Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Korti yaelezwa heroin zilivyofichwa, kunaswa

Muktasari:

  • Mshtakiwa Salum Jongo (45), mkazi wa Mbezi Beach anadaiwa kuficha dawa hizo kwa Tatu Nassoro (45) baada ya kuhofia kupekuliwa nyumbani kwake

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeleezwa jinsi mfanyabiashara, Salum Jongo alivyoficha kilo 51 za dawa za kulevya aina ya heroin nyumbani kwa mpenzi wake, Tatu Nassoro, eneo la Vetenari, wilayani Temeke.

Jongo (45), mkazi wa Mbezi Beach anadaiwa kuficha dawa hizo kwa Tatu (45) baada ya kuhofia kupekuliwa nyumbani kwake.

Wawili hao pamoja na Ernest Semagoya (48), mkazi wa Mbezi Beach na Amin Sekibo, mkazi wa Mbezi Tangibovu, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 78/2020.

Katika mashtaka matatu wanadaiwa kutakatisha Sh62.9 milioni, kuongoza genge la uhalifu na kusafirisha heroin zenye uzito wa kilo 51.47.

Jana, Wakili wa Serikali, Glory Kimaro akishirikiana na Cuthbert Mbilingi, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ajali Milanzi walidai hayo walipowasomea washtakiwa maelezo ya mashahidi na vielelezo baada ya upelelezi wa kesi kukamilika.

Hatua hiyo ya usikilizwaji ilifanyika kwa saa sita, ulinzi uliimarishwa katika chumba cha Mahakama ambako kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa.

Wakili Glory alidai katika kuthibitisha mashtaka, upande wa Jamhuri unatarajia kuwa na mashahidi 11 na vielelezo 14, yakiwamo maelezo ya onyo ya Jongo, hati ya upekuzi, hati ya ukamataji mali, hati za kusafiria za Semagoya na Jongo, magari manane ya washtakiwa na ripoti ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Amedai mashahidi wanatarajia kutoa ushahidi Mahakama Kuu, Kitengo cha Uhujumu Uchumi na Makosa ya Rushwa, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi.


Wakili Kimaro amedai Jongo alikamatwa Septemba 7, 2020, nyumbani kwake Mbezi Beach, baada ya Sekibo kuwaeleza askari polisi kuwa alipeleka heroin nyumbani kwa Jongo zikiwa kwenye mfuko maarufu kama ‘shangazi kaja.’

Inadaiwa baada ya kupata taarifa, polisi walikwenda nyumbani kwa Jongo ambaye alikataa kufungua mlango, ndipo askari mmoja alikwenda kugonga dirishani na kujitambulisha akimweleza wanataka kufanya upekuzi.

"Jongo alikubali, akafungua mlango na kuruhusu askari kufanya upekuzi, ambako walikuta kadi tatu za benki, kitambulisho cha Taifa, kadi za gari, hati ya kusafiria na magari mawili Toyota IST na Toyota RAV4, vitabu vitatu vya hundi, simu nne za mkononi na begi moja," amedai Kimaro.

Amedai baada ya upekuzi, Jongo alikamatwa na kupelekwa kituo cha Polisi Tazara kuhojiwa.

Inadaiwa Septemba 8, 2020, Jongo aliwaambia polisi kuna dawa zipo Temeke, eneo la Vetenari, nyumbani kwa mpenzi wake, Tatu Nassoro.

Wakili huyo amedai polisi walikwenda kufanya upekuzi nyumbani kwa Tatu wakishirikina na mjumbe wa nyumba 10, shina namba nane eneo la Vetenari, Temeke.

Wakili Mbilingi amedai wakiwa hapo, Jongo alimuomba Tatu ufunguo wa kabati la nguo akatoa begi kubwa na kulifungua.

Amedai askari walianza upekuzi katika nyumba hiyo saa 9.20 alasiri na kumaliza saa 11.40 jioni.

Inadaiwa Jongo alieleza kuwa na uhusiano na Tatu kwa miaka minne, lakini hakumweleza kuwa anajihusisha na biashara ya dawa za kulevya kwa sababu Semagoya alimwambia biashara hiyo inahitaji usiri wa hali ya juu.

Katika kabati inadaiwa ilikutwa mifuko minane yenye heroin ikiwa na uzito tofauti, wa kwanza ukiwa na kitambaa cha bluu ukiwa na pakiti 10 zenye uzito wa kilo 10.7.

Mfuko wa pili wa sulphate ulikuwa na kilo 14 za heroin, ukiwa pamoja na mwingine wa buluu uliokuwa na pakiti 11 zenye uzito wa kilo 8.89. Wa tatu unadaiwa kuwa mweusi uliokuwa na pakiti sita zenye uzito wa kilo sita za heroin, mfuko wa nne ulikuwa wa rangi ya kahawia uliokuwa na pakiti moja yenye uzito wa kilo moja.

