Kunenge ataka watoto Pwani kusoma elimu zote

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge akiwa na Viongozi wa Wilaya ya Mkuranga kukagua na kuangalia utekelezaji wa miradi ambayo Serikali imepeleka fedha za kutatua kero na kuboresha maisha ya jamiii, ikiwemo miradi ya ujenzi wa shule mpya za Sekondari za mradi wa SEQUIP.

Muktasari:

  • Akizungumza wanafunzi wasichana ambao wanasoma kidato cha kwanza katika sekondari mpya za Kilimahewa, Samia Suluhu Hassan ambazo zimejengwa kupitia mradi Sequip, ameonyesha kufurahishwa na idadi kubwa ya wasichana katika shule hizo.

Mkuranga. Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amewataka wazazi na walezi kuwaacha watoto wao wapate elimu zote na sio ya madrasa pekee kwani zote hizo zina umuhimu kwa kizazi cha sasa.

Kunege ameyasme hayo leo Jumatano Novemba 8, 2023; katika ziara yake wilayani Mkuranga, ikiwa na lengo la kuangalia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Sekondari ya Kilimahewa, kata Kata ya Kilimahewa wilayani humo.

Shule hiyo inadaiwa kuwa mkombozi kwa zaidi ya wanafunzi 150 katika kata hiyo ambao awali walilazimika kutembea zaidi ya kilomita 10 kufuata elimu katika kata jirani.

Hivyo basi, RC Kunenge amesema: “...watu wanadhani kwamba watoto wakisoma elimu ya madrasa hawawezi tena kusoma elimu ingine jambo ambalo sio sahihi kabisa, ni lazima wazazi wawahamasishe watoto wakiwemo wa kike wasome elimu zote.”

Akizungumza wanafunzi wasichana ambao wanasoma kidato cha kwanza katika sekondari mpya za Kilimahewa, Samia Suluhu Hassan ambazo zimejengwa kupitia mradi Sequip, ameonyesha kufurahishwa na idadi kubwa ya wasichana katika shule hizo.

"Nimefarijika sana kuona idadi kubwa ya watoto wanaosoma katika shule nyingi ambazo ni mpya, ni wa kike ambapo kwa Sekondari ya Kilimahewa pekee, wapo wasichana 79  kati ya wanafunzi 140 shuleni hapo, huku kwa Sekondari ya  Samia Suluhu Hassan, wasicha ni  24 kati ya wanafunzi wote 45.

"...ukiangalia Mkuu wa Wilaya Khadija Nasir ni mwanamke kama nyie ana digrii zaidi ya moja, kwa hiyo na ninyi msome mna hii shule ya Kilimahewa nzuri tunatarajia tuone matokeo mazuri angalieni Rais Samia...amesoma tena anajua uchumi vizuri anajua takwimu vizuri mambo yote amesoma anajua."

Katika taarifa ya Mkuu wa Shule ya Kilimahewa, Rabii Athumani amesema ujenzi wa shule hiyo umegharimu Sh528 milioni na kwamba imekamilika kwa asilimia 98, huku ikiwa na maabara za masomo ya sayansi, pamoja na maktaba mbili.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Khadija Nasir amesema shule hizo zote mwaka huu zimeanza na kidato cha kwanza.

Baadhi ya wanafunzi Fatma Nasib na Bakat  Kilindo wamesema wanatarajia kufaulu masomo na kushiriki pia shughuli za nyumbani.