Ripoti: Vijana tisa kati ya 10 hawana maadili

Khadija Shariff, Mkuu wa Programu Milele Zanzibar Foundation akielezea jambo wakati wa uzinduzi wa ripoti ya stadi za maisha na maadili kwa vijana

Muktasari:

Utafiti uliozinduliwa leo Januari 26, 2023 na Taasisi ya Regional Education Learning Initiative (Reli) kwa kushirikiana na taasisi ya Uwezo Tanzania umeonyesha kundi kubwa la vijana nchini halina maadili na stadi za maisha.


Dar es Salaam. Utafiti uliozinduliwa leo Januari 26, 2023 na Taasisi ya Regional Education Learning Initiative (Reli) kwa kushirikiana na taasisi ya Uwezo Tanzania umeonyesha kundi kubwa la vijana nchini halina maadili na stadi za maisha.

Ripoti hiyo ya 'Mchanganuo wa stadi za maisha na maadili katika Afrika Mashariki’ uliofanyika Julai, 2022 imehusisha vijana kuanzia umri wa miaka 13 hadi 17 katika wilaya 34, kaya 11,802 zikihusika na vijana 14,645 walihusishwa kutoka Tanzania Bara.

Utafiti huo umeonyesha kijana mmoja pekee kati ya 10 ana heshima na kujali maadili katika jamii, ambayo ni sawa na asilimia 12.5 ya vijana wote waliohusika katika utafiti huo.

Vilevile, utafiti huo umeonyesha kuwepo kwa uelewa mdogo wa vijana kujitambua na kutatua tatizo ambapo asilimia 16.8 pekee wana uwezo huo.

Akizungumzia matokeo ya utafiti huo, Mbunge wa Jimbo la Ubungo na mdau wa Elimu, Profesa Kitila Mkumbo amesema uelewa mdogo wa kutatua matatizo na stadi za maisha unasababishwa na hali ya ubora wa elimu.

"Vijana waliohusika kwenye uchunguzi huu wengi wapo shuleni, napata mshituko kuona Wanafunzi Wana uelewa mdogo wa kutatua matatizo na nalihusisha hili na ubora wa elimu yetu," amesema.

"Tukiwekeza hapa kwenye elimu Bora huko mbele kazi itakuwa rahisi kwenye stadi za maisha Kama kujitambua, kutatua matatizo, ushirikiano na heshima," ameongeza.

Akizungumzia suala la maadili ya vijana kushuka Tanzania, Mwenyekiti wa ngome ya vijana Chama cha ACT Wazalendo, Abdul Nondo amesema chanzo cha tatizo hilo ni mtindo wa maisha ya jamii ya sasa.

“Kwa umri wa vijana waliohusika kwenye utafiti huu ni wazi kwamba jamii inamchango mkubwa kwenye hili, na hata ukifanya utafiti kujua maadili ya jamii utapata majibu sawa kama ripoti hii,”amesema.

Nondo amesema malezi ya mzazi mmoja yameongezeka kwa sasa na inaweza kuwa ni sababu mojawapo ya heshima na maadili kwa ujumla kushuka kwa vijana na watoto, pia ameshauri Wizara ya elimu kuangalia mtalaa na ikiwezekana kuongeza somo la maadili na stadi za maisha.

Glori Olomi, Ofisa mawasiliano na utaratibu wa Taasisi ya Vijana ya Tanzania, Youth Development Initiative (TYDI) amesema kuhusu mmomonyoko wa maadili kwa kundi la vijana wa umri wa miaka 13 hadi 17 tatizo kubwa linasababishwa na wazazi.

“Wazazi wana jukumu kubwa kwenye malezi. Kwa sasa hivi watoto wadogo wanamiliki simu na wanaiga baadhi ya mambo ambayo sio utamaduni wetu kutokana na utandawazi,”amesema.