilimia 22 mwaka 2011 hadi asilimia 1.8 mwaka 2018 na kwamba kati ya 2011 na 2017 ukuaji wa Pato la Taifa (GNP) ulikuwa wa asilimia 7.8 lakini kufikia 2018 ulikuwa chini hadi asilimia 6.8.
Kutokana na hali kuwa mbaya, kati ya mwaka 2015 na 2020, Benki Kuu (BoT) ilichukua hatua kadhaa ama kusimamisha, kuunganisha au kufunga baadhi ya benki, zikiwamo Benki ya Wanawake Tanzania, Twiga BanCorp, Ecobank, Efatha Bank, Covenant Bank, Kagera Farmers' Cooperative Bank, Meru Community Bank na Njombe Community Bank.
Waandishi wa kitabu hicho wanasema ingawa ni sahihi kwa BoT kuchukua hatua kali dhidi ya mabenki katika hali ya ufilisi, ni kweli vilevile kwamba hali ya uchumi wa Taifa ina athari kubwa kwa hali ya taasisi hizo za kifedha.
Waandishi hao waligundua kuwa karibu benki zote zilizoathirika zilikuwa za binafsi, isipokuwa Twiga Bancorp, ambayo hatimaye iliunganishwa na Benki ya Posta Tanzania (TPB) pamoja na Benki ya Wanawake na kuunda Benki ya Biashara Tanzania (TCB).
Kwa hiyo, kadiri biashara zilivyokuwa zikipungua siku baada ya siku tangu 2016, hatima ya sekta kibinafsi ilikuwa katika hali mbaya zaidi. Serikali iliamua kuunda "Kikosi Kazi" kukusanya kodi kwa niaba ya taasisi yenye mamlaka hayo kisheria, TRA.
Katika mchakato huo, biashara nyingi zilikumbana na hali ngumu zaidi. Akaunti nyingi za biashara zilizuiwa na mabilioni ya pesa kuchukuliwa. Katika baadhi ya matukio, kwa sababu zinazojulikana zaidi na Serikali, wamiliki wa biashara walishtakiwa kwa makosa ya utakatishaji wa fedha na uhujumu uchumi.
Kuhusu Chato
Baada ya kueleza kinaganaga hali ya biashara ilivyokuwa na masaibu yaliyowakumba wafanyabiashara wengi, waandishi wa ‘I am the State’ wakaigeukia Chato.
Wanasema wakati biashara zikiporomoka katika maeneo mengi ya nchi kati ya 2016 na 2020 kutokana na mazingira yaliyotajwa hapo juu, kipindi hicho kilikuwa cha neema kwa Chato.
Ulianzishwa uwekezaji wa kimkakati katika wilaya ambayo haikujulikana kwa jumuiya yoyote kubwa ya wafanyabiashara, kinaandika kitabu hicho.
Biashara za Chato hazikuendeshwa na soko, wanasema, lakini zilisukumwa kisiasa na Rais ambaye alikuwa amejitokeza kukaidi sayansi ya biashara katika azma yake ya kubadili na kuendeleza mji wake wa Chato.
Na hivyo ndivyo Benki ya CRDB ilivyojikuta kwenye mtanziko ilipoamriwa kufungua tawi Chato lililofunguliwa Machi 9, 2018.
Kitabu kinamnukuu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei akisema benki hiyo ilikuwa imekataa kufungua tawi hilo Chato kwa sababu upembuzi yakinifu umeonyesha hakuna uwezekano wa kufanya biashara, lakini kuanzishwa kwa tawi hilo kulitokana na “utafiti uliofanywa na Rais mwenyewe.”
Ilionekana wazi kuwa pamoja na kwamba CRDB inaongoza kwenye orodha ya benki kubwa nchini kama NMB, NBC, Stanbic, Standard Chartered, Absa, DTB, Exim, Azania na Citi Bank, haikuwa na nia ya kunyakua fursa hii ya kuwepo Chato hadi ilipolazimishwa na mkuu wa nchi.
Watafiti wa kitabu hicho walizunguka Chato kuangalia huduma mbalimbali katika hoteli, baa, migahawa na nyumba za wageni. Uchunguzi wao ukabaini kuwa nyumba nyingi za kulala wageni zimeamua kushusha gharama za huduma kutokana na kupungua kwa wateja.
Wakati wa utafiti wao walitembelea hoteli kubwa Chato kwa kulinganisha. Katika matokeo ya utafiti wanabainisha kuwa biashara zilikuwa zimedorora.
Mathalan, wanazungumzia pia maeneo ambayo Halmashauri ya Wilaya ya Chato ilipima na kuuza takriban viwanja 2,000.
Kati ya hivyo, viwanja 1,500 vilipata wateja ingawa wengi kwa mkopo. Mradi huo ulivutia wanunuzi kutoka Chato na kwingineko, hasa watumishi wa umma. Lakini tangu mwaka 2021, kitabu kinabainisha, mradi unaonekana kutelekezwa, huku watu wengi waliokuwa wameanza ujenzi wakionekana kubadili mawazo.
Waandishi wa kitabu hicho wamebaini kuwa kati ya viwanja vyote vilivyopatikana katika mradi huu, ni asilimia 30 tu ndio vinaendelezwa. Wamebaini pia kuwa kuna hali ya kuzorota kwa biashara huko Chato na kwamba furaha kubwa iliyoshuhudiwa kati ya 2015 na 2021, imefifia.
Biashara nyingi ambazo zilikuwa zimeanza kuota mizizi, hususan za ujenzi, zimesimama na kuwa tangu Machi 2021 biashara nyingi zimefungwa. Wawekezaji wamepunguza kasi au wamebadili mawazo yao.
Timu ya utafiti ya kitabu ilibaini kuwa watumishi wengi wa Serikali, hasa wale wa ofisi binafsi ya rais, walinunua viwanja hivyo ili kumvutia. Baadhi yao walikuwa wameanza ujenzi, lakini hawajafanya maendeleo zaidi tangu Machi 2021 Magufuli alipoaga dunia.
Waandishi wa kitabu wamebaini kuwa wengi wao walikuwa wakiendeleza viwanja vyao wakati wa safari za kikazi kwenda Chato kwa sababu wangekaa Chato kwa miezi kadhaa kulingana na muda wa kukaa kwa bosi wao, lakini kwa kuwa safari rasmi zimekoma, nao wameacha kwenda.
Kitabu kinataja ujenzi wa Hoteli ya Burigi-Chato Park. Jiwe la msingi liliwekwa na Waziri wa Maliasili na Utalii wakati huo, Dk Hamis Kigwangalla Oktoba 10, 2019. Lakini shughuli za ujenzi wake nazo zimesimama na eneo lipo katika hali mbaya.
Kesho tutapitia ya sura ya tatu, The Dilemma of ‘I am the State’ (Mtanziko wa ‘Mimi ndiye dola’).