Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kilichoipaisha Wizara ya Nishati hiki hapa

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Felchesmi Mramba

Dodoma. Maboresho ya huduma kwa wananchi, ufuatiliaji wa karibu wa miradi na uwazi wa taarifa vimetajwa kuwa sababu kuu zilizopelekea kupanda kwa kiwango cha utendaji kazi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kutoka asilimia 95 katika robo ya tatu hadi asilimia 96.16 katika robo ya nne ya mwaka wa fedha 2024/2025.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema hatua hiyo ni matokeo ya jitihada za makusudi za watendaji kuhakikisha huduma za nishati zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

“Huduma zimeboreshwa na tunaona matokeo yake kupitia tathmini hizi. Utoaji taarifa kwa wananchi kwa wakati, utekelezaji wa miradi kwa ufanisi na matumizi ya mitandao ya kijamii katika elimu ya Nishati Safi ya Kupikia, vyote vimechangia kupanda kwa kiwango hiki,” amesema Mramba.

Amelitaja Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuwa mfano wa mafanikio baada ya kuimarisha mawasiliano na wananchi, jambo lililoimarisha uaminifu na kuleta maboresho katika huduma.

Aidha, amesisitiza taasisi nyingine kuongeza juhudi katika kutumia mitandao ya kijamii kuhamasisha matumizi ya majiko yenye kutumia umeme kidogo, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuhamasisha nishati safi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk James Mataragio, amesema ongezeko hilo la utendaji ni ishara kuwa mfumo wa tathmini ulioanzishwa umeleta ufanisi wa kazi na kuwahimiza watendaji kuendelea kushirikiana na Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini.

Mkurugenzi wa kitengo hicho, Anita Ishengoma, amesema tangu kuanza kwa tathmini hizo, kumesaidia kusimamia miradi kwa karibu zaidi na kuongeza uwajibikaji wa Idara na Taasisi.

“Ufanisi umeongezeka kwa sababu kila idara sasa inawasilisha taarifa kwa wakati na inajua inatathminiwa,” amesema.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Idara ya Umeme na Nishati Jadidifu imeibuka kinara ikifuatiwa na Kitengo cha Manunuzi na Kitengo cha Tehama. Upande wa Taasisi, Tanesco imeongoza, ikifuatiwa na Ewura na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA).

Mikoa ya Tanesco iliyofanya vizuri zaidi ni Manyara, Kinondoni Kusini na Simiyu, huku ikielezwa kuwa hakuna mkoa ulioshuka chini ya asilimia 91.83.

Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati, wakuu wa vitengo vya tathmini kutoka wizara mbalimbali na mameneja wa kanda wa Tanesco.