Sababu nne Rais Samia kufanya mabadiliko Baraza la Mawaziri

Rais Samia Suluhu Hassan akitoa taarifa  ndogo ya mabadiliko ya nafasi za Uongozi katika Serikali,  Ikulu jijini Dar es Salaam Januari 3, 2023. Picha na Ikulu

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko katika wizara kwa kuteua watu wapya na kuwaacha wengine kulingana na mahitaji yake na mazingira ya sasa.

Sababu za msingi za mabadiliko ya Baraza la Mawaziri ni saba. Mosi, Rais mpya anapokula kiapo. Hiyo ni kwa mujibu wa Katiba, ibara ya 51 (3) (a) na 57 (2) (e na f). Pili, anapombadili Waziri Mkuu, anapaswa atangaze upya Baraza la Mawaziri, kutii sharti la Katiba, ibara ya 51 (3) na 57 (2).

Tatu, Rais anapofuta wizara, nne, anapounda wizara mpya. Sababu ya tano, Rais anapoondoa wenye utendaji usiomridhisha, sita, anapobadili majina ya wizara na sababu ya saba ni pale Rais anapotaka kuipa Serikali nguvu tofauti (government refresh).

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, amepata kusimulia kisa cha kumwita aliyekuwa Waziri Mkuu katika uongozi wake, Rashid Kawawa, akamwambia: "Hujafanya kosa lolote, ila nataka niweke mtu mwingine." Mwalimu Nyerere alimsifu Kawawa kuwa alielewa na akakubali bila kinyongo.

Mabadiliko hayo ambayo Mwalimu Nyerere aliyafanya, yalilenga kuipa Serikali nishati tofauti (nguvu mpya). Kawawa aliteuliwa kuwa Waziri Asiye na Wizara Maalumu, kiti cha Waziri Mkuu kikakaliwa na marehemu Edward Sokoine.


Mabadiliko ya Rais Samia

Uchambuzi wa maingizo mapya, muundo mpya wa wizara na utambulisho wa ofisi ya Naibu Waziri Mkuu, unatengeneza sababu nne za msingi.

Rais Samia anakuwa Rais wa pili kati ya sita, walioiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutambulisha cheo cha Naibu Waziri Mkuu. Kwa mara ya kwanza, Rais Ali Hassan Mwinyi alimteua Dk Salim Ahmed Salim kuwa Naibu Waziri Mkuu.

Kulikuwa na sababu, Mwinyi aliingia madarakani akimkuta Salim ni Waziri Mkuu. Wakati huo, nchi ilikuwa chini ya mfumo wa chama kimoja. Rais kutokea Zanzibar, sharti Waziri Mkuu atoke Bara. Mwinyi na Salim wote walikuwa Wazanzibari.

Joseph Warioba aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu, Salim akawa Naibu Waziri Mkuu, vilevile Waziri wa Ulinzi. Salim alikoma kuwa Naibu Waziri Mkuu Septemba 1989, alipochaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU), hivi sasa unaitwa Umoja wa Afrika (AU).

Augustine Mrema, Waziri wa Mambo ya Ndani mchapakazi, alimvutia Mwinyi, akamteua kuwa Naibu Waziri Mkuu. Hata hivyo, katika kitabu "Mzee Rukhsa" ambacho Mwinyi amesimulia maisha yake, ameeleza cheo hicho kilisababisha mgongano kwenye Baraza la Mawaziri, akakifuta.

Rais Samia amemteua Doto Biteko kuwa Naibu Waziri Mkuu. Hivyo, katika historia ya Tanzania, Doto anakuwa kiongozi wa tatu kushika wadhifa huo, baada ya Salim na Mrema. Pamoja na unaibu Waziri Mkuu, Biteko pia ni Waziri wa Nishati.

Uteuzi wa Doto upo kwenye matawi mawili, ama Rais anakoshwa na utendaji wa mbunge huyo wa Bukombe, hivyo kumpandisha ngazi au ameona Ofisi ya Waziri Mkuu ina majukumu mengi na inahitaji msaidizi na Doto ndiye mtu sahihi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, kwa kuwa Naibu Waziri Mkuu, Doto atakuwa anashughulikia uratibu wa shughuli za Serikali. Katiba, ibara ya 52 (1), inaeleza kuwa Waziri Mkuu ndiye mtendaji mkuu wa Serikali. Kwa maana hiyo, Doto atashughulikia uratibu wa shughuli za Serikali chini ya Waziri Mkuu.

Pamoja na kuanzishwa Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu, Rais Samia ameanzisha wizara mpya mbili, kwa kuivunja iliyokuwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Sasa kuna Wizara ya Uchukuzi chini ya Profesa Makame Mbarawa na Wizara ya Ujenzi, iliyokabidhiwa kwa Innocent Bashungwa.

Doto kuwa Naibu Waziri Mkuu, angeweza kumteua pasipo kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri. Hata hivyo, kuvunja wizara na kuunda mpya mbili, hizo ni sababu mbili za msingi za kufanya mabadiliko ya baraza, miongoni mwa sababu saba za msingi.

Sababu ya tatu ya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri ambayo ipo dhahiri ni kuimarishwa kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Sasa wizara hiyo imepewa Naibu Waziri wa Afrika Mashariki ambaye ni Stephen Byabato, aliyetokea Nishati.

Sababu ya nne ni kuipa Serikali nishati mpya. Wapya wameingia, Jerry Silaa, sasa ndiye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, amechukua nafasi ya Angeline Mabula, aliyeondolewa. Anthony Mavunde, amekuwa Waziri wa Madini, akichua nafasi ya Doto.

Kuna uhamisho, January Makamba, amekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akichukua nafasi ya Stergomena Tax, ambaye amekwenda Wizara ya Ulinzi. Kabla ya hapo, January alikuwa Nishati, wizara ambayo sasa ipo chini ya Doto.

Mohammed Mchengerwa, amekuwa Waziri wa Tamisemi, akitokea Maliasili na Utalii, alipompisha Angellah Kairuki. Kabla, Kairuki alikuwa Tamisemi. Dk Damas Ndumbaro kutoka Katiba na Sheria hadi Utamaduni, Sanaa na Michezo, akibadilishana ofisi na Dk Pindi Chana.