Kwa nini cheo cha Naibu waziri mkuu

Dar es Salaam. Mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri na Makatibu wakuu yaliyofanywa jana na Rais Samia kwa kumteua Dk Doto Biteko kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati yanamfanya kiongozi huyo kuingia kwenye historia ya kuwa Mtanzania wa tatu kushika wadhifa huo.

Dk Biteko, ambaye ni mbunge wa Bukombe, mkoani Geita atakuwa anashughulikia uratibu wa shughuli za Serikali.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, Ibara ya 52 inaainisha majukumu ya Waziri Mkuu, lakini haisemi chochote kuhusu cheo cha Naibu Waziri Mkuu wala majukumu yake.

Katiba inaeleza Waziri Mkuu atakuwa na madaraka juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa siku hata siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano na ndiye ambaye atakuwa kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni.

Hii ni mara ya tatu kwa Tanzania kufanya uteuzi wa Naibu Waziri Mkuu. Mwaka mmoja baada ya Rais Ali Hassan Mwinyi kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muhula wa kwanza wa miaka mitano Oktoba 1985, alimteua Salim Ahmed Salim kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Januari 24, 1993 Rais Mwinyi alimpandisha cheo aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Augustine Mrema, kuwa Naibu Waziri Mkuu huku akiendelea kushikilia cheo chake cha Waziri wa Mambo ya Ndani.

Wadhifa huo alipewa kutokana na mambo kadhaa aliyofanya, mojawapo likiwa ni kumaliza mgogoro wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Arumeru, uliokuwa umedumu kwa muda mrefu ambao ungeweza kuleta maafa.

Hata hivyo, Mrema hakudumu sana katika wizara hiyo. Novemba 1994 wafadhili wengi walitishia kuwa wangeondoa misaada yao huku Mwalimu Nyerere akiandika kitabu kuisema Serikali ya Mwinyi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Kristomus alisema upo uwezekano Rais ameamua kutengeneza cheo cha Naibu Waziri Mkuu na kumpa nafasi hiyo Biteko ili ajikite katika uratibu wa shughuli za Serikali kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Alisema kwa muda mrefu Rais Samia amekuwa akilalamikia taasisi za Serikali kutosomana, hivyo huenda uteuzi wa Biteko unalenga kuhakikisha anakwenda kuzisimamia taasisi hizo zinazohusika na utendaji wa shughuli za Serikali.

Alisema pia kuna uwezekano wa uteuzi huo wa Biteko kufanyika kwa sababu za kisiasa ili kwenda na upepo wa chaguzi zijazo, hasa kuangalia masilahi ya Kanda ya Ziwa ambako ni eneo la kimkakati inapofikia kwenye uchaguzi mkuu hapa Tanzania.

Mbunge wa Sengerema (CCM), Hamis Tabasamu alipongeza hatua ya kuanzishwa kwa cheo cha Naibu Waziri Mkuu, kwani kitawezesha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kupata usaidizi katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Doto Biteko ni mwadilifu wala Rais hajakosea katika jambo hilo. Haya ni mabadiliko makubwa sana katika nchi, tumuunge mkono Rais,” alisema.