Inadaiwa wa tano ulikuwa mwekundu ukiwa na pakiti moja yenye uzito wa kilo moja; wa sita ulikuwa na rangi ya kaki, ukiwa na pakiti moja yenye uzito wa gramu 890. Mfuko wa saba unadaiwa kuwa wa zambarau ukiwa na pakiti moja yenye pipi 67 zenye unga unaodaiwa kuwa heroin yenye uzito wa gramu 961.

Mfuko wa nane, unadaiwa kuwa mweusi ukiwa na pakiti nane zenye uzito wa kilo nane.

Inadaiwa kabatini pia kulikutwa kifurushi chenye unga wenye uzito wa kilo moja, kilichofungwa kwenye mfuko wa nailoni angavu.


Amedai kabatini pia kulikutwa fedha tasilimu Sh58 milioni zikiwa kwenye mfuko wa kitambaa cheusi.  Wakili huyo alidai baada ya upekuzi ilijazwa fomu ya ukamataji na kisha Jongo na Tatu walipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kwa mahojiano.

Inadaiwa dawa na fedha viliwekwa kwenye maboksi makubwa mawili na kufungwa. Baadaye yalikabidhiwa Polisi na kupelekwa kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamba na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa hatua zaidi.


Walivyoanza biashara

Inadaiwa na upande wa mashtaka katika mahojiano, Jongo alidai alianza biashara ya dawa za kulevya baada ya kushawishiwa na Semagoya.

Inadaiwa Jongo alieleza walijuana na Semagoya mwaka 2016 baada ya Semagoya kubadili dini na kuwa Muislamu, akapewa jina la Mulik na walikuwa wakifanya mazungumzo ya biashara baada ya kutoka ibada katika msikiti wa Nuru, uliopo Mbezi Beach.

Inadaiwa maongezi pia yalifanyika kwenye mgahawa na alipatiwa kilo 20 za dawa hizo ambazo alizipeleka Temeke Vetenari,  Mtaa wa Sandali.

Upande wa mashtaka unadai Jongo alikiri kumjua Amin kupitia Semagoya.


Jinsi walivyokamatwa

Inadaiwa jioni ya Septemba 5, 2020, Mkaguzi wa Polisi, Hassan Masawika alipata taarifa kutoka kwa msiri kuwa kuna mtu anajihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya, eneo la Mbezi Beach, ambaye kila alfajiri husambaza kwa washirika wake.

Inadaiwa Septemba 6, 2020 saa 11 alfajiri, Masawika akiongozana na mweyekiti wa Serikali ya mtaa wa Mbezi Beach A na askari kutoka DCEA walikwenda kwenye nyumba ya Ernest Semagoya iliyopo Mbezi Beach na kugonga mlango.

Inadaiwa Semagoya alikwenda getini, ndipo Masawika na mwenyekiti wa Serikali ya mtaa walipojitambulisha na kumtaka afungue mlango kwa ajili ya kufanya upekuzi.

Semagoya inadaiwa alikataa kufungua mlango akidai anakwenda kuvaa kwa kuwa alikuwa amevaa kanzu tu.

Baada ya dakika 40 kupita, alifungua mlango na kuruhusu upekuzi kufanyika na ilikutwa simu moja ya mkononi aina ya Iphone na Sh1 milioni, fedha za Msumbiji 7,370 na Sh400 za Kenya.

Inadaiwa upekuzi ukiendelea kwenye simu ya mshtakiwa waliona picha za pakiti za dawa za kulevya zilizoonekana kupigwa Septemba mosi, 2020.

Upande wa mashtaka unadai alipohojiwa alidai alipiga picha dawa hizo kutoka kwa Wasomali na ni kumbukumbu yake. Pia inadaiwa alieleza dawa hizo aliziuza nchini Kenya kwa mtu aitwaye Babaa.

Inadaiwa juhudi za kumtafuta Babaa zilishindikana kwa madai kuwa Semagoya hakuwa na mawasiliano naye, badala yake alidai kuna dawa zipo kwa Sekibo.

Inadaiwa nyumbani kwa Amin walimkuta mkewe na baada ya upekuzi zilipatikana Sh3.5 milioni.

Sekibo inadaiwa aliendelea kutafutwa baada ya taarifa kupatikana kuwa alijificha na ilipofika saa tano usiku, alikamatwa na kupelekwa kituo cha Polisi Tazara.

Akiwa kituoni inadaiwa alikiri kufanya biashara, akieleza Jongo alimpelekea mfuko wa shangazi kaja ukiwa na dawa za kulevya.

Inadaiwa kwa maelezo ya Sekibo, askari walikwenda nyumbani kwa Jongo, Mbezi Beach A kufanya upekuzi.

Hakimu Milanzi baada ya kusikiliza maelezo hayo, alisema kwa mamlaka aliyonayo ameihamishia kesi hiyo Mahakama Kuu kwa ajili ya kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka.

Amesema washtakiwa wataendelea kubaki rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.