Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kilimo kinavyoibadili Mbeya kielimu

Muonekano wa shule ya Avocado Sevondari iliyopo wilayani Rungwe mkoani Mbeya iliyojengwa kupitia zao la Parachichi.

Muktasari:

  • Mbeya imeanza kutumia kilimo kufungua fursa nyingi ikiwamo elimu kwa kujenga shule ikiwa na malengo ya kuongeza thamani katika mazao yanayolimwa na kurejesha huduma kwa jamii.

Mbeya. Kwa miaka mingi kilimo kimekuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Mkoa wa Mbeya, kikitoa ajira, chakula na mapato kwa maelfu ya wananchi.

Sasa sekta hiyo imechukua sura mpya, baada ya baadhi ya halmashauri kuanza kutumia mapato yatokanayo na mazao ya kimkakati kujenga shule, hatua inayopanua huduma za elimu na kuonyesha namna rasilimali za kilimo zinavyoweza kubadilisha maisha ya jamii.

Kupitia mkakati huo, shule zinazojengwa zimepewa majina ya mazao yanayochangia kwa kiasi kikubwa mapato ya halmashauri husika, zikiwamo Mayeka Sekondari (zamani Tumbaku Sekondari) wilayani Chunya, Pareto Sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Avocado Sekondari wilayani Rungwe na Cocoa Girls wilayani Kyela.

Mbali na kuhamasisha uzalishaji wa mazao hayo, shule hizo zimeongeza upatikanaji wa elimu kwa watoto waliokuwa wakitembea umbali mrefu kufuata masomo, hususan katika maeneo ya vijijini.

Kwa mujibu wa viongozi wa mkoa, uwekezaji huo umechangia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza ufaulu wa wanafunzi. Mkoa wa Mbeya kwa sasa unaendelea kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa kwa kufikia zaidi ya asilimia 90 ya ufaulu, huku lengo likiwa ni kufikia ufaulu wa asilimia 100 katika miaka ijayo.

Mbeya ni miongoni mwa mikoa inayotegemewa kwa uzalishaji wa mazao ya biashara na chakula nchini. Mazao kama pareto, parachichi, kakao, tumbaku, kahawa, ufuta, maharage, viazi, ndizi na korosho yameendelea kuwa chanzo kikuu cha mapato ya wakulima, halmashauri na Serikali kwa ujumla.

Katika kipindi cha miaka ya karibuni, Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta ya kilimo kupitia ruzuku ya mbolea, kuimarisha kilimo cha umwagiliaji na kuhamasisha matumizi ya teknolojia ili kuongeza uzalishaji na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mkoani Mbeya, halmashauri zimeamua kwenda hatua zaidi kwa kurejesha sehemu ya mapato yanayotokana na mazao hayo kwa wananchi kupitia ujenzi wa miundombinu ya elimu.

Wilayani Chunya, ambako kilimo cha tumbaku ni miongoni mwa shughuli kuu za kiuchumi, Halmashauri Imejenga shule ya wasichana iliyokuwa ikijulikana kama Tumbaku Sekondari kabla ya kubadilishwa jina na kuitwa Mayeka Sekondari. Shule hiyo kwa sasa imefikia kidato cha tatu, huku Serikali ikiendelea na ujenzi wa bweni ili kuboresha mazingira ya kujifunzia.

Muonekano wa Shule ya Sekondari ya Wasichana (Cocoa Girls) iliyopo wilayani Kyela mkoani Mbeya iliyojengwa kupitia tozo za zao la Cocoa.

Mbali na hilo, Halmashauri ya Chunya ina mpango wa kujenga shule nyingine kupitia mapato yanayotokana na madini ya dhahabu, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kutumia rasilimali za eneo hilo kuboresha huduma za jamii.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, mapato yatokanayo na zao la pareto yamewezesha ujenzi wa Pareto Sekondari. Halmashauri hiyo inategemea kilimo kwa zaidi ya asilimia 80 ya mapato yake ya ndani, huku pareto, kahawa, ufuta, mahindi na viazi vikiwa miongoni mwa mazao yanayochangia mapato hayo.

