Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kivumbi cha uchaguzi, Mchengerwa apewa zigo

Viongozi walioapishwa wakila kiapo cha maadili Ikulu ndogo Tunguu Zanzibar Septemba 1, 2023. Picha na Ikulu

Dar/Zanzibar. Mwakani kuna kivumbi, nacho si kingine bali uchaguzi unaosubiriwa kwa hamu wa Serikali za Mitaa.

Kwa kuona ukubwa wa kivumbi hicho na kama mkakati wa Serikali kujipanga, Rais Samia Suluhu Hassan, amemtwisha mzigo Mohamed Mchengerwa aliyemteua kuwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Katika maelekezo yake kwa Mchengerwa, Rais Samia alitumia neno ‘kivumbi’ badala ya uchaguzi, kauli inayoweza kutafsiriwa kama msisitizo wa kuonyesha ukubwa na ugumu wa shughuli hiyo inayotarajiwa kufanyika mwakani.

Hata hivyo, wakati Samia akieleza hayo na akiwa na imani kubwa na Mchengerwa, baadhi ya wadau wa siasa, hasa kutoka vyama vya upinzani, wamesema Tamisemi isiwe sehemu ya usimamizi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Hoja yao inajikita katika mfumo wa usimamizi unaotoa mamlaka ya kusimamia uchaguzi kwa watumishi wa Serikali, baadhi wakitokana na chama tawala, hivyo kuona kwamba si rahisi kwao kutenda haki.

Baada ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alieleza haja ya uchaguzi huo kusimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) badala ya Tamisemi.

Katika uchaguzi huo, CCM ilishinda nafasi zote katika Serikali za Mitaa, hali iliyochochea malalamiko zaidi dhidi ya Tamisemi.

Samia akihutubia jana Ikullu ndogo ya Tunguu, Zanzibar, baada ya kuwaapisha viongozi wapya aliowateua na wengine kuwabadilisha wizara, alisema amemhamishia Mchengerwa Tamisemi akitambua mwakani kuna kivumbi.

“Mwakani kuna kivumbi na mimi nakujua, najua unaweza. Kivumbi kile kinafanana na kifua chako, najua unaweza, kwa hiyo nimekupeleka Tamisemi, ni kazi ili mwakani tuseme vizuri.

“Mengine sitaki kuyachambua hapa, wanasema usimwage mtama kwenye ndege wengi, sasa mtama wetu tutachambuana hapa ndani tukibaki katika kikao kazi,” alisema Rais.

Maelekezo hayo ya Rais yalitanguliwa na sifa katika utendaji wa Mchengerwa, ambaye awali alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.

“Tutakapowachambua hapa wengine ni mabingwa wa mabadiliko. Nimseme hapa Mchengerwa kwa mfano, nilipompeleka Utumishi mwanzo ninamteua, kaingia na kasi kubwa, kelele zikawa nyingi.

“Nikasema mmh! labda waziri wangu kazidi kupandisha mabega, nikampeleka Michezo; kaenda Michezo kazi aliyofanya mnaiona, kaacha kazi nzuri sana. Katoka Michezo nimempeleka Utalii,” alisema na kuongeza kuwa, huko aliweka mipango mizuri ambayo ikitekelezwa sekta hiyo itakua.

“Mipango aliyoiweka sekta ile nani anakwenda utalii, Angellah (Kairuki), sekta ile ukienda kufuata yaliyowekwa, mambo yanakwenda kupanda, Hassan (Abass - Katibu Mkuu) yupo pale amefanya kazi nzuri sana, wameweka mipango na waziri kwako ni kusimamia utendaji,” alisema.

Siri ya mabadiliko

Rais Samia alisema msingi wa mabadiliko hayo ni kuona mageuzi katika yale ambayo wananchi wameahidiwa.

“Kwa wale wapya nadhani mnayaona yanayotokea bungeni na mmekuwa mkipaza sauti kubwa kwa mawaziri, sasa yale mliyokuwa mnapazia sauti kayafanyeni ninyi.

“Wanasema ukitaka uhondo wa ngoma, sasa mpo kwenye ngoma tunatarajia mcheze kweli kweli na mlete yale mabadiliko mliyokuwa mkiyashauri,” alisema.

