Kwa kila kilo 470 za malisho unalipwa Sh49, 000

Muktasari:

  • Taasisi ya Land O'Lakes Venture37 imeanzisha mfuko wa kuwalipa wazalishaji wa malisho kama sehemu ya motishha kwa lengo la kuongeza uhakika wa chakula cha mifugo hatua ambayo itapunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Dar es Salaam. Katika jitihada za kupunguza migororo kati ya wakulima na wafugaji leo umeanzishwa mfuko mpya wa motisha kwa ajili ya kuongeza malisho ya mifugo nchini.
Tanzania inatajwa kuwa na idadi ya mifugo milioni 69.6. Migogoro kati ya wakulima na wafugaji imekuwa ni jambo la kawaida, kumbukumbu mbaya zaidi ni tukio la Desemba 2000, kilosa mkoani Morogoro ambapo watu 38 waliuawa.
Mbali na kuepusha migogoro hiyo kuanzishwa kwa mfuko huo pia kutasaidia kukuza biashara kwa wafugaji kwa kuongeza tija katika uzalishaji wa maziwa na ubora wa nyama.
Akizungumza katika uzinduzi wa mfuko huo, leo Januari 24 jijini hapa, Mkurugenzi msaidizi wa Ardhi ya Malisho katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi Gabriel Bura, amesema mfuko huo umeanzishwa kupitia mpango wa kimataifa uitwao AgriResults ambao hutumia mashindano ya zawadi za Lipa-kwa-Matokeo kuhamasisha, au "kuvuta", sekta binafsi kuondokana na vikwazo vya soko la kilimo.
Amesema kwa Tanzania zimetengwa Dola za Kimarekani 223,000 (Sh520 milioni) kwa kipindi cha mwaka mmoja na kwa kila kilo 470 za malisho ambazo mzalishaji atazalisha atapata motisha ya dola 21 (Sh49, 000).
Takwimu zilizopo za malisho zinaonyesha kuwa uwezo wa nchi ni kuzalisha tani milioni 7.97 za malisho yasi asili na marobota) na dhidi ya mahitaji ya tani milioni 146.98.
Bura amesema kutokana na takwimu hizo nchi inakabiliwa na uhaba wa tani milioni 139.01 za malisho hivi sasa mkazo umeelekezwa kwenye marobota ya nyasi, mikunde au mimea mingine ambayo inaweza kukaushwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya malisho.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi, katika mwaka wa fedha wa 2021/22 nchi ilizalisha marobota 274,095 pekee ya malisho yenye thamani ya Sh1.1 bilioni. Taasisi za serikali zilizalisha marobota 156,018 yenye thamani ya Sh624.1 milioni, huku sekta ya kibinafsi ikizalisha marobota 118,077 yenye thamani ya Sh472.3 milioni.
“Tatizo kubwa ni mitazamo ya wafugaji wanaoamini katika nyasi asilia na sio marobota. Sasa tunatumia mbinu ya shule ya shambani ili kushughulikia tatizo hilo,” amesema Bura.
Ameongeza kuwa “Si jambo la mara moja kubadili mitazamo yao. Inaweza kuchukua miaka mitano hadi 10. Sisi (serikali) tunahitaji kushikamana na sekta binafsi ili kuharakisha mchakato huo.”
Kiongozi wa timu ya AgResults, Neema Mrema alisema ili mtu aweze kupata motisha anaweza kuzalisha na kuuza tani 100 za malisho.
Amesema lengo ni kuhakikisha ng’ombe wasiopungua 10,000 katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga na Morogoro wanapata lishe bora.
“Tunalenga tani 5,000 za malisho katika kipindi cha mwaka mmoja cha motisha ya malisho. Tunawatafutia (wazalishaji) kumiliki na kuendeleza ardhi ili kusiwe na migogoro kati ya wafugaji na wakulima,” alisema Bi Mrema wakati wa uzinduzi wa mfuko huo leo Januari 24.
Kadhalika amesema mradi huo unaoendeshwa na Land O'Lakes Venture37, unalenga kuimarisha uwezo wa wafugaji wadogo ili kuongeza tija ya maziwa ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya maziwa na bidhaa za maziwa.
Amesema kutokana na mradi huo lita milioni 23 za maziwa zilitarajiwa kuzalishwa ambazo zinaweza kuwafanya wakulima kupata mapato ya Sh9.4 milioni.