Kiwanda cha kuzalisha vitendanishi kuirahishia Serikali bajeti afya

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godween Molely akikata utepe kuashilia uzinduzi wa kiwanda cha kutengeneza vitendanishi wa afya cha Action Medeor Kibaha Mkoani Pwani. Picha na Sanjito Msafiri
Kibaha. Serikali ya Tanzania itaanza kunufaika na unafuu wa bajeti ya kila mwaka kwenye Wizara ya Afya kwa kununua vitendanishi kwa gharama nafuu siku chache zijazo baada ya kuzinduliwa kiwanda cha kutengeneza vitendanishi wilayani kibaha mkoani Pwani. Cha Action Medeor.
Kiwanda hicho ambacho kimejengwa kwa ushirikiano wa wadau kutoka nchi mbili Ujerumani na China ambayo kwa asilimia kubwa ndiyo wanaotoa teknolojia ya uzalishaji kimezinduliwa leo na Naibu Waziri wa Afya, DK Godwin Mollel kwa niaba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambacho uwekezaji wake ni Sh5 bilioni.
Akizungumza leo wakati wa uzinduzi huo waziri huyo amesema kuwa Tanzania imekuwa ikitumia bajeti kubwa ya pesa kuagiza dawa na vitendanishi nje ya nchi lakini kwa mujibu wa uongozi wa kiwanda hicho unaonyesha kuwa kitakapoanza uzalishaji watauzia bei ya chini ya asilimia 50 jambo ambalo linaleta matumaini na faraja kwa nchi na wananchi kwa ujumla.
“Serikali imeendelea kujenga vituo vya afya na hospitali nyingi nchini na kazi kubwa ambayo ilikuwa ikiumiza kichwa ni bajeti yavitendanishi hivyo sasa hatua ya kujengwa kiwanda hiki itailetea Serikali unafuu na pia itakuwa faida kwa wananchi kwani watapata tiba zote hapa ndani ya nchi kwa kuchangia gharama nafuu,”amesema.
Naibu Waziri wa Afya upande wa Zanzibar, Hassani Hamisi Hafidh amesema kuwa wakati Serikali ikiendelea kufanya jitihada za kusogeza huduma za afya ka jamii, baadhi ya watu wameendelea kubeza jitihada hizo na kutoa maneno yasiyona staha jambo ambalo linapaswa kupuuzwa.
Amewataka viongozi wa ngazi za wilaya na mikoa Tanzania Bara kutowafumbia macho baadhi ya wataalamu wa afya ambao wamekuwa wakifanya kazi kilegevu na hata kusababisha vifo kwa wananchi na badala yake wawaripoti wizarani ili hatua za mapema zichukuliwe dhidi yao.
Mkurugenzi mtendaji wa kiwanda hicho, Christoph Bonsmann amesema kuwa kwa kuanzia wametoa ajira zaidi ya 20 kwa watanzania na kwamba kadri siku zinavyoendelea wataongeza idadi hiyo huku wakizingatia taratibu za kulipa kodi mbalimbali kulingana na sheria za nchi.
Amesema kuwa kadri siku zinavyoenda wataendelea kuzalisha bidhaa mbalimbali zinazokidhi viwanda na ubora ili kuwasaidia Watanzania katika maswala ya huduma za upatikanaji wa matibabu.