Kodi mpya za digitali: Mtihani kwa uchumi

Kodi mpya za digitali: Mtihani kwa uchumi

Muktasari:

  • Utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu unaoanza wiki ijayo utakuwa changamoto kubwa kwa sekta ya huduma za fedha kidigitali kutokana na kuanzisha tozo mpya katika huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi na katika kadi za simu, wadau katika sekta hiyo wamesema.

Utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu unaoanza wiki ijayo utakuwa changamoto kubwa kwa sekta ya huduma za fedha kidigitali kutokana na kuanzisha tozo mpya katika huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi na katika kadi za simu, wadau katika sekta hiyo wamesema.


Huku simu za mkononi zikiwa kitu muhimu katika mabadiliko ya kidigitali na fedha na kuthibitisha thamani yake wakati wa janga la virusi vya corona, Covid-19, wengi walitarajia mabadiliko ambayo yangepunguzia mzigo mlipakodi kwa pande zote; watoaji huduma na watumiaji.


Wataalamu katika sekta hii wanasema tozo mpya hazitaathiri mipango ya uwekezaji, lakini pia wanataka kuangaliwa upya kwa malengo ya kibiashara na mikakati ya uendeshaji.


Pia wanasema hatua za kikodi katika bajeti ya mwaka 2021/22 zinaweza kudumaza ukuaji wa fedha za kidigitali na kuathiri ajenda ya taifa ya ujumuishaji kifedha. Mwisho wake, wanaelezea, juhudi za kuifanya Tanzania za kuwa na uchumi wa kidigitali na nia ya taifa ya kuwa na jamii ambayo haitumii fedha taslimu, haitakuwa kipaumbele.

Kodi mpya za digitali: Mtihani kwa uchumi


Akizungumza baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya serikali mapema mwezi huu, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Standard Chartered Bank nchini Tanzania na mwenyekiti wa Chama cha Maofisa Watendaji Wakuu (CEO RoundTable), Sanjay Rughani, alisema kodi zilizopendekezwa katika miamala ya fedha kwa simu za mkononi na katika SIM Card zinaweza kukwamisha ajenda ya ujumuishaji wa makundi mbalimbali katika huduma za fedha na kuwa na athari nyingine.


“Uamuzi wa kuweka kodi mpya katika uhamishaji wa fedha kwenye simu na kurudisha tozo katika kadi za simu utakuwa na athari katika ukuaji wa muda mrefu wa kiuchumi na imara wa kifedha,” ofisa mwandamizi wa Chama cha Waendeshaji Huduma za Simu za Mkononi (TAMNOA) alisema akiomba jina lake lisitajwe.


“Ukuaji tuliouona katika sekta utapungua kwa kiwango kikubwa,” alisema mtaalamu wa mawasiliano ya nje wa kampuni ya huduma za simu hizo alipoongea na The Citizen saa chache kabla ya Bunge kupitisha bajeti ya Sh36.33 trilioni kwa ajili ya mwaka ujao wa fedha.


Kutekeleza mpango wa kwanza wa fedha wa serikali ya awamu ya sita, Hazina inapanga kukusanya takriban Sh1.6 trilioni kutokana na tozo za kodi zilizoanzishwa katika sekta ya wasiliano ya simu kwa mwaka 2021/22.


Fedha zitakazokusanywa, ambazo ni Sh10-10,000 katika kila muamala na Sh0-200 kwa kila kadi ya simu kwa siku, zitatumiwa katika miradi miwili mikubwa inayoendelea; Sh2.03 trilioni kwa ajili ya kutekeleza mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR). Fedha nyingine zitatoka katika tozo zilizowekwa katika mafuta na vinywaji vikali, yaani Sh60,769.35 milioni.


Akiwasilisha makadirio hayo jijini Dodoma mwezi huu, Dk Nchemba alisema: “Napendekeza kufanya mabadiliko katika Sheria ya Mawasiliano ya Posyta na Kielektroniki kama ifuatavyo: “Kuweka tozo ya Sh10 hadi Sh10,000 katika kila muamala wa fedha wa simu wa kutoa na kupokea. Kiwango cha tozo kinatofautiana kutegemea na thamani ya kila muamala wa kutoa au kupokea. Pendekezo hili linategemewa kuongeza mapato ya serikali kwa Sh1,254,406.14 milioni.


“Kuweka kodi ya Sh10 hadi Sh200 kwa siku kwa kadi za simu kutegemea na uwezo wa mtumiaji kuongeza salio. Pendekezo hili linatarajiwa kuongeza mapato ya serikali kwa Sh396,306 milioni.”


