Kumbe Nimrod Mkono alikuwa mwinjilisti
Mbunge wa zamani wa Musoma Vijijini, Wakili Nimrod Mkono enzi za uhai wake.
Muktasari:
Kwa mujibu wa Shadrack, marehemu Mkono alikuwa Mwinjilisti wa kusambaza neno la Mungu kwa njia ya biashara ya vitabu huku akiwekeza rasimali zake kusaidia vijana wengi kupata elimu.
Dar es Salaam. Japo wengi wanamjua Nimrod Mkono kama Mwanasiasa (Mbunge mstaafu), Wakili na Mfanyabiashara aliyetumia fedha zake kwa maendeleo ya watu wake, kisichojulikana ni kumba aliwahi pia kuwa Mtumishi wa Mungu akihudumu kama Mwinjilisti.
Akizungumza baada ya mapokezi ya mwili wa Mkono jijini hapa, mdogo wa marehemu Shadrack Mkono amesema matendo ya kaka yake akiwa bado angali hai, ni ushahidi tosha kuwa alimpenda Mungu na aliwapenda watu pia.
Kwa mujibu wa Shadrack, marehemu Mkono alikuwa Mwinjilisti wa kusambaza neno la Mungu kwa njia ya biashara ya vitabu huku akiwekeza rasimali zake kusaidia vijana wengi kupata elimu.
“Nikiwa bado mdogo nasoma chuo kikuu, nilikuwa namshuhudia akiuza vitabu vya Injili, pesa aliyoipata aliitumia kwenda shule,” amesema Shadrack leo Mei 27, 2023 nyumbani kwa marehemu Masaki jijini Dar es Salaam.
Mbunge huyo wa zamani wa Musoma Vijijini kuanzia 2000 hadi 2015 na baadaye jimbo la Butiama mwaka 2015 hadi 2020 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), alifariki dunia Aprili 18,2023 jijini Florida nchini Marekani alikokuwa akitibiwa tangu mwaka 2018.
Taarifa zinasema kuwa Mkono alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu (Alzheimer) kwa muda mrefu, hali iliyomsababishia kuacha shughuli za ubunge na uwakili ili kwenda kupambania afya yake kwa miaka mine.
Mwili wake umewasili leo alfajiri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam (JNIA) kabla ya kuanza ratiba za ibada nyumbani kwake Masaki.
Akifafanua namna alivyopenda binadamu, Shadrack ametoa mfano wa wazazi wengi waliopata msaada wa kuendeleza watoto wao kielimu baada ya kukwama kiuchumi.
“Walikuwa wanakwenda nyumbani kuomba na aliwapokea, akawasaidia kuendelea kidato cha tano na sita, ni wengi siwakumbuki na walihamia nyumbani wengine kwa hiyo alipenda binadamu kwa dhati ili wawe na maisha mazuri.”
Wadau wa siasa wanamtaja kama mwana maendeleo na kwamba amejenga shule nyingi jimboni kwake zikiwemo, Chifu Ihunyo, Chifu Wanzangi, Chifu Osward Mang’ombe, Shule za Sekondari za Butuguri na Kasoma lakini pia Shule ya Msingi Busegwe, nyingine nyingi. Lakini pia alitoa mchango mkubwa kufanikisha kupatikana kwa wilaya ya Butiama.
Ratiba ya maziko inaonyesha kuwa mwili wa Wakili huyo maarufu, unatarajiwa kuzikwa Mei 29, mwaka huu katika Kijiji cha Kigori, Kata ya Busegwe wilayan Buatiama, Mkoa wa Mara.
Hata hivyo, kabla ya maziko hayo, kesho Mei 28, mwaka huu waombolezaji watapata fursa ya kutoa heshima za mwisho kwa Mbunge huyu wa zamani katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Baadaye, mwili huo utasafirishwa kwa njia ya anga kupitia JNIA kuelekea Mwanza na baadaye safari kwa njia ya barabara kuelekea wilayani Butiama, Mkoa wa Mara yaliko makazi yake ya asili, itafuata.