Kungwi afariki dunia kwenye ajali akisubiriwa kumfunda bibi harusi
Muktasari:
- Kungwi huyo alikuwa akisubiriwa kwenye shughuli ya kumfunda bibi harusi. Shughuli hiyo iliahirishwa, hata hivyo inafanyika leo Desemba 12, 2024 ambapo msichana huyo ataangwa rasmi kesho Desemba 13, 2024.
Tanga. Mkazi wa Kata ya Vibaoni iliyopo katika Halmashauri ya Mji Handeni, ambaye ni kungwi wa kufunda wasichana wanaokwenda kuolewa, Mwanahamisi Mbelwa (40) amefariki dunia pamoja na mwingine mmoja kwenye ajali iliyohusisha lori la mafuta na bodaboda ambayo alipanda.
Dereva huyo wa bodaboda naye alifariki hapo hapo na abiria wake huku abiria mwingine akijeruhiwa katika ajali hiyo iliyotokea jana Desemba 11, 2024 eneo la Kwediyamba, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa pikipiki kujaribu kulipita lori na kuteleza hadi kuingia uvunguni mwa lori na kusababisha vifo hivyo.
“Walipakiana watatu, wenyewe wanaita mishikaki, alipojaribu kupita gari kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kuwepo utelezi, akateleza na kuingia chini ya hilo lori ambapo watu wawili wamefariki na mmoja kujeruhiwa na kupelekwa Hospitali ya Mji wa Handeni,” amesema Kamanda Mchunguzi.
Akielezea namna ajali hiyo ilivyotokea, mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Habiba Amiri amesema walimuita kungwi huyo kwa ajili ya shughuli ya kumweka msichana wao ndani, ambapo yeye na dada yake wanafanya shughuli hizo kwa muda mrefu.
Amesema wakati wanafika eneo la tukio, dereva wa lori alionekana kumuonya dereva wa bodaboda asimpite kutokana na ubovu wa barabara kwa kuwa ni hatari na ndipo alipoteleza na kuingia kwenye tairi la lori hilo.
Licha ya dereva wa lori kutoa tahadhari, mwenzake alipenya pembeni ya barabara na kwa bahati mbaya alidondoka na abiria wake wote wawili na tairi za nyuma za lori ziliwakanyaga kichwani.
“Tulikuwa na shughuli ya watoto, wakati tunakusanyika, kuna lori la mafuta lilikuwa linatoka mjini likiwa na mwendo wa polepole, wala lilikuwa halikimbii, ile pikipiki ilipandisha kina dada wawili, ilipofika hapa ikiwa inalipita lile lori, dereva akampa ishara bodaboda asipite kutokana na sehemu hiyo ni mbaya, lakini akapita, ndipo wakapata ajali,” amesema Habiba.
Ameeleza kuwa baada ya ajali, dereva wa pikipiki na abiria wake walirushwa barabarani na kuingia uvunguni mwa lori kwenye tairi za nyuma na kuwakanyaga na watu wawili walifia hapo hapo na mmoja akijeruhiwa.
Hata hivyo, Rajabu Tumbotumbo ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya harusi ambayo marehemu alitakiwa kwenda, amesema baada ya shughuli ya kumweka mtoto ndani, nusu saa kabla ya ajali, aliongea na Mwanahamisi kuhusu kuwahi kwenye harusi ya mdogo wake.
“Hawa wanafunda mwali, kuna ngoma ya Kizigua inaitwa Machindi, ndio huchezwa wakati wa kuwafunda, kwa hiyo asubuhi nimewasiliana nao wakasema wanakwenda Kwediyamba kuchukua ngoma, wakati wanarudi, sasa tukiwa tunawasubiri nyumbani kwa ajili ya kumfunda bibi harusi wetu, ndio tunasikia tukio la ajali na kuambiwa wapo waliofariki,” amesema Rajabu.
Rajabu ameongeza kuwa ilibidi kuahirishwa kwa shughuli ya kumfunda bibi harusi wao kutokana na ajali hiyo ambapo leo Desemba 12, 2024, watamuaga ukumbini baada ya kutokea ajali iliyosababisha kifo cha kungwi wao.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji Handeni, Stephen Julius amesema amepokea miili ya marehemu wawili ambao ni Ali Ramadhani (20) ambaye alikuwa ni dereva wa pikipiki hiyo na Mwanahamisi Mbelwa (40) ambao walipokelewa wakiwa wamefariki.
Amesema majeruhi mmoja ambaye ni mmoja wa wafundaji, amejeruhiwa kwenye maeneo ya masikio na michubuko kwenye sehemu nyingine za mwili, lakini anaendelea vizuri baada ya kupata matibabu.
Marehemu Mwanahamisi amezikwa wilayani Handeni, huku dereva aliyekuwa akiendesha bodaboda hiyo akitarajiwa kuzikwa mchana wa leo Desemba 12, 2024 maeneo ya Mtaa wa Barabara Moto huko Handeni.