Vijana wanavyoangamia kwa dawa za kulevya
Muktasari:
Siku moja jioni nikiwa Kituo cha Daladala cha Tabata Mwananchi nikisubiri usafiri wa kunipeleka nyumbani baada ya kumaliza kazi zangu.
Siku moja jioni nikiwa Kituo cha Daladala cha Tabata Mwananchi nikisubiri usafiri wa kunipeleka nyumbani baada ya kumaliza kazi zangu.
Mara nikaona kijana akiwa amevaa suruali ikiwa katikati ya makalio, alisimama kama vile mlemavu wa viungo.
Nilihisi anataka kuanguka kumbe lilikuwa ni pozi lake, shingo yake aliinamisha huku akiwa amefumba macho na kukoroma kama yuko usingizini.
Mdomoni udenda ulimtiririka mithili ya matone ya maji kwenye bomba, aliyumba huku na huku kama mtu ambaye amelemewa na usingizi na makosa pa kulala.
Masikini kumbe ni mwathirika wa dawa ya kulevya. Pamoja na hali aliyokuwa nayo hakuna aliyemsogelea wala kumsaidia, aliogopwa.
Siku nyingine nikiwa kwenye daladala, mara vijana wawili wa kiume na kike waliingia ndani ya daladala hiyo na kuketi kwenye viti.
Walikuwa wakitokwa na udenda mdomoni na muda wote waliinamia chini na walionekana wenye usingizi mzito kiasi cha mmoja kudondoka chini.
Ni ajabu! Kwa hali hii kuna kila dalili Taifa letu kuwa jalala na wodi za watu walioathirika na dawa za kulevya kama tusipokuwa waangalifu.
Nasema hivyo nikiwa na maana ya kwamba, kila ninapopita mitaani naona sura nyingi za vijana zikiwa zimelewa kumbe ni kutokana na dawa za kulevya.
Kinachochochea uteja
Ugumu wa maisha, ukosefu wa ajira kwa vijana, migogoro ndani ya familia, makundi mabaya kwa vijana, hatua za ukuaji ni moja ya vitu vinavyotajwa kuwa vichocheo vya matumizi hayo.
Abdurahiman Muhonda, makazi Mabibo jijini Dar es Salaam ni mmoja wa kundi la vijana hapa nchini ambao ni waathirika wa dawa hizo za kulevya.
Anasema, “Nilianza kutumia dawa za kulevya nikiwa na umri wa miaka 13, baada ya wazazi wangu kufariki na kuibuka mgogoro mkubwa ndani ya familia,” anasema.
Muhonda anasema kwamba, baba yake alikuwa na wake wawili na watoto 21 akiwa bado mdogo wazazi wake walitangulia mbele za haki, hivyo alibaki akilelewa na mama wa kambo na ndugu wengine.
“Nilikuwa mtoto wa mwisho kwa tumbo la mama yangu. Hivyo nilikuwa bado mdogo wakati wazazi wangu wanafariki. Wakubwa zangu waliondoka nyumbani na kutokomea kusikojulikana kutokana na manyanyaso,” anasema.
“Niliendelea kukaa na mama wa kambo lakini nikiwa sikuwa na uelekeo wa maisha. Ndugu zangu tuliozaliwa tumbo moja, wote walitoroka nyumbani.
Anasema alipofikisha miaka 13 aliamua kutoroka na kwenda mtaani, huko alikutana na genge la vijana wavuta bangi na kujiunga nao.
“Huo ulikuwa mwanzo wa kutumia dawa za kulevya kiasi ambacho kilibadilisha tabia yangu na mwonekano,” anasema.
Daktari wa magonjwa ya akili wa Hospitali ya Kairuki jijini Dar es Salaam, Ally Chirukile anasema kinachosababisha kukithiri kwa matumizi ya dawa za kulevya ni ile hali ya watu kuamini kwamba hawezi kufanya kitu bila kutumia dawa hizo.
Vijana wengi wamejenga hisia kwenye ubongo kwamba hawezi kufanya kitu fulani mpaka atumie dawa za kulevya.
Anasema ukishajenga kitu hicho kwenye akili ni lazima utatumia tu na ndicho kinachowasumbua vijana wengi hasa walio katika umri wa kubalehe.
