Vijana Afrika Mashariki watwishwa zigo vita dhidi dawa za kulevya
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, wakati akifunga Jukwaa la Vijana la Afrika Mashariki kuhusu Dawa za Kulevya (EAYFD) 2026, lililofanyika kwa siku tatu jijini Arusha.
Muktasari:
- Jukwaa hilo lililobeba kaulimbiu isemayo: ‘Kuharakisha Kupunguza Mahitaji ya Dawa za Kulevya Miongoni mwa Vijana wa Afrika Mashariki,’ limewakutanisha zaidi ya viongozi vijana 200 kutoka nchi 12.
Arusha. Vijana wa Afrika Mashariki na Kati wametakiwa kuwa mabalozi wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kuelimisha jamii, kuhamasisha kinga na kushiriki kwa vitendo katika matukio mbalimbali ya kudhibiti dawa hizo.
Wito huo umetolewa leo Jumapili Juni 7, 2026 na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo wakati akifunga jukwaa la vijana la Afrika Mashariki kuhusu dawa za kulevya (EAYFD) 2026, lililofanyika kwa siku tatu jijini Arusha.
Lyimo amesema vijana ni nguvu muhimu katika kupunguza matumizi ya dawa za kulevya na wanapaswa kuwa sehemu ya suluhisho endelevu la changamoto hiyo inayoathiri maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii.
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, wakati akifunga Jukwaa la Vijana la Afrika Mashariki kuhusu Dawa za Kulevya (EAYFD) 2026, lililofanyika kwa siku tatu jijini Arusha.
“Hampaswi kuonekana kama walengwa pekee wa programu za kupambana na dawa za kulevya, bali washirika katika kubuni na kutekeleza suluhisho endelevu. Nendeni sasa mkawe mabalozi wa mapambano haya katika jamii zenu,” amesema.
Amesema matumizi na biashara ya dawa za kulevya yameendelea kuwa tishio kwa jamii na uchumi wa nchi nyingi za Afrika, hali inayohitaji ushirikiano wa karibu kati ya serikali, taasisi na vijana wenyewe. Aidha, amesisitiza umuhimu wa elimu, mifumo ya msaada wa kifamilia na kuunda mazingira salama kwa vijana kujadili changamoto zao bila hofu.
Jukwaa hilo lililobeba kaulimbiu isemayo: ‘Kuharakisha Kupunguza Mahitaji ya Dawa za Kulevya Miongoni mwa Vijana wa Afrika Mashariki,’ limewakutanisha zaidi ya viongozi vijana 200 kutoka nchi 12.
Mratibu wa jukwaa, Halima Omar amesema lengo ni kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto na kuimarisha nafasi ya vijana katika utungaji wa sera za kupambana na dawa za kulevya.
George Ochieng kutoka Kenya amesema jukwaa hilo limewapa vijana maarifa na ujuzi wa vitendo, unaowawezesha kuwa viongozi wa mabadiliko katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, kuanzia jamii, taifa hadi ngazi ya ukanda.