Kuchelewa kwa makarani kwawakatisha tamaa wananchi
Muktasari:
Kuchelewa kwa makarani wa sensa kwa katika baadhi ya maeneo ya manispaa ya Morogoro, kumewafanya baadhi ya wananchi kuondoka nyumbani na kuendelea na shughuli zao.
Morogoro. Baadhi ya wananchi wa mitaa ya kata ya Lukobe mjini hapa wameamua kutoka kwenye nyumba zao na kwenda kuendelea na shughuli zao baada ya kuona kuwa makarani wa sensa hawajafika hadi kufikia saa sita mchana.
Akizungumza na Mwananchi leo Agosti 23, mmoja wa wananchi hao Hemed Mustafa Suleiman amesema kuwa tangu asubuhi amekaa nyumbani kwake akisubiri makarani wa sensa ili aweze kuheshabiwa lakini makarani hawakutokea.
"Changamoto ninayoiona ni kutokuwepo kwa uhakika wa kufika kwa makarani leo hii, mimi ni fundi mjenzi kutoka kwangu ndio kupata riziki.
“Sasa nimekaa tu hapa nyumbani nasubiri hao makarani ambao sijui wanakuja muda gani, hii inanikatisha tamaa hata kesho sina uhakika kama watakuja ama hawatakuja," alisema Selemani.
Kwa upande wake balozi wa mtaa wa Tushikamane kata ya Lukobe, Fatuma Kivulale amewataka wananchi wa mtaa huo kuacha namba zao za simu kwa watoto wao, majirani ama kwake ili makarani hao watakapofika mtaani hapo aweze kuwajulisha warudi kutoa taarifa zao na kuhesabiwa.
"Hapa mtaani wengi ni wafanyabiashara wa kwenye masoko, mafundi ujenzi na wengine wanafanya shughuli zao binafsi sasa walitegemea makarani wangefika mapema, lakini kuchelewa kwa makarani kumewafanya washindwe kusubiri.”