Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kongamano la Utumishi wa Umma kufanyika Dar, Dk Nchimbi kuwa mgeni rasmi

Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dk Ernest Mabonesho, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumanne, Juni 16, 2026.

Muktasari:

  • Taasisi za umma na binafsi, wataalamu, watafiti pamoja na wadau wa maendeleo wameshauriwa kushiriki kikamilifu katika kongamano hilo ili kuchangia mjadala kuhusu mustakabali wa utumishi wa umma na maendeleo ya taifa.

Dar es Salaam. Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), kwa kushirikiana na Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar (IPA), kimeandaa Kongamano la Pili la Utumishi wa Umma Tanzania litakalofanyika Juni 18, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo ambalo litawakutanisha takribani washiriki 300 kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumanne, Juni 16, 2026, Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dk Ernest Mabonesho, amesema kongamano hilo linafanyika chini ya kaulimbiu: Nafasi ya Utumishi wa Umma katika Kufanikisha Malengo ya Dira za Taifa 2050.”

Amesema kaulimbiu hiyo imechaguliwa kwa kuzingatia hatua ambayo Tanzania imefikia katika maandalizi na utekelezaji wa maono ya maendeleo ya muda mrefu.

Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa Tanzania Bara inalenga kujenga uchumi shindani unaotegemea viwanda, maarifa, ubunifu na matumizi ya teknolojia za kisasa, huku Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 ikilenga kuimarisha uchumi kupitia sekta za kimkakati, zikiwemo uchumi wa buluu, utalii wa kisasa, kilimo chenye tija na mifumo ya kidijitali.

“Katika kufanikisha maono haya, utumishi wa umma una nafasi ya kipekee kama chombo kikuu cha utekelezaji wa sera, mipango na programu za maendeleo.

“Kongamano hili litatoa jukwaa la kutafakari namna bora ya kujenga utumishi wa umma wenye ufanisi, weledi, ubunifu na uwezo wa kukidhi mahitaji ya taifa la sasa na la baadaye,” amesema.

Ametaja malengo ya kongamano hilo kuwa ni kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mchango wa utumishi wa umma katika kufanikisha Dira za Taifa 2050, kuimarisha uwezo wa taasisi za umma katika kuzingatia misingi ya uwajibikaji, weledi na uadilifu, pamoja na kuchambua matumizi ya teknolojia na ubunifu katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Malengo mengine ni kukuza ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kueneza mbinu bora za kiutawala miongoni mwa taasisi mbalimbali nchini.

Kongamano hilo litahusisha mada mbili kuu zitakazowasilishwa na viongozi waandamizi wa Serikali.

“Mada ya kwanza itawasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu Zanzibar, Dk Saada Mkuya Salum, kuhusu nafasi ya utumishi wa umma katika kukuza ubora wa taasisi na kuchangia utekelezaji wa malengo ya Dira 2050.

“Mada ya pili itawasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, ambaye atajadili mchango wa ubunifu na mabadiliko ya kidijitali katika utumishi wa umma kwa ajili ya kuchochea maendeleo endelevu.”

Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar (IPA), Dk Salum Rashid Mohammed amesema kongamano hilo ni mwendelezo wa ushirikiano uliopo kati ya vyuo hivyo viwili katika kukuza taaluma na ubora wa utumishi wa umma nchini.

Amesema kongamano la kwanza lilifanyika Zanzibar mwaka jana na kwamba mafanikio yake yamechochea kuandaliwa kwa kongamano la pili litakalofanyika Dar es Salaam.

“Kuandaa kongamano la aina hii si jambo rahisi, lakini tunaamini litazalisha mawazo, mapendekezo na uzoefu ambao utasaidia kuboresha utendaji wa taasisi za umma na utoaji wa huduma kwa wananchi,” amesema.