Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kuhamishwa daladala kivukoni, bajaji wachekelea

Dar es Salaam. Wakati madereva wa daladala wakilia kuhamishwa kituo cha daladala Kivukoni na kupangiwa vituo vingine mbadala, waendesha bajaji wameshangalia wakisema hiyo kwao ni sikukuu.

Jana Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) ilitangaza kuwa Oktoba 20 ndio itakuwa mwisho wa matumizi ya kituo hicho kwa daladala zote zinazokomea safari zake hapo, ili kupisha ujenzi wa kukifanyia upanuzi kituo hicho, ikiwa ni awamu ya tatu ya ujenzi wa miundombinu yatakapopita mabasi hayo.

Maeneo mbadala ambako watahamishiwa ni Mtaa wa Ohio, Posta ya zamani na pembezoni mwa ukuta wa Wizara ya Ardhi.

Wakizungumza leo Jumatano Oktoba 10, 2023 kwa nyakati tofauti na Mwananchi Digital, kuhusu maamuzi hayo, baadhi ya waendesha bajaji akiwemo Jasmini Milanzi, amesema kuwepo kwa daladala nyingi katika kituo hicho ilikuwa kwao ni kilio.

Jasmini alifafanua kuwa daladala hizo zimekuwa kero kwao kwa kuwa wao ni watu wenye ulemavu, hivyo hawawezi kutoka kwenda kuita abiria mpaka wawafuate walipo.

“Hii ni tofauti na wenzetu daladala, konda anashuka na kuitia abiria hadi katika geti wanapotokea wakiwa wameshuka kwenye pantoni, hivyo tunatamani waondoke hapa hata kesho kwani ni neema kwetu hii,” amesema Jasmini.

Mwendesha bajaji ambaye ni mlemavu, Rehema Rwegeshora, amesema kabla ya daladala kwenda eneo hilo, walikuwa walau hawakosi kuondoka na Sh50,000 lakini kwa sasa kupata hata Sh20,000 ni kazi, na kwamba baadhi yao wameamua kurudi barabarani kuomba.

Saleh Awadhi ambaye ni mzee wa waendesha bajaji walemavu amesema pamoja na maamuzi hayo mazuri ya kuwaacha hapo, wanaomba wakati upanuzi  huo  wa kituo cha Dart ukifanyika, wafikirie pia kuweka eneo kwa ajili ya bajaji kwa kuwa ni eneo ambalo walemavu wengi wanalitegemea kuendesha maisha yao.

Kwa upande wao bodoboda akiwemo Mrisho Rafael, amesema hilo kwao halina shida kwa kuwa sio bajaji wala daladala zilizowahi kuathiri biashara yao.

Hamis Mkumba, amesema kwa kuwa wote wanatafuta riziki hawaoni kwa nini wafurahie wenzao kuondoka isipokuwa wanawaonea zaidi huruma abiria ambao watapata tabu kuzifuata mbali zilipo daladala.

Madereva walia

Katibu wa madereva wa Kivukoni (Kibatike), Zuberi Juma amesema hawajashirikishwa katika maamuzi hayo na kushangaa tu jana wanayasikia hayo kwenye vyombo vya habari.

Hata hivyo, Juma amesema maeneo mbadala wanapopelekwa sio rafiki kwao wala kwa abiria, kwani hayana choo na kuhoji watu wakishikwa na haja watapata wapi huduma hiyo.

Wakati waendesha bajaji wakiwa wanachekelea, kwa upande wao madereva wa daladala akiwemo Mohammed Swai, amesema kilichofanywa sio sawa kwa kuwa eneo wanalopelekwa ni dogo hivyo itawawia ugumu katika kugeuza magari yao.

“Maeneo yote ukiangalia yaliyotengwa nafasi yake ni ndogo, sisi magari yetu ni makubwa, tutageuzaje wakati wa kutaka kutoka,”amesema Swai.

Yahaya Issa, amesema anasiitika maamuzi hayo yanatolewa wakati ndio kwanza wana mwezi tangu Latra ianzishe ruti ya Chang’ombe – Kivukoni na kueleza kuwa kwa nini Latra walizitoa wakati walijua kunakuja kufanyika ujenzi.

Rajabu Kitogo, amependekeza kuwa ni vema wangeachwa kuegesha magari yao pembezoni mwa uzio wa ujenzi, kwa kuwa hata zamani wakati kituo hicho kilipokuwa kinajengwa walikuwa wanafanya kazi kwa mtindo huo.


Halamashauri ya Jiji yatia neno

Mwananchi Digital ilimtafuta Mkurugenzi wa Halmashauri ya  Jiji la Dar es Salaam, Jomaary Mrisho, ambao ndio unamiliki maeneo vituo vilipopangwa, amesema malalamiko yaliyotolewa na madereva wataangalia namna gani wataweza kuyafanyia kazi ikiwemo suala la vyoo na ufinyu wa eneo.

“Hatuwezi kutarajia changamoto kabla hatujaingia na kuziona, kadri watakapokuwa wakifanya shughuli zao na tukazigundua, tutazifanyia kazi kwa haraka sana.

“Kwa kuwa hawa kwetu ni wadau muhimu sio tu kwenye usafiri bali kwa uchumi wa Halmashauri ya Jiji la Ilala na nchi kwa ujumla,” amesema Mkurugenzi huyo.