Anafafanua kuwa, kijana anapokuwa kwenye umri wa kubalehe anakutana na mambo mengi na anakuwa anatamani kuonja kila kitu anachokiona na kukisikia masikioni mwake. Chirukile anasema kijana anapokuwa katika wakati huo anatakiwa kuwa kwenye uangalizi wa wazazi kwani ni kipindi hatari cha mtoto kuharibika na ni kipindi cha kuanza kuwa na marafiki wa aina mbalimbali. “Ikitokea kijana amekuwa na marafiki wabaya inakuwa ni hatari kwake kwani inakuwa ni rahisi kujiingiza katika matumizi ya madawa ya kulevya maana kuna msemo usemao ndege wenye manyoya ya kufanana hutembea pamoja,” anasema.
Anasema sababu nyingine inayochochea mambo hayo ni mitindo ya maisha, katika mtindo wa maisha kuna mambo mengi moja ni migogoro ndani ya familia, umaskini, ukosefu wa ajira na utandawazi.
Vitu hivi pia ni vichocheo vya vijana kujiingiza katika matumizi ya dawa ya kulevya, tukizungumzia suala la ukosefu wa ajira ni tatizo kubwa linalowakumba vijana wetu,” anasema.
“Ukitembea barabarani unaweza ukawahurumia vijana, walio wengi wana maisha magumu, hajui kesho atakula na atalalaje,” anasema.
Daktari wa magonjwa ya binadamu kutoka Mgodi wa Geita (GGM), Kiva Mvungi anasema: “Kijana akikosa udhibiti kutoka kwa wale wanaomlea humfanya aanze na hatimaye kudumu na tabia hizi,” anasema.
Anasema na msongo wa mawazo kutokana na sababu mbalimbali humfanya mtu atumie dawa ya kulevya kwa kuamini kwamba akitumia ataliwazika na kusahau matatizo yote aliyonayo, mfano matatizo ya kifamilia, ya kikazi na ya ndoa.
Madhara ya dawa za kulevya
Dk Chirukile anasema madawa ya kulevya ni vitu ambavyo hutumiwa kwa njia ya kunywa, kula au hata kujichoma, yakiingia mwilini yanaenda kupumbaza akili.
“Hubadili akili au fikra za mtumiaji kuwa tofauti na akili ya kawaida, kwa maana hufanya kazi kuliko vile inavyotakiwa kufanya,” anasema.
Anasema madawa haya hayatumiwi kwa lengo la kuleta tiba au manufaa katika mwili bali hutumiwa kwa lengo la kujistarehesha. Dk Chirukile anaeleza kuwa mtu anayetumia dawa za kulevya, anaweza kupata matatizo ya akili yaani kuwa mwendawazimu, kuishiwa nguvu za kiume, uwezo wa kufikiri, kuwa mgomvi pia zinaweza kusababisha kifo.
Mtaalamu wa afya ya akili, Dk John Chikomo anasema kijana anayetumia dawa hizo inakuwa ni rahisi kupata maambukizo ya magonjwa kama Ukimwi, saratani ya mapafu.
Kijana anaweza kupata ugonjwa wa mifupa na damu, kupungikiwa na nguvu kazi ya taifa, kwani wengi wanaotumia dawa za kulevya, hushindwa kufanya kazi zinazoleta maendeleo katika jamii na kuwa kama mizigo na wengine hufa katika umri mdogo kutokana na maradhi ya kuambukizwa.
Anasema wengi wanakuwa wagomvi wanapenda kufanya uhalifu kama vile ukabaji, ubakaji na unyang’anyi wa mali za watu, siyo kwamba ni akili zao timamu, hapana. Wanapomeza dawa hizo huwa zinaenda kushtua ubongo.
Dk Kairuki anasema athari nyingine ni kupata matatizo ya kimaumbile kama vile ukosefu wa uzazi, kukosa nguvu za kiume, upofu na kuvurugika kwa mfumo wa sauti.
Mfano mirungi hukosesha nguvu za kiume na bangi huvuruga au kuharibu baadhi ya mishipa ya fahamu na kusababisha upofu na matatizo mengineyo.
Anasema pia mbali na hiyo, mwathirika wa dawa ya kulevya kuna wakati anakuwa anabadilika na kuwa kama mtu aliyepungukiwa na akili, kupata maumivu makali ya kichwa, wakati mwingine kuwashwa.
Jitihada zinahitajika ili kumaliza tatizo la matumizi ya dawa za kulevya nchini. Vijana wanasema ili kumaliza tatizo hilo, Serikali iboreshe hali ya uchumi, vijana wapate ajira kwani ugumu wa maisha ndiyo unasababisha yote hayo.
Maoni au maswali tuma [email protected] au 0713247889