Prime
Kitanzi chawang’ang’ania watatu walioua Kibosho
Muktasari:
- Mawakili wa warufani waliwasilisha hoja tano za rufaa wakidai kuwa Mahakama hiyo ya chini ilikosea kisheria kuwatia hatiani warufani kutokana na shitaka lenye dosari ambalo pia lilitofautiana na ushahidi na kuendesha mashauri kinyume na sheria.
Arusha. Mahakama ya Rufani Tanzania imebariki adhabu ya kunyongwa hadi kufa waliyopewa wakazi wa tatu wa Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Watu hao walihukumiwa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua Lukresia Mwacha, kwa kumshambulia kwa kumpiga ngumi, mateke, waya wa umeme na fimbo.
Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani limetupilia mbali sababu tano za rufaa walizowasilisha, ikiwemo ya madai ya kushindwa kuchunguza na kutathmini ushahidi wote wa upande wa mashitaka uliokuwa unapingana na kushindwa kuthibitisha shitaka bila shaka yoyote.
Warufani hao ni Juliana Kimaro, Fortunatus Kisoka na Clemencia Kisoka, ambao maelezo ya kosa lililosababisha wahukumiwe kifo, yanaeleza kuwa usiku wa Machi 19, 2016 huko Kibosho Kirima wilayani Moshi, walimuua Lukresia.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Pamela Mazengo aliyepewa mamlaka ya ziada kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo ya mauaji, aliisikiliza na kutoa hukumu Septemba 11, 2020.
Katika kuthibitisha kesi hiyo, upande wa mashtaka uliegemea zaidi ushahidi wa pande mbili ikiwemo wa mama wa marehemu ambaye alikuwa shahidi wa kwanza, Fausta Mwacha na ushahidi wa shahidi wa tano ambaye ni mdogo wa marehemu, Boniface Mwacha.
Ushahidi wa pili ni uliotolewa na marehemu kabla hajafariki ambaye alimweleza mpelelezi wa Polisi kuhusu namna alivyoshambuliwa na warufani hao.
Mama wa marehemu, alidai mahakamani kuwa siku ya tukio baada ya mkutano wa dini uliofanyika karibu na nyumbani kwake, saa mbili usiku marehemu aliondoka akiwa na viti alivyotakiwa kurudisha kwenye baa ya baba yake, mtaa wa Ngurungi, Kibosho Kirima Kati.
Muda mchache baadaye, mama huyo alidai alisikia kengele na kukimbilia kuelekea upande huo uliokuwa karibu na baa ya mumewe ambapo alipofika alimkuta marehemu amezungukwa na watu wakiwamo warufani akiwa chini amejeruhiwa.
Alieleza kuwa eneo hilo lilikuwa na mwanga uliotokana na taa za umeme zilizokuwa zikiwaka kutoka kwenye baa hiyo na aliwaona na kuwatambua warufani hao ambao alikuwa anafahamiana nao.
Alidai kuwa wakati mrufani wa kwanza alimpiga marehemu ngumi na mateke, wa pili alimpiga na waya wa umeme na mrufani wa tatu alitumia fimbo kumpiga zaidi kichwani, huku John Kimaro aliyetajwa alikuwa amesimama tu akitazama kipigo hicho.
Alidai kuwa aliwakabili warufani, akitaka kujua kwa nini walikuwa wakimshambulia bintiye. Mrufani wa pili alijibu mara tatu, "mama nimekuheshimu sana, nilitaka nimalize kazi lakini nimekuheshimu', akimaanisha kwamba "ni kwa heshima yako kwamba nimeacha kumpiga, lakini nilitaka kumuua papo hapo."
Mdogo wa marehemu (shahidi wa tano), alidai kumkuta dada yake wamejeruhiwa akiwa amelala chini na kuwa aliwaona warufani wote watatu.
Marehemu alipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Moshi, kisha kupelekwa Hospitali ya Mawezi ila hali yake ilizidi kuwa mbaya, akapelekwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Aprili 11, 2016 na kufanyiwa upasuaji wa kichwa Aprili 14, mwaka huo.
Shahidi wa tatu wa Jamhuri, Konstebo Ramadhan Saidi, aliiambia mahakama Machi 20, 2016, alimuhoji marehemu kuhusu tukio hilo na aliwataja waomba rufaa hao kuwa miongoni mwa waliomshambulia.
Daktari bingwa wa magonjwa kutoka Hospitali ya KCMC, Dk Alex Mremi ambaye aliufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Aprili 18, 2016, alithibitisha kifo hicho kilitokana na jeraha kubwa la ubongo.
Katika kuwatia hatiani warufani kwa kosa la mauaji, Hakimu alieleza ushuhuda wa shahidi wa kwanza na ushahidi wa matibabu, umethibitisha marehemu alikufa kifo cha kikatili.
