Kumbe Mkama siyo ‘Wakili,’ TLS yamkana

Muktasari:

  • Mkama anadaiwa kusababisha taharuki hiyo Jumanne Mei 23, 2023 katika mahakama hiyo kwa kile kinachodaiwa kuwazuia Polisi wasiwakamate upya  washtakiwa aliokuwa anawatetea mahakamani hapo ambao walifutiwa kesi yao, hali iliyosababisha kukamatwa kwake.

Dar es Salaam. Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kimejitenga na ‘Wakili’ Baraka Mkama anayedaiwa kusababisha vurugu katika lango kuu la kuingilia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kikisem sio wakili na wala sio mwanachama wa chama hicho cha kitaaluma.

Mkama anadaiwa kusababisha taharuki hiyo Jumanne Mei 23, 2023 katika mahakama hiyo kwa kile kinachodaiwa kuwazuia Polisi wasiwakamate upya  washtakiwa aliokuwa anawatetea mahakamani hapo ambao walifutiwa kesi yao, hali iliyosababisha kukamatwa kwake.

Hata hivyo baada ya taarifa hiyo kuruka katika vyombo vya habari ikiwemo gazeti la Mwananchi na mitandao yake ya kijamii, taarifa ziliibuka kuwa Mkama sio Wakili na hata namba ya uwakili aliyoitaja wakati anahojiwa na TLS haikuwa yake bali ya Wakili mwingine na ndipo Baraza la TLS lilipounda timu kuchunguza sakata hilo.

Taarifa iliyotolewa leo  Julai 27, 2023 na kusainiwa na Raisi wa TLS, Harold  Sungusia imeeleza baada ya TLS kupokea taarifa ya uchunguzi uliofanywa na timu uliyounda imejiridhisha pasina shaka kuwa Mukama sio wakili wala mwanachama wa TLS na hata katika mfumo wa usajili wa mawakili (e-wakili) hayupo.

Mei 24, 2023 TLS iliunda timu ya mawakili watano kuchunguza sakata la ‘Wakili’ Mkama anayedaiwa kusababisha vurugu katika eneo hilo la Mahakama.

Walioteuliwa kufanya uchunguzi katika sakata hilo ni Mawakili Magreth Mwihava (Mwenyekiti), Hekima Mwasipu (mjumbe) Emanuel Augustine (mjumbe) na Anastazia Muro ambaye ni Katibu wa timu.

Timu hiyo pamoja na mambo mengine ilifanya uchungu wa kina kwa kumfanyia mahojiano Mkama mwenyewe, Uongozi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jeshi la Polisi, Ofisa wa Polisi aliyehusika katika sakata hilo, na baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, ili kujua sababu za vurugu hizo na kuangalia katika mfumo wa e-wakili.

Hata hivyo, Ijumaa Mei 26, 2023 timu hiyo iliyongozwa na Mwenyekiti wa TLS Tawi la Ilala, Margreth ilikabidhi ripoti ya uchuguzi kwa Baraza la TLS kwa ajili ya uamuzi.

Taarifa hiyo inasema katika mahojiano yaliyofaywa baina ya Mkama na timu hiyo, alikiri kuwa yeye sio wakili ingawa amekuwa akifanya kazi kama wakili tangu mwaka 2019.

Pia katika mashauri aliyokuwa anayasimamia akiigiza kama wakili, alikuwa akiwatoza wateja wake kiasi cha Sh3 milioni na kuendelea kwa kesi na kwamba katika mfumo wa usajili wa Mawakili (e-Wakili) ilibainika kuwa Mukama sio mwanchama wa TLS.

“Kwa sababu hiyo, TLS itashirikiana na vyombo vya dola na vyombo vya utoaji haki ili kuhakikisha kuwa hatua stahiki za kisheria zinachukuliwa dhidi ya muhusika, pamoja na watu wengine kama yeye ili kukomesha tabia hii ambayo inaelekea kuenea maeneo mengi nchini,” imesema taarifa hiyo na kuongeza;

“Katika kufuatilia tukio hili, TLS imepata taarifa muhimu za ziada kuhusu mtandao wa watu wasiokuwa Mawakili wanaofanya kazi za uwakili (vishoka) hivyo imeiongezea muda Kamati teule ya uchunguzi kuendelea kufuatilia mtandao huo na kuwasilisha taarifa zake za ziada ifikapo Mei 31, 2023.”

Kwa upande mwingine, TLS imeunda kikosi kazi (Anti-Vishoka Taskforce) kitakachofanya kazi ya kudhibiti watu ambao hawastahili kufanya kazi za mawakili.

Kwa mantiki hiyo, Baraza la Uongozi la TLS linaomba ushirikiano toka kwa wanachama wake na wadau wengine pamoja na wananchi ili kwa pamoja waweze kukomesha uharifu huo.

Sakata la Mkama:

Itakumbukwa kuwa sakata la Mkama lilitolea Mei 23, 2023 katika Mahakama hiyo, baada ya washtakiwa Khalid Somoe (54), Raphael Lyimo (40), Betty Mwakikusye (41), Abdiel Mshana (57), kufutiwa kesi ya jinai namba 99/2019.


Kesi hiyo ilifutwa na Hakimu Mkazi Mkuu Romuli Mbuya, baada ya Wakili wa utetezi, Agatha Fabian na Baraka Mkama kuwasilisha maombi ya kuifuta kesi hiyo kutokana na kutoendelea kwa muda mrefu.

Hata hivyo muda mfupi baada ya Mahakama kuwafutia kesi, askari polisi waliokuwa wakilinda usalama katika mahakamani hapo, waliwakamata washtakiwa hao na katika harakati hizo, alijitokeza Mkama na kuanza kuzuia wateja wake wasikamatwe.

Hali hiyo ilizua taharuki ambayo ilisababisha akamatwe na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi na kisha kupelekwa kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya uchunguzi.