Kinachokwamisha ongezeko vituo vya kujaza gesi kwenye magari hiki hapa

Magari yakiwa kwenye foleni ya kujaza gesi jijini Dar es Salaam

Muktasari:

  • Tangu huduma ya kujaza gesi kwenye magari ianze mpaka sasa takriban magari 3,000 tu ambayo yamefungwa mfumo wa gesi huku kukiwa na vituo vitatu pekee vya kujaza nishati hiyo jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Usimamizi wa bomba la kusambaza gesi kuwa kwenye umiliki wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kodi kubwa katika uagizaji wa vifaa vya kujengea vituo, ni miongoni mwa mambo yanayochangia kusuasua kwa ujenzi wa vituo vya kujazia gesi kwenye magari.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Aprili mosi, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waagizaji na wasambazaji wa Mafuta (Taomac), Raphael Mgaya, alipozungumza na Mwananchi.

Tangu huduma hiyo ya kujaza gesi ianze mpaka sasa zaidi ya magari 3,000 yamefungwa mfumo wa gesi huku kukiwa na vituo vitatu pekee vya kujaza nishati hiyo.

Vituo hivyo ni pamoja na cha Ubungo kinachomilikiwa kwa ubia kati ya TPDC na kampuni ya Pan African.

Kituo kingine ni cha Tazara kinachomilikiwa na Kampuni ya Anric Gas na kilichopo Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere kinachomilikiwa na Kampuni ya TAQA Arabia.

 Akizungumzia kwa kina suala la kuwepo kwa kasi ndogo ya kuongezeka kwa vituo hivyo, Mgaya amesema kuna matatizo makubwa mawili, mojawapo likiwa la mfumo wa usimamizi.

Amesema mfumo uliopo sasa umempa TPDC haki ya kumiliki miundombinu ya kusafirishia gesi hata kama mmiliki atajenga kwa fedha zake mpaka kituoni kwake.

 “Hii ya TPDC kuwa wamiliki wa bomba ina changamoto, ndiyo maana mnaona kumekuwa na kujivuta katika kuwekeza kwenye vituo hivyo vya kujazia gesi, kwa kuwa hakuna mtu aliye tayari kuweka hela yake ya biashara katika mtindo huo,” amesema.

Mgaya amesema kazi ya kujenga bomba kutoka TPDC kwenda kwenye kituo cha mmiliki ilipaswa ifanywe na wenyewe kwa kuwa ndiyo mwenye mamlaka ya kusambaza miundombinu hiyo.

Hata hivyo, ili TPDC isambaze na kujenga ni  lazima ihakikishiwe huko wanakopeleka bomba kuna wateja.

Kutokana na mchakato huo, amesema wawekezaji wengine wanaamua kujenga mabomba hayo wenyewe, lakini mwisho wa siku TPDC ndiye mmiliki.

Mgaya amesema baada ya mwekezaji kujenga, ndipo aanze mchakato wa kuidai TPDC gharama zake ambazo zinalipwa kidogo kidogo kupitia tozo atakazokuwa anatozwa anaponunua gesi.

“Kwa utaratibu huu, kupata mwekezaji katika eneo hilo inakuwa vigumu kidogo,” amesema Mgaya.

Hata hivyo, Mgaya ameishauri Serikali kuwaachia wawekezaji wajenge mabomba hayo wenyewe na kuyamiliki, tofauti na ilivyo sasa.

Ametaja kikwazo kingine kuwa ni kodi kubwa ya uagizaji wa vifaa vya kujengea vituo hivyo.

Katika hili, ameishauri Serikali ipunguze kodi kwenye vifaa vya kujenga miundombinu ya vituo hivyo ambavyo vinatoka nje ya nchi, hali itakayowapunguzia gharama na kuvutia wawekezaji wengi katika eneo hilo.

 “Ili uweze kupata mkopo kutoka benki, ndani ya miaka saba unapaswa uwe umerudisha mkopo wao lakini kwa bei hizi ndogo za gesi, ni ngumu mwekezaji kurudisha mkopo huo kwa kuwa kituo kimoja cha kujaza gesi kinaweza kukuchukua zaidi ya miaka saba kurejesha faida na fedha ulizotumia.


Mwitikio si mdogo

Akizungumzia kusuasua huko, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame amesema mwitikio si mdogo kama inavyodhaniwa, bali kuanza utekelezaji ndio imechukua muda.

Makame amesema mpaka sasa takwimu zinaonyesha tayari kuna kampuni zisizopungua 30 ambazo zimeomba kuwekeza katika eneo hilo na kati ya hizo, zipo zisizopungua tano ambazo ziko kwenye hatua mbalimbali ya ujenzi wa vituo na mabomba.

Amezitaja kampuni hizo ni pamoja na ya Puma ambayo mpaka Agosti mwaka huu inatarajia iwe imejenga vituo vitano.

Wawekezaji wengine ni kampuni ya Energo inayojenga kituo la Mikocheni karibu na kiwanda cha Cocacola, pia  Taqa Dalbit ambayo imeshajenga  kituo Uwanja wa Ndege na inatarajia kujenga kingine eneo la Viwanja vya Posta na miaka mitatu ijayo imejipanga iwe imejenga vituo 12 jijini Dar es Salaam.

Amesema kampuni nyingine ambazo zipo katika hatua ya ujenzi ni ya uuzaji wa mafuta ya Big Bon, nayo inatarajia kujenga vituo viwili, BQ Contractors, Rafiki Energies na Rashal Energies.

