Waziri Kairuki ataka fedha za miradi zitumike kwa uadilifu

Muktasari:

  • Kairuki amesema hayo mjini Morogoro katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao kazi cha mafunzo ya Katibu wasaidizi wa Tume ya Utumishi wa walimu (TSC) kuhusu ufafanuzi wa kanuni za maadili na utendaji kazi katika utumishi wa walimu.

Morogoro. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Angellah Kairuki ametaka fedha za miradi zitumike kwa uadilifu na uzalendo wa hali ya juu ili kuleta tija na kuwa na matokeo chanya ambayo yatawezesha nchi yetu kupiga hatua kimaendeleo.

Kairuki amesema hayo mjini Morogoro katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao kazi cha mafunzo ya Katibu wasaidizi wa Tume ya Utumishi wa walimu (TSC) kuhusu ufafanuzi wa kanuni za maadili na utendaji kazi katika utumishi wa walimu.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, David Silinde alisoma hotuba ya waziri huyo kwa niaba yake pia alizindua kijitabu kipya cha kanuni za maadili ya kazi ya ualimu.

Waziri huyo amesema Rais Samia Suluhu Hassan amefanya juhudi kuhakikisha kuwa serikali inakuwa na miradi ya maendeleo ikiwemo mradi wa Boost kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia, kupitia mradi huo ameridhia kiasi cha Sh1.15 trilioni zielekezwa kwenye sekta ya elimu katika kuboresha zaidi elimu ya msingi.

“ Niwaombe wote tushirikiane vyema katika utekelezaji wa mradi huu ili kuleta ufanisi uliokusudiwa katika sekta ya elimu na  hata  Rais wetu amesisitiza fedha hizi za miradi zitumike kwa uadilifu na uzalenzo wa hali ya juu ili kuleta tija  na matokeo chanya,” amesema Waziri Kairuki.

Ametoa wito kwa taasisi zote zinazoshiriki kutekeleza mradi huo, kuwa na ushirikiano wakati wote wa utekelezaji  wa shughuli  za mradi ili kuhakikisha hakuna kinachokwama na kuongeza ufanisi.

“ Tunatakiwa kuunga mkono jithada za Rais wetu kwa kuhakikisha kuwa, tunazungatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyowekwa katika matumizi ya fedha za utekelezaji wa shughuli za mradi huu,” amesema Kairuki.

Pia ameonya kwa wasimamizi wa mradi huo kutobadilisha matumizi ya fedha za mradi kinyume cha shughuli zilizopangwa.
Waziri Kairuki amesema wadau wa maendeleo ikiwemo  Benki ya Dunia kwa kukubali kuufadhili mradi  huo na namna ambavyo wanavyoendelea kuziunga mkono juhudi za serikali yetu kuwaletea amendeleo wananchi.

Kwa mujibu wa waziri, mradi huo utatekelezwa kwa awamu kwa muda wa miaka mitano kuanzia 2021/2022 hadi 2025/26 na umelenga kujenga madarasa 12,000 , kuhakikisha shule 6,000 zinakuwa na mpango wa shule salama, kuongeza uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya awali kutoka asilimia 75 hadi kufikia asilimia 85.

Eneo jingine ni kuimarisha Mpango wa Mafunzio Endelevu ya Walimu Kazini (Mewaka), kununua vifaa vya Tehama kwa shule zaidi ya 800 za msingi na vituo vya walimu kwa ajili ya kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji na mafunzo endelevu ya walimu kazini.

Katika hatua nyingine ameitaka Tume hiyo kuhakikisha kuwa walimu wote nchini wanajengewa uwezo kuhusu kanuni za maadili ya  utendaji kazi katika utumishi wa walimu kwa kuzingatia ufafanuzi uliofanyika.
Pia ametaka uandaliwe utaratibu ili walimu wapya wanapoajiriwa waelimishwe kuhusu kanuni hizo na wanaposaini mikataba ya ajira wasaini kukubali kuzitekeleza.

Mwenyekiti wa TSC, Profesa Willy Komba  amesema kuwa tume hiyo imelazimika kufanya mapitio ya kanuni za maadili ya utendaji kazi katika utumishi wa walimu  kupitia kijitabu cha kanuni za maadili ya kazi ya ualimu  ambacho kimetumika tangu mwaka 2018 hadi sasa.

Profesa Komba amesema hatua hiyo ni kutokana  na kuwepo kwa mabadiliko ya sera, sheria, kanuni, taratibu, utandawazi na ongezeko la idadi  ya walimu  na kulazimu kufanya mapitio na kutoa ufafanuzi unaoendana na mabadiliko hayo.