Kwa upande wa Wilaya ya Rungwe, zao la parachichi limeendelea kuwa mhimili wa uchumi wa wananchi. Kupitia tozo zinazotokana na zao hilo, Halmashauri imejenga Avocado Sekondari, shule ya mchanganyiko inayotarajiwa kuanza kutoa huduma muda wowote.

Kyela nayo imeamua kutumia mapato yatokanayo na zao la kakao kujenga shule ya wasichana ya Cocoa Girls. Shule hiyo tayari ina wanafunzi wa kidato cha pili, huku ujenzi wa bweni, jengo la utawala na vyoo ukiendelea.

Wananchi wamepongeza hatua hiyo wakisema imeondoa adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata shule na kupunguza gharama kwa wazazi.

Mkazi wa Wilaya ya Mbeya, Yusuph Mwankenja anasema kabla ya Pareto Sekondari kujengwa walilazimika kuwasafirisha watoto wao kwenda shule za mbali, jambo lililoongeza gharama na kuwachosha wanafunzi.

“Kwa sasa watoto wanafika shule kwa wakati na mazingira ya kujifunzia yameboreshwa. Tunaona matokeo yake kupitia ongezeko la ufaulu,” anasema.

Naye Beatrice Aloyce anasema uamuzi wa kujenga shule katika maeneo ya pembezoni umepunguza mzigo kwa wazazi na kuongeza fursa za watoto kupata elimu karibu na makazi yao.

“Serikali imefanya jambo kubwa. Sasa jukumu letu ni kuendelea kushirikiana nayo ili watoto wetu wapate elimu bora,” anasema.

Mkulima wa zao la kakao, Faustine Charles anasema uwekezaji huo unaonyesha kuwa kilimo si chanzo cha mapato pekee bali pia kinaweza kuwa msingi wa maendeleo ya jamii.

“Kilimo ndicho uti wa mgongo wa uchumi wetu. Tunapolima kwa tija na kupata masoko, matokeo yake yanaonekana hata kwenye sekta ya elimu,” anasema.

Mtaalamu wa kilimo, Benjamin Alex anasema uzoefu wa Mbeya unapaswa kuigwa na mikoa mingine kwa kutumia mapato ya shughuli za kiuchumi kuwekeza katika huduma za jamii badala ya kutegemea Serikali Kuu pekee.

Anasema pamoja na kilimo, mapato yatokanayo na sekta nyingine kama madini na uwekezaji yanaweza kuelekezwa katika ujenzi wa shule, vituo vya afya na miundombinu mingine muhimu.

Kwa upande wake, mdau wa elimu Benjamin Rafael anasema kila mkoa una rasilimali inayoweza kutumika kuleta maendeleo ya wananchi iwapo mapato yake yataelekezwa katika miradi yenye manufaa ya moja kwa moja kwa jamii.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli amesema halmashauri hiyo nayo imeanza maandalizi ya kujenga shule kupitia mapato yatokanayo na zao la mpunga.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Frolah Luhala amesema baada ya mafanikio ya Cocoa Girls, halmashauri ina mpango wa kujenga shule ya wavulana kupitia mapato ya zao la mawese kadri makusanyo yatakavyoongezeka.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Tamimu Kambona amesema baada ya kutumia mapato ya tumbaku kujenga shule, sasa kuna mpango wa kujenga shule nyingine itakayopewa jina la Dhahabu kutokana na mchango wa madini katika uchumi wa wilaya hiyo.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Erica Yegela amesema zaidi ya asilimia 80 ya mapato ya ndani ya halmashauri yanatokana na sekta ya kilimo, jambo linaloifanya kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya elimu na huduma nyingine za jamii.

Kwa Mbeya, kilimo hakibaki tena kuwa shughuli ya kuzalisha chakula na kuongeza kipato cha wakulima. Kimekuwa daraja la kuwafikisha watoto shuleni, kupunguza umbali wa kutafuta elimu na kuwekeza katika kizazi kitakachobeba maendeleo ya baadaye. Hivyo, kila gunia la mazao linalovunwa shambani linaendelea kubeba si tu thamani ya kiuchumi, bali pia matumaini ya elimu na maendeleo ya jamii.