Kizungumkuti uzalishaji pamba Katavi

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko akitoa maagizo kwa viongozi kufuatilia kwa ukaribu uzalishaji zao la pamba. Picha na Mary Clemence

Muktasari:

  • Usimamizi mbovu katika uzalishaji wa pamba mkoani Katavi, watajwa kama chanzo kutofikia malengo ya uzalishaji na hivyo kushindwa kukidhi mahitaji ya kinu cha kuchambua pamba cha kampuni ya NGS.

Katavi. Usimamizi mbovu katika uzalishaji wa pamba mkoani Katavi, watajwa kama chanzo kutofikia malengo ya uzalishaji na hivyo kushindwa kukidhi mahitaji ya kinu cha kuchambua pamba cha kampuni ya NGS.

Wakulima wa pamba katika msimu wa 2022/2023 kupitia vyama vya ushirika wamezalisha tani 7.6 ilihali kiwanda hicho kina uwezo wa kuchambua tani 50 kila mwaka.

Changamoto hiyo inaathiri kiwanda kukosa malighafi ya kutosha licha ya kuwekeza kwa gharama kubwa na kwamba pia Serikali inapata mapato kidogo kutokana na wakulima kuzalisha kwa kiwango cha chini.

Hayo yametajwa katika kikao cha tathmini ya uzalishaji wa zao hilo mkoani hapa, na Ofisa Kilimo Mkoa wa Katavi, Farid Abdallah ambapo amesema pamoja na mambo mengine, uduni huo wa uzalishaji unachingiwa na wakulima kukosa usimamizi wa kutosha.

Bwana Kilimo huyo ametaja changamoto nyingine kuwa ni kutopandwa kwa mbegu zote zinazosambazwa kwa wakulima.

“Uwepo wa mashambulizi ya wadudu (chawa jani) umesababisha kushusha uzalishaji, pia wakulima kutong’oa masalia ya pamba ambayo yanasababisha ongezeko la wadudu na magonjwa kwenye uzalishaji,” amesema ofisa huyo.

Kutokuwepo mafunzo ya rejea ya mara kwa mara kwa Maafisa ugani/kilimo katika vituo vya utafiti inapelekea kasi ndogo ya uhamasishaji.

Kwa upande wake Mkurungezi wa kinu hicho, Njalu Silanga ameomba tafiti zifanyike ili kubaini maeneo yanayohitaji mbole na yasiyohitaji.

“Nimebaini kuna baadhi ya maeneo ambayo ardhi yake haihitaji kuwekewa mbolea lakini wakulima wanatumia, inawaongezea gharama zisizo za msingi,” amesema Silanga.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko akitoa msimamo wa Serikali, amesema kuwa katika msimu wa 2023/2024 Wakuu wa Wilaya wanatakiwa kufuatilia suala ugawaji mbegu na uzalishaji.

Amesema uzalishaji wa pamba msimu uliopita hauendani na mbegu zilizosambazwa kwa wakulima ambazo zilikuwa tani 8.7 na kwamba matarajio ilikuwa zipandwe kwenye heakari 43,605,000 na kwamba zingezalisha tani 17.4.

“Kwanini uzalishaji uwe tani 7.6? Mbegu zilikwenda wapi? Wakuu Wilaya hakikisheni mnadhibiti upotevu wa mbegu ambazo hazifiki shambani,” amehoji RC huyo na kutoa maagizo.

Kutokana na hali hiyo mkoa umejiwekea mikakati ya kuongeza uzalishaji wa pamba msimu wa 2023/2024 ambapo unatarajia kuvuna kilo tani 20,000.