Kivuko kumaliza kero ya wanafunzi kupanda mitumbwi Ukerewe

Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Adam Malima (Aliyeinama) akichomelewa chuma kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa vivuko vitatu vitakavyotoa huduma ya usafiri katika visiwa vilivyoko ndani ya Ziwa Victoria. Ujenzi huo unahusisha kivuko cha Bwiro-Bukondo Wilayani Ukerewe, Nyakariro-Kome wilayani Sengerema na Ijinga-Kahangala wilayani Magu mkoani hapa. Picha na Mgongo Kaitira.

Muktasari:

  • Serikali imeweka jiwe la msingi la ujenzi wa vivuko vitatu ndani ya Ziwa Victoria ambacho ni kitakachotoa huduma kati ya kisiwa cha Bwiro na Bukondo wilayani Ukerewe.

Mwanza. Huenda adha ya wanafunzi wanaoishi katika Kisiwa cha Bwiro na Bukondo wilayani Ukerewe kutumia mitumbwi kwenda shuleni ikamalizika baada ya serikali kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kivuko katika visiwa hivyo kinachogharimu zaidi ya Sh4.4 bilioni.
Uwekaji wa jiwe hilo umeenda sambamba na ujenzi wa kivuko kitakachotoa huduma ya usafiri kwa wakazi wakiwemo wanafunzi kati ya eneo la Nyakariro na Kome wilayani Sengerema unaogharimu Sh8 bilioni na eneo la Ijinga na Kahangala wilayani Magu mkoani hapa ambacho kinachogharimu zaidi ya Sh5 bilioni.

Akizungumza na Mwananchi katika hafla ya uwekaji wa jiwe la ujenzi wa vivuko hivyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ukerewe, Joshua Manumbu amesema wilaya hiyo yenye visiwa zaidi ya 38 inakabiliwa na uhaba wa vivuko jambo linalowalazimu wanafunzi kutumia mitumbwi kwenda shuleni.
Amesema kutokana na matumizi ya mitumbwi kwenda na kutoka shuleni wanafunzi hujikuta wakipata ajali huku akisema kukamilika kwa kivuko hicho mbali na kuimarisha usalama wao pia itaongeza maudhurio kwa wanafunzi hao.

"Mawimbi yanapokuwa makubwa wanafunzi wengine hukacha shule na kuishia mitaani kwani hawawezi kumudu kasi ya mawimbi hayo. Lakini Kivuko hiki kikikamilika itaongeza usalama kwa watoto wetu," amesema Manumbu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Songoro Marine Transport Limited, Meja Songoro amesema ujenzi wa kivuko kitakachotoa huduma kati ya Kisiwa cha Bwiro na Bukondo wilayani Ukerewe na Ijinga hadi Kahangala wilayani Magu utakamilika Julai 15,2023 huku kivuko cha Nyakariro hadi Kome wilayani Sengerema ukikamilika Julai 31 mwaka huu.
"Tutahakikisha tunakamilisha ujenzi wa vivuko hivi kwa wakati na kuzingatia thamani ya mradi husika. Lengo ni kuhakikisha serikali inaendelea kutuamini wakandarasi wazawa katika miradi mikubwa kama hii," amesema Songoro.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa), Lazaro Kihalala amesema kivuko cha Bwiro-Bukondo kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 200, tani 100 za mizigo na gari ndogo 10 huku kivuko cha Nyakariro-Kome kikibeba abiria 800, tani 170 za mizigo na gari ndogo 22.

Kuhusu kivuko cha Ijinga-Kahangala wilayani Magu, Kihalala amesema kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 200, tani 100 za mizigo na gari ndogo 10, huku Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima akimtaka mkandarasi kuzingatia muda wa utekelezaji wa mradi huo.

"Hatuwezi kuhatarisha usalama wa raia hasa wanaotumia vivuko hivi kwa hiyo nawahakikishia kuwa vifaa hivyo tutafanya ufuatiliaji tukishirikiana na Shirika la Uwakala wa Meli (TASAC) unafanyika ili kuzingatia viwango vya kimataifa (IMS)," amesema Malima.