KKKT Kijitonyama waja na utaratibu mpya

Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kijitonyama Dk Eliona Kimaro.

Muktasari:

  • Licha ya uchache wa waumini kujitokeza katika ibada ya asubuhi (Morning glory) baadhi ya viongozi wa Kanisa KKKT Kijitonyama wameanza utaratibu ikiwemo kufahamu baadhi ya taarifa za waumini ili kuhakikisha ibada zinafanyika.

Dar es Salaam.Siku moja baada ya Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kijitonyama Dk Eliona Kimaro kupewa likizo, ibada ya asubuhi (Morning glory) imefanyika huku viongozi wakiweka utaratibu mpya.

Mwananchi ilifika kanisani hapo leo Jumatano Januari 18, 2023 saa 12:25 asubuhi na kukuta ibada ya 'Morning glory' ikiendelea huku baadhi ya viongozi wakiwa kwenye lango kuu la kanisa hilo na utaratibu wa kufahamu baadhi ya taarifa za waumini ikiwemo jumuiya anayosali na kama ana namba.
Licha ya uchache wa waumini pia baadhi ya viongozi wa kanisa hilo wamehakikisha ibada hiyo inafanyika kutokana na baadhi ya waumini kuzuia jana kufanyika ile ya 'evening glory' baada ya kuandamana na mabango wakimtaka mchungaji wao Dk Kimaro.
Utaratibu huo wa kutambua waumini umeanza kutumika baada ya sakata la mchungaji Kimaro kushika kasi jana Januari 16, 2023 iliposambaa video katika mitandao ikimuonyesha mchungaji huyo akiwaeleza waumini wake kuwa amepewa likizo ya siku 60 baada ya kuitwa katika ofisi ya msaidizi wa askofu na kufanya kikao na mkuu wa Jimbo la Kaskazini.

"Semina yetu ni ya wiki mbili (Semina ya neno la Mungu), lakini niliitwa ofisi ya msaidizi wa askofu, tulikuwa na kikao na Mkuu wa Jimbo la Kaskazini Mchungaji (Jacob) Mwangomola. Nimepewa barua ya likizo ya siku 60 kesho asubuhi (leo Jumatano) atahubiri Mchungaji Anna na ataendelea kuwa Mchungaji wenu," amenukuliwa kwenye video hiyo.
“Kwa mujibu wa barua nitarudi Machi 17 (2023) na sitakuja hapa, barua inanilekeza kuripoti Makao Makuu ya Dayosisi. Kwa hiyo mimi ni Mchungaji wa Lutherani nina heshimu kiapo changu cha kichungaji na kuishi katika kiapo na maadili…
“Pia kwa neema ya Mungu kwa sababu hiyo imenilazimu kutii na kwenda kwenye hiyo likizo na baadaye kuripoti kwenye ofisi ya askofu kama nilivyoelekezwa,” anasema Mchungaji Kimaro katika video hiyo.
Mbali ya video hiyo, ipo nyingine iliyosambaa ikiwaonyesha baadhi ya waumini wa usharika huo wakiangua vilio, wakati mchungaji huyo akifanya maombi ndani ya kanisa hilo wakati akiaga.
Hata hivyo, mmoja wa waumini ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema, watu wamevunjika moyo kutokana na kilichofanyika haiwezekani mchungaji apewe likizo ya siku 60, wakati ndio mwanzo wa semina.
“Pamoja na kuwepo mgawanyiko kila mtu ana imani yake siyo wote waliokuja kusali hapa wanafurahishwa na kilichotokea, ndio maana hata viongozi wanajitahidi ibada hii isivurugike kama ile ya jioni watu ni wachache,”alisema muumini huyo.
Muumini mwingine Helleni Minja anayefanya biashara nje ya kanisa hilo amesema, asubuhi ni vigumu kuzuia ibada kutokana na watu wengi kwenda kazini lakini ibada ya jioni na Jumapili hazitafanyika hadi mwafaka upatikane.


Msimamo wa waumini
Jana baada ya kushindikana kufanyika kwa ibada ya jioni waumini hao walifanya kikao cha pamoja na kukubaliana kutoingia ndani ya Kanisa hilo hadi watakaporudishiwa Mchungaji wao Dk Kimaro.
Uamuzi huo ulifikiwa na waumini hao baada ya kukubaliana kukutana chini ya mti katika viwanja hivyo kila siku saa 11:00 jioni hadi pale mchungaji atakaporudishwa.
 "Tumesimama hapa kwa kuwa tuna maumivu yanayogonga mioyo yetu. Tuko hapa kwa kuwa hatujui kuhani wetu alipo,"alisema mmoja wa waumini.
Walisema utaratibu uliotumika kumsimamisha mchungaji huyo siyo sahihi kwani aliyemsimamisha alipaswa kufika usharikani hapo na kuwaeleza waumini kilichotokea.