Wateule wapya walioapishwa ni Jerry Silaa (Waziri wa Ardhi), Alexender Mnyeti (Naibu Waziri Mifugo), Dunstan Kitandula (Naibu Waziri Utalii) na Judith Kapinga (Naibu Waziri Nishati).

Alisema mabadiliko hayo si adhabu, bali ni kuimarisha maeneo mbalimbali na anachotarajia ni jitihada kutoka kwa wateule na utumishi mzuri.

“Kuna mwingine akipata anasema sasa watanijua mimi ni nani, kwa hiyo sisi ni watumishi wa watu, katika utumishi wa watu uhusiano ni jambo zuri sana, sasa kujipandisha unataka kukaribia mbinguni hutatumikia watu,” alisema.

Rais Samia aliwataka watendaji hao kuwa wapole na kuacha kukurupuka wanapofanya mambo na uamuzi.

“Naombeni sana upole si ujinga, upole ndiyo maarifa. Unatulia unafikiri jambo mara mbili, mara tatu kabla hujatoa uamuzi na kauli, kwa hiyo naomba mkatulie mkatumikie watu,” alisema.

Kauli za viongozi

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi aliahidi ushirikiano kutoka katika Serikali yake kwa viongozi wote waliopewa nafasi za Muungano.

“Naridhika sana kwa mambo mengi ya ushirikiano yanayofanyika kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na ya Mapinduzi ya Zanzibar,” alisema.

Alieleza zipo taasisi zisizo za Muungano zinazijengea uwezo zile za Zanzibar, akisisitiza hiyo ni hatua nzuri na muhimu kwa masilahi ya Taifa.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alisema mabadiliko hayo ni safu nzuri kuelekea ushindi katika chaguzi zijazo.

“Mheshimiwa Rais ameona ni vyema apange safu inayoweza kufunga magoli zaidi ili twende kuanzia mwaka kesho, uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwaka unaofuata Uchaguzi Mkuu twende tukafunge magoli ya ukweli si ya kubabaisha,” alisema.

Aliwasisitiza viongozi hao kudumisha ushirikiano, akiwasihi kuzingatia falsafa ya Rais Samia ya R4, hasa ile ya mabadiliko.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Abdulrahman Kinana alisema ni wakati mwafaka kwa wateule wote kutathmini ilani ya uchaguzi ya chama hicho.

Kinana alisema wananchi wana matumaini makubwa na watendaji hao, hivyo wanatakiwa kufanya kazi kwa ufanisi kufikia matarajio hayo.

Alichosema Mchengerwa

Mwananchi lilizungumza na Waziri Mchengerwa kufahamu siri ya mafanikio yake kila wizara anayopelekwa.

Alisema misingi na falsafa ya uongozi, ilikwisha kuwekwa na Mwalimu Julius Nyerere na kubwa ni uzalendo.

Anasema wakati anasoma waliimba nyimbo za uzalendo na matamko mbalimbali ya uzalendo kwa Taifa yalikuwa yakitolewa ambayo yalimjenga.

Mchengerwa alisema ana miaka takriban 23 katika utumishi wa umma, akifanya kwenye mihimili yote mitatu ya Mahakama, Bunge na Serikali.

“Nimejifunza mengi na najua Watanzania wanataka nini. Tamisemi ni wizara ya wananchi, sijui afya, miundombinu na mengine mengi yapo Tamisemi ambayo ndiyo roho ya nchi...” alisema Mchengerwa na kuongeza:

“Tunawezaje kuwafikia wananchi kama tunakuwa na watumishi wazembe, tunawezaje kutatua matatizo ya wananchi kama tunajifungia ofisini, hatutimizi wajibu wetu ipasavyo?”

Katika kusisitiza hilo, Mchengerwa alisema: “Sasa wizara inarudi kwa wananchi, tutairudisha kwa wananchi, kwa viongozi kufanya kazi usiku na mchana, kuzungumza na wananchi na kutatua changamoto zao.”

Kuhusu uchaguzi wa mwakani, alisema: “Mimi sina hofu nao, kwani tafsiri ya Rais ni kwenda kufanya kazi...Kama kuna sehemu hatutafanya kazi, basi utakuwa ni mgumu, lakini kama tutafanya kazi, tutatatua kero za wananchi, miradi itatekelezwa, utakuwa uchaguzi mwepesi sana…’’