“Hivyo mwitikio upo, lakini watu wamechelewa tu kuanza utekelezaji, awali kulikosekana taarifa sahihi kwa wadau juu ya uwekezaji huu, lakini hilo tumelishughulikia na baada ya muda mfupi watu watashuhudia vituo vingi vikitoa huduma hii,”amesema Makame.


Umiliki wa bomba

Kuhusu umiliki wa bomba kutoka TPDC kwenda kwenye vituo vya wawekezaji, Makame amekiri kuna changamoto, hasa pale bomba hilo linapoenda umbali mrefu kutoka walipo wao.

Hata hivyo, amesema inapojitokeza hali hiyo, TPDC humweleza mmiliki ajenge na watakatana, kila anapokuwa ananunua gesi kwao kwa kipindi cha miaka isiyopungua mitatu.

Makame amesema sababu ya kufanya hivyo ni pale TPDC inaposhindwa kujenga kwa wakati ambao mwekezaji anautaka.

Amefafanua kuwa umiliki wa mabomba hayo kwa TPDC umewekwa kwa makusudi ili kuwepo kwa uhuru wa watu wengine kuunganishwa katika bomba hilo pindi watakapohitaji.

“Unaweza kufananisha kwa mbali na mtu anapotaka kuvutiwa umeme, nguzo anayolipia inakuwa mali ya Tanesco, hivyo mtu mwingine atakapotaka kujiunga na huo umeme, hupaswi kumtoza chochote kwa kuwa wewe ndio ulilipia.

“Ila tofauti yetu hapa sisi tutakulipa kidogokidogo kila unaponunua gesi kwetu mpaka pale hela yako uliyotumia kuvuta bomba hilo itakapokwisha,”anasema mkurugenzi huyo.

“Tunavyojua mtu anapojenga kituo, lengo lake ni kuuza gesi, hivyo atapata faida kwenye kuuza gesi na sio haki ya kuunganisha watu kwenye bomba kwa sababu hiyo ni kazi ya TPDC,” amesema.

Hata hivyo, amesema hili linaweza kubadilika endapo muhusika atakubali kufanya nao makubaliano ya kimaandishi kuwa hatazuia watu wengine kujiunga na bomba hilo, hivyo wakamwachia umiliki.


Kodi ya vifaa

Makame amezungumzia pia kodi za vifaa kuwa juu kuwa hilo linashughulikiwa na katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2024/2025 itakayosomwa bungeni Juni mwaka huu, itazungumzia kupunguzwa bei ya vifaa vya kufunga mifumo ya gesi katika magari.

“Hilo la gharama za vifaa kwenye vituo tumelichukua, tutapanga siku ya kukutana na wadau kujua wanatakaje ili tuweze kuwasilisha mapendekezo yetu bungeni na kwa kuwa limekaa kisera zaidi, tutaliwasilisha kwa Wizara ya Fedha,” amesema Makame.

Akizungumzia mpango wa kuongeza vituo vyao, Makame amesema TPDC iko mbioni funguo vituo vya kuhamishika katika barabara kuu za Jiji la Dar es Salaam, ikiwemo ya Bagamoyo, Kilwa, Morogoro, Kigamboni na katikati ya jiji.

Na hilo watalifanya ndani ya miezi minane kuanzia sasa.

“Tumeamua tuweke vituo vya kuhamishika, ili huko baadaye wawekezaji watakapoongezeka, sisi inakuwa rahisi kuhamishia vituo hivyo maeneo mengine ambapo havipo,” amesema.


Uhakika wa wateja

Hata hivyo, Profesa Abel Kinyondo, mtaalam wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ametoa mawazo tofauti, akisema anachokiona yeye ni kuwa kwenye sekta hiyo ya gesi tatizo ni watu binafsi kutokuwa na uhakika wa wateja na kutokuwepo utashi wa kisiasa kutoka serikalini.

Amesema haiwezekani Serikali inahamasisha watu kufunga mifumo ya gesi kwenye magari yao, wakati yenyewe bado inaagiza magari ya watumishi wake yanayotumia mafuta.

“Wafanyabiabiashara wanaangalia mahali pa kuwekeza palipo na uhakika na fedha zao  zitarudi vipi. Kwa hiyo kama Serikali nayo ingeonyesha kwa vitendo kwa kupiga mrufuku uingizaji wa magari yanayotumia mafuta na kutaka yaletwe ya gesi,  ni wazi vituo vingi vingefunguliwa.

“Lakini kinachofanywa sasa ni watu kulima kijamaa, lakini wanakula kibepari. Serikali hapa inapaswa kuonyesha mfano, hivyo visingizio vingine wanavyotaja sekta binafsi wala visingekuwepo,”amesema profesa huyo.

Mmoja watumiaji wa gesi ya kwenye magari, Grace Mwakibinga amesema licha ya nishati hiyo kuwa rahisi, lakini huwapotezea muda pale wanapotaka kuijaza kwenye magari yao.

“Nadhani Serikali ifike mahali ipunguze ukiritimba na kutaka kila kitu kuendesha yenyewe, ndio maana kukawa na sekta binafsi. Basi iwaache huru kufanyabiashara hii ili wananchi tupate huduma kwa urahisi,” amesema mtumiaji huyo.

Naye Shola Chiwale amesema uhamasishaji wa watu kujiunga na mfumo wa gesi kwenye magari uende sambamba na upatikanaji wa huduma hiyo mtaani.

“Tumehamasika kuhamia kwenye gesi, ndio maana sasa hivi vituo unakuta magari yapo kwenye foleni, haya mambo yanapaswa kwenda sawa, sio mnahamasha watu kufunga gesi lakini hakuna vituo vya kutosha,” amesema.