Licha ya wananchi wanapinga kodi hizo na wataalamu kushauri kuwa tozo hizo zitadumaza ukuaji na maendeleo ya sekta, baadhi wanasema athari hasi katika maendeleo zitakuwa za muda mfupi na ndogo.


Wataalamu wa taasisi ya kukuza masoko yenye makao yake makuu jijini London, Tellimer Group wanasema awali uhamisho wa fedha utapungua, lakini utainuka ndani ya miezi michache kama ilivyokuwa nchini Kenya wakati serikali ilipochukua hatua kama hiyo.
“Kama Kenya, tunaamini kodi mpya zitapunguza uhamishaji fedha kwa miezi michache ya mwanzo baada ya kuanza kutumika kwa kuwa wateja watakasirika, lakini kiwango kinatarajiwa kukua kwa kiasi kikubwa baadaye – hizi ni huduma ambazo mteja hana mbadala,” inasema Tellimer.


Katika hatua ya kupandisha matumizi ya data, serikali imeondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika simujanja, vishkwambi na modem. Waziri Nchemba alisema hatua hiyo inataka kuhakikisha lengo la kufikia asilimia 80 kwa watumiaji wa internet linafikiwa ifikapo mwaka 2025 kutoka asilimia 46.
Katika mapendekezo yake kwa Kamati ya Bajeti ya Bunge kabla ya bajeti ambako alipendekeza kuondoa VAT katika simujanja, TAMNOA ilisema umiliki wa simu ulikuwa chini nchini, ukiwa asilimia 25.


Akitoa maoni kuhusu uamuzi wa kuondoa VAT katika simujanja wiki iliyopita, muasisi na mmiliki wa taasisi ya Lase Financial Services Limited, Lawrence Mlaki, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa kuna uwezekano kodi hizo mpya zitaathiri watu wa kipato cha chini.


Alisema kurudisha kodi katika kadi za simu kutapandisha gharama za huduma hizo na unafuu wa simu. Awali tozo hiyo iliwekwa Julai mwaka 2013 lakini ilidumu kwa miezi sita tu. Tangu wakati huo kumekuwa na wasiwasi katika sekta kuwa ingerudishwa.


Vyanzo katika sekta hiyo vinasema ni baada ya kuondolewa kwa tozo serikali ilipandishwa ushuru katika huduma ya mawasiliano ya simu za mkononi hadi kufikia asilimia 17 kutoka asilimia 14.5. Kupunguzwa kwa ushuru huo lilikuwa moja ya mapendekezo ya TAMNOA ambayo hayakuzingatiwa na serikali.


“Tunelewa kuwa kupanda kwa kiwango cha ushuru kutoka asilimia 14.5 hadi asilimia 17 kulikuwa hatua ya muda mfupi kufidia fedha ambazo serikali ilipoteza katika mapato kutokana na kuondolewa kwa kodi ya kadi za simu ya Sh1,000 katika mwaka wa fedha wa 2013/14,” ilisema TAMNOA katika mapendekezo yake ya bajeti.


Uongozi wa wakati huo ulikuwa umeahidi kiwango cha asilimia 14.5 kwa mwaka uliofuatia, hii inamaanisha – kuanzia mwaka 2014/15 na kuendelea. Hilo halikufanyika na linaifanya Tanzania kuwa ya pili kwa kiwango cha juu cha ushuru katika huduma za simu za mkononi barani Afrika, ikiwa imezidiwa na Zambia.
TAMNOA ilisema asilimia tatu ya ushuru iliyopendekezwa ingeongeza faida katika sekta, kukuza uwekezaji ambao ambao mwishoni ungeiongezea serikali kodi zaidi.


Chama cha Mfumo wa Simu za Mkononi Duniani (GSMA) kinasema kuwa tozo katika muda wa maongezi ingeweza klupunguzwa hadi asilimia 12, hatua ambayo ingeongeza watumiaji milioni 2.4 na hivyo kukuza mapato ya serikali kwa dola 58 milioni za Kimarekani (sawa na takriban Sh135 bilioni za Kitanzania) kw amwaka na kuongeza Pato la Ndani kwa dola 438 milioni, miaka mitano baada ya mabadiliko ya kodi.


“Utozaji kodi katika sekta ya simu za mkononi unaweza kuzaa manufaa ya muda mfupi, lakini hili linagharimu maendeleo na ukuaji wa muda mrefu wa kiuchumi na kijamii na hivyo utakinzanana na uzalishaji.


“Kwa kupunguza kodi katika sekta ya simu za mkononi, serikali ya Tanzanian haitaweza kuendeleza ukuaji wa kidigitali na ujumuishasji wa kifedha pekee, bali pia kuweza kupata tena mapato makubwa ya kodi kwa kutumia mkongo ambao una ufanisi na ni mpana.”

Imeandikwa na Costantine Muganyizi