Kilimanjaro yavunja rekodi fedha za maendeleo

Muktasari:

  • Fedha kwa ajili ya maendeleo zilizotolewa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa Mkoa wa Kilimanjaro katika kipindi cha miezi sita kimevunja rekodi, Mkuu wa mkoa huo Stephen Kagaigai amesema.


Moshi. Fedha kwa ajili ya maendeleo zilizotolewa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa Mkoa wa Kilimanjaro katika kipindi cha miezi sita zimevunja rekodi, Mkuu wa mkoa huo Stephen Kagaigai amesema.

Mkuu huyo wa Mkoa Kilimanjaro ameyasema hayo leo Jumamosi Januari 22, 2022 katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika (MoCU) wakati wa uzinduzi wa Tamasha la utamaduni mkoa Kilimanjaro, ambapo Rais Samia ni mgeni rasmi.

Akitoa salamu za mkoa huo kwa Rais ambaye pia ni Chifu Hangaya, Kagaigai amesema katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2021, mkoa huo umepokea Sh57.39 bilioni sawa na asilimia 40 ya bajeti yote ya maendeleo.

“Hiki ni kiwango kikubwa cha fedha za maendeleo kuwahi kupokelewa mkoani hapa katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa Serikali. Kwa niaba ya wananchi wa Kilimanjaro tunakushukuru (Rais Samia) sana,”amesema.

Akifafanua zaidi, mkuu huyo wa mkoa amesema mkoa huo ulipokea Sh7.88 bilioni ambazo ni sehemu ya mkopo wa Sh1.3 trilioni kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa ajili ya ustawi na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Uviko-19.

Mbali na kiasi hicho, lakini mkoa huo ulipokea Sh2.48 zinazotokana na tozo kwenye miamala ya simu, Sh18 bilioni za ruzuku ya maendeleo kwa Serikali za mitaa na pia mkoa ulipata Sh4.2 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za Kata.

Halikadhalika mkoa huo ulipokea Sh418.1 milioni ambazo ni fedha za mpango wa matokeo, Sh22.44 bilioni kwa ajili ya matengenezo na ukarabati wa barabara na ukapokea Sh1.9 bilioni kwa ajili ya miundombinu ya maji katika mkoa huo.

Mkuu huyo wa mkoa alimweleza Rais kuwa fedha zote zilizopokelewa zimeelekezwa kwenye ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya utoaji wa huduma  katika sekta za Afya, Elimu, Maji, barabara na madaraja.