Kishindo cha Sumaye

Muktasari:

Anakwenda kuzungumza nini. Ndio swali unaloweza kujiuliza kuhusu mkutano wa waziri mkuu wa zamani, Frederick Sumaye na waandishi wa habari kesho Jumatano Desemba 4, 2019.

Dar es Salaam. Anakwenda kuzungumza nini. Ndio swali unaloweza kujiuliza kuhusu mkutano wa waziri mkuu wa zamani, Frederick Sumaye na waandishi wa habari kesho Jumatano Desemba 4, 2019.

Sumaye ameitisha mkutano huo siku chache baada ya kushindwa uchaguzi wa uenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani.

Licha ya kuwa mgombea pekee, alipigiwa kura 48 za hapana kati ya kura 76.

 Kulingana na taratibu za chama hicho uchaguzi huo utarudiwa.

Taarifa iliyotolewa leo Jumanne Desemba 3, 2019 na  Evanuru Nasari, katibu msaizidi wa ofisi ya waziri mkuu huyo mstaafu inaeleza kuwa  lengo la mkutano huo ni kuzungumzia masuala ya siasa nchini na mwenendo wa uchaguzi unaoendelea  Chadema.

Sumaye aliyekuwa waziri mkuu mwaka 1995 hadi 2005 pia amechukua fomu kugombea uenyekiti wa Chadema, atachuana na mwenyekiti wa sasa wa chama hicho, Freeman Mbowe na mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe.

Sumaye aliyejiunga  Chadema Agosti 22,  2015 akiunga dhana ya mabadiliko iliyotangazwa na vyama vya upinzani vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) akitokea CCM,  alikuwa nguzo kwenye kampeni za mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.

Katika kampeni hizo, Sumaye alizunguka karibu nchi nzima akimnadi  Lowassa ambaye Machi Mosi, 2019 alirejea CCM.

Akizungumza na Mwananchi mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema  amesema hawana taarifa kuhusu mkutano huo wa Sumaye.

"Tunaona barua hiyo katika mitandao kama wengine, tumeshtushwa kuona barua yenye nembo ya Taifa inatumika kuitisha mkutano wa kiongozi wetu," amesema Mrema.