Kifo hicho kilichotokana na jeraha kwenye ubongo, huku ushahidi wa mama na mdogo wa marehemu ukionyesha waliwatambua warufani ndiyo walimshambulia marehemu na kuwa licha ya jambo hilo kuhitaji uthibitisho, ushahidi wa mazingira ulionyesha marehemu alishambuliwa na warufani.
Sababu za rufaa
Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo ya jinai namba 448/2020, Mawakili Martin Kilasara, Hellen Mahuna na Lilian Mushemba waliwawakilisha warufani hao.
Mawakili wa warufani waliwasilisha hoja tano za rufaa ambazo wanadai Mahakama hiyo ya chini ilikosea kisheria kuwatia hatiani warufani kutokana na shitaka lenye dosari ambalo pia lilitofautiana na ushahidi, kuendesha mashauri kinyume na sheria.
Nyingine ni kushindwa kuchunguza na kutathmini ushahidi wote wa upande wa mashitaka, ambao ulikuwa unapingana, wa ajabu, hautoshi na haukutegemewa na kutoa shitaka dhidi ya warufani bila kuthibitishwa bila shaka yoyote na kushindwa kuzingatia utetezi wa warufani.
Jamhuri ikiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Veridiana Mlenza na Mawakili wa Serikali, Agatha Pima na Julieth Komba, ambao walipinga vikali rufaa hiyo na kueleza kesi hiyo ilithibitishwa bila kuacha shaka.
Hukumu ya rufani
Baada ya kupitia na kuchambua hoja za mawakili wa pande zote mbili, jopo la majaji watatu wa Mahakama ya rufani, Jaji Dk Gerald Ndika, Jaji Zephrine Galeba na Jaji Leila Mgonya, walitupilia mbali hoja zote tano za rufaa hiyo, Juni 6, 2024 katika vikao vyake vilivyokaa Moshi.
Huku wakinukuu mashauri mbalimbali ya Mahakama ya Rufani, majaji hao wameeleza kuwa mabishano ya shahidi au mashahidi hayawezi kuepukika katika kesi yoyote, endapo hayaathiri kesi.
Wakitolea mfano Rufaa ya jinai namba 92 ya mwaka 2007 iliyokatwa na Dickson Elia, Nsamba Shapwata na mwingine dhidi ya Jamhuri, iliyotolewa Mei 30, 2008. Katika kesi hiyo mahakama ilisema mara kwa mara katika mashauri yote mikanganyiko ya kawaida na hitilafu hutokea katika ushahidi.
Walieleza kuwa kwa kuongozwa na maoni yaliyotangulia, wamepitia kwa uangalifu uthibitisho uliorekodiwa wakizingatia hoja zinazoshindana na mawakili ikiwemo endapo marehemu alifariki Aprili 17, 2016 (kulingana na ushahidi wa shahidi wa kwanza na tano) au Aprili 18, mwaka huo kama ilivyodaiwa na shahidi wa pili.
“Suala hili ni dogo kwa wazi na shahidi wa pili ushahidi wake juu ya kipengele hicho ulikadiria wakati wa kifo na hakujafanya kuwa anatoa wakati halisi. Kwa vyovyote vile kutokulingana huku hakubadili ukweli kwamba marehemu alifariki,” amesema.
Kuhusu madai ya chuki kati ya marehemu na familia yake na upande mmoja wa warufani hasa mrufani wa pili (Fortunatus) , Amesema hiyo ni hoja dhaifu na haiwezi kuondoa ushahidi wa mashitaka kwamba mrufani wa kwanza na wa pili waliotambuliwa eneo la tukio.
Kuhusu kinyongo, Hakimu wa kesi hiyo alishikilia kwa usahihi, ukurasa wa 184 wa kumbukumbu ya rufaa, kwamba chuki hizo zisingekuwa sababu ya familia ya marehemu kutengeneza kesi dhidi ya warufani, kwani ushahidi upo wazi warufani walimjeruhi marehemu ambaye alikuja kufariki kutokana na majeraha hayo.
Katika uchambuzi wa mwisho, majaji hao waliona mahakama ya awali ilizingatia ushahidi wa shahidi wa kwanza na wa tano kwamba warufani walimshambulia na kumjeruhi marehemu Machi 19 , 2016 na kusababisha kifo chake mwezi mmoja baadaye.
“Hiyo ni kwa kuzingatia mazingira ambayo mauaji yalitokea na ushahidi wa shahidi wa kwanza kwamba mrufani wa pili alitangaza kwenye eneo la tukio kuwa wanataka kummaliza marehemu jioni hiyo,”imeeleza hukumu hiyo.
“Hatuoni ugumu wowote wa kuunga mkono uamuzi wa mahakama kwamba marehemu aliuawa kwa ufedhuli. Mwisho hatuoni umuhimu wowote wa rufaa hii, hivyo tunaitupilia mbali ,” walisema katika hukumu yao iliyopatikana katika mtandao wa mahakama kuu wa TanzLII.