Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KONA YA WASTAAFU: Pale mstaafu anapohitaji pensheni iongezwe…!

Muktasari:

  • Kama ilivyo kwa watu wengi ingawa si wote, mzee wetu mstaafu angependa naye kuamini kwamba daima fedha inakuwa haitoshi. Jinsi mtu anavyopata nyingi ndivyo matumizi nayo yanavyoongezeka.

Kama ilivyo kwa watu wengi ingawa si wote, mzee wetu mstaafu angependa naye kuamini kwamba daima fedha inakuwa haitoshi. Jinsi mtu anavyopata nyingi ndivyo matumizi nayo yanavyoongezeka.

Hata wale tunaoaminishwa kwamba ni matajiri wa dunia nzima, nao wanahaha kuongeza walichonacho, pengine katika kuthibitisha kwamba kweli, daima hela haitoshi.

Kwenye msimamo huu mzee mstaafu angependa kuongeza ‘uwe nazo basi’! Kwamba kwanza uwe nazo halafu hayo ya kuongezeka matumizi yafuate baadaye!

Mstaafu wetu haachi kutabasamu kwa uchungu anapoangalia pensheni yake ya mwezi ambayo hata wajukuu zake wameipa hadhi ya ‘laki si pesa’ na anaishia kujiuliza ana matumizi gani ambayo ‘laki si pesa’ yake ya mwezi ikiongezwa ataingia kwenye daraja la ‘fedha haitoshi’, maana tayari yeye fedha haitoshi!

Mstaafu wetu amestaafu miaka 15 iliyopita. Bado anapokea pensheni hadhi ya ‘laki si pesa’ aliyokuwa akipokea miaka hiyo 15 iliyopita. Ana bahati. Kuna wasaafu wenzake waliostaafu miaka 25 iliyopita nao bado wanapokea pensheni ya Sh50,000 kwa mwezi! Elfu hamsini pensheni kwa mwezi? Mstaafu na wajukuu zake wameshindwa hata kuipa hadhi yake elfu hamsini, labda tu ‘hamsini, tunataniana?’!

Mzee wetu anakiri miezi ya mwanzo wakati anaanza kupokea pensheni yake ya ‘laki si pesa’ miaka hiyo ya 90 mwishoni zilionekana nyingi za kutamba na kutanua! Nani atapokea pensheni ya laki moja na elfu tano na visenti kadhaa hata akilala tu mwezi mzima, asitambe na kutanua? Unaambiwa wakati huo hata hadhi ya ‘laki si pesa’ ilikuwa haijatungwa!

Ikatungwa. Mstaafu akaanza kukiona cha moto na pensheni yake ya laki moja na elfu tano na visenti kadhaa. Akaanza kuona kumbe pensheni yake ya laki moja na vishilingi na visenti kadhaa sio mali kitu. Ni ‘laki si pesa’ tu! Ni ‘hamsini, tunataniana?’ tu. Akaanza kuona ‘daima fedha haitoshi’ kwa maana halisi na sio kwa usemi wa mfano tu! Ilikuwa haitoshi kweli!

Tushukuru kwamba mstaafu wetu hajafikia kwenye ule mfano ulio kwenye vitabu vitakatifu vya dini wa mfanyabiashara ambaye baada ya kuchumia sana juani na kujaza maghala yake akajipongeza kwa kuuambia moyo wake sasa upumzike, unywe, ule na ufurahi, kumbe Mungu anamtizama tu na kumuambia kimoyomoyo; “Zumbukuku wee, usiku huu huu wanakuja kuchukua roho yako…na kukuelekeza Kinondoni!”

Bado mstaafu wetu hajaelekezwa Kinondoni, lakini kulinganisha pensheni yake ya ‘Hamsini? Tunataniana!’ ama ya ‘laki si pesa’ na hali halisi, cha moto anakiona…na kuna mtu sasa hivi atamuelekeza Kinondoni!

Hapo katikati hizi benki zenu za kitekinilojia zikaingia kati na kuchangamkia dili. La kumkopesha mstaafu hela kwa dhamana ya pensheni yake tu. Hawana haja ya kuona nyumba wala shamba wala nini, pensheni tu. Kutokana na shida zao, wastaafu wengi wakachangamkia dili hili. Na mwezi ule ule unapochukua mkopo wako, mabenki haya ya kitekinolojia yanafanya vitu vyao vya kukata riba na tozo zao zisizotofautisha huyu ni mstaafu asiye na kipato kinachoeleweka na huyu ni mfanyabiashara, woote machinjioni!

Baada ya benki kufanya vitu vyake vya kukata riba na tozo vya mkopo wa wastaafu, kutoka ‘laki si pesa’ yake ya laki na elfu tano na vichenji kadhaa mstaafu wetu sasa anapokea elfu arobaini na nne na visenti kadhaa kwa mwezi kwa miaka mitatu ijayo kulipa mkopo! Yule ‘hamsini, tunataniana’ sasa anapokea elfu tano mpaka kumi na tano pensheni yake ya mwezi kwa miaka mitatu ijayo kulipia mkopo wa benki usioangalia makunyanzi.

Mstaafu wetu anafahamu wazi pensheni yake inatokana na alichokatwa mwenyewe kutoka kwenye mshahara wake. Mwajiri wake akaongeza kidogo na mstaafu akawekewa kwenya kibubu chake cha akiba ya uzeeni. Ndicho hiki sasa kimeishia kukatwa kama riba na tozo na benki zenu hizi za kisiku hizi ambazo haziangalii makunyanzi, bali zinakata tu, awe ni mstaafu asiye na kipato chochote bali pensheni tu, au awe ni mfanyabiashara wa ‘kiasi cha mboga tu!’ Woote machinjioni!

Miaka 60 baada ya Uhuru mstaafu anadhani sasa wakati umefika wa kujipapasa sawasawa mifukoni, ili mstaafu alipwe kinachomstahili. Kinachoonyesha kwamba yeye kweli ni mstaafu aliyeikuza nchi hii toka ikiitwa Tanganyika hadi kuitwa Tanzania.

Yeye ndiye anayeijua nchi hii ilikotokea na inakokwenda. Ndiye anayejua vifaa vilivyotumika kuitengeneza ‘keki ya Taifa’, ingawaje kwa jinsi ilivyo yeye hajaila na inatafunwa na wenye meno tu, aliowasomesha bure mwenyewe kwa kodi yake! Yeye akisogelea tu anaishia kuambiwa ana kisukari haruhusiwi kula vitu vyenye sukari! Jamani! Hata keki aliyoshiriki mwenyewe kuitengeneza?

Serikali ijipapase na kumuongeza msaafu pensheni yake. Inawezekana. Wale wa ‘laki si pesa’ na wale wa ‘hamsini, tunataniana?’ wapate pensheni kama laki mbili unusu au hata zaidi, kwa mwezi. Inawezekana. Wapensheni wenyewe wamebaki wangapi, kama nusu nzima hawajatangulia Kinondoni duniani kote, wastaafu ni kundi muhimu katika jamii. Tanzania tusiwe tofauti. Kwa pensheni hii ya ‘hamsini, tunataniana?’ Tunacheza.

Tusomane Ijumaa ijayo.

0754 340606 / 0784 340606