Kwa nini Maalim Seif alipendwa?

Kwa nini Maalim Seif alipendwa?

Muktasari:

  • Nimepata wakati mgumu kuandika hii makala juu ya Maalim Seif. Kwa hakika ni vigumu sana kujaribu kufupisha maisha ya Maalim Seif katika dakika chache, lakini kwa vile nimeulizwa na watu mbalimbali juu ya nilivyomfahamu na siasa zake, nami nimeamua niandike kidogo. Nilimfahamu Maalim Seif wakati alipokuwa kiongozi.

Ni takriban siku nane zimepita tangu kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar na nguli wa siasa nchini, Maalim Seif Hamad. Ni kipindi kigumu kwangu na kwa Watanzania.

Nimepata wakati mgumu kuandika hii makala juu ya Maalim Seif. Kwa hakika ni vigumu sana kujaribu kufupisha maisha ya Maalim Seif katika dakika chache, lakini kwa vile nimeulizwa na watu mbalimbali juu ya nilivyomfahamu na siasa zake, nami nimeamua niandike kidogo. Nilimfahamu Maalim Seif wakati alipokuwa kiongozi.

Wakati huo mimi ni mwanafunzi na kwa mtu yeyote kama mimi ambaye tangu nikiwa na umri mdogo nilipenda siasa. Wakati huo tulikuwa tunafahamu ndani ya chama kimoja wakati huo Chama cha Mapinduzi.

Wakati ule, Zanzibar kulikuwa na makundi mawili ya kisiasa, na Maalim Seif alikumbukwa sana mwaka 1984 alipokuwa Waziri Kiongozi wakati wa Ali Hassan Mwinyi aliposhika nafasi ile, watu wengi watakumbuka alitajwa zaidi katika siasa za wakati ule na alinasibishwa zaidi na mafanikio ya serikali ya awamu ya tatu kuliko hata Rais kwasababu ya uwezo na kipaji chake.

Nakumbuka katika majarida ya wakati ule “African Events”, kaka yetu Ahmed Rajab aliandika makala akimuelezea Maalim Seif kama kiongozi, alimpa sifa za kijana mwenye nguvu ya kutenda, mahiri na mwenye maono.

Kwahiyo alituvutia wengi wakati huo tupo kwenye maskuli na ulipokuja mvutano, yaani zilipokuja siasa mpya za awamu ya tatu, walikuwapo wapinzani ndani ya chama kimoja cha CCM, waliokuwa wakipingana na siasa zile za kimaendeleo wakitaka tubaki kule kule tulipotoka. Kwa hiyo, kukawa na makundi mawili ndani ya CCM maarufu yakaja kujulikana kama ‘Frontliners’ wakiongozwa na Maalim Seif, na ‘Liberators’ ambao ni tabu kusema nani kinara wake, lakini walikuwa wakijumuisha wakati ule kama aliyekuwa Waziri Kiongozi Ramadhan Haji Faki, Mzee Hassan Nassor Moyo, Abdallah Said Natepe, Ali Mzee Ali aliyekuwa katika baraza la mapinduzi wakati ule na wengine.

Kwa vijana nikiwamo mimi, tulivutiwa na hawa vijana waliokuwa wakiwakilishwa na Maalim Seif na baadaye kama tunavyojua Maalim Seif hatimaye hakudumu katika siasa za CCM kwasababu ya misimamo yake ile, aliondolewa katika nafasi yake na kufukuzwa uanachama. Baada ya mwaka mmoja tu alikamatwa akafunguliwa kesi za kubuni. Aliambiwa amefanya mkusanyiko usio halali na baadaye akaambiwa amekutwa na nyaraka za siri za serikali.

Kipindi kile alipokuwa gerezani, huku nje ndio kulivuma zaidi umaarufu wake na ndicho kipindi ambacho moja kwa moja mimi nilianza kujiunganisha naye nikiwa ni mwanafunzi wa Lumumba, kwasababu wengi tulikuwa tukimuita kuwa ni Mandela wa Zanzibar.

Kipindi kile Mandela alikuwa anatambulika kote duniani kuwa alikuwa anapigania haki na uhuru wa watu weusi waliokuwa wanakandamizwa Afrika Kusini na akipinga ubaguzi na ilikuwa ni fahari kwa Wazanzibari kumnasibisha Maalim Seif na harakati za Afrika Kusini.

Sote tulikuwa tukienda mahakamani na hatukuruhusiwa kulikaribia gari alilokuwa akiteremshwa lakini kwa mbali atatoa alama ya dole gumba kuashiria alama ya msimamo na tukiingia mahakamani kusikiliza kesi huku tukiisikia sauti yake akitoa salamu ndani ya ukumbi ikitikisa kuashiria kuwa huyu ni jabari wa siasa za upinzani dhidi ya CCM

Hivyo ndivyo nilivyoanza kumfahamu Maalim Seif. Lakini baadaye, alipotoka gerezani siku ya mwanzo kabisa nilikwenda kumuona nyumbani kwake Mtoni na ndio ikawa mwanzo ya safari ya kisiasa tuliyoifanya pamoja na alikuta tayari tumeanzisha harakati za “Kama Huru” ikiongozwa na marehemu Shaabani Khamis Mloo kama mwenyekiti wake, Hamed Seif Hamad kama Makamu Mwenyekiti na Mzee Ali Haji Pandu kama katibu wake na tukafanya naye harakati. Hakupata nafasi ndani ya chama lakini vilipoundwa vyama vingi ikaanzishwa CUF, Maalim Seif aliniita na kuniarifu kuwa nimeteuliwa kuwa Katibu wa Katibu Mkuu wa chama, wakati huo Katibu Mkuu alikuwa ni Shaabani Khamis Mloo.

Yako mengi ya kusema, lakini ninachoweza kusema kwetu sisi alikuwa si kiongozi tu, alikuwa ni baba mlezi, alikuwa ni mwalimu wetu. Amelipata jina la “Maalim” kwasababu ya kazi ya kusomesha, lakini likanasibika naye zaidi si kwa kusomesha kwake skuli za Unguja na Pemba, lakini ni katika kazi zake za siasa za kusomesha Wazanzibari kisiasa na sisi ambao alitujenga kisiasa na kutuandaa kuwa viongozi wa muda mrefu sana. Hivyo ndivyo ambavyo nimemjua Maalim Seif, nimefanya kazi naye nikiwa katibu wake akiwa Katibu Mkuu wa chama, nimefanya kazi naye katika mazungumzo ya mwafaka wa mwanzo wa mwaka 1995.

Mwafaka wa pili 2000, hadi jaribio la kutafuta mwafaka wa tatu lililokwama Butiama likianzia Bagamoyo 2007 mpaka 2008 na hatimaye maridhiano tuliyofanya yakiongozwa na Rais Aman Abeid Karume na yeye Maalim Seif.

Nimefanya kazi naye muda mrefu. Na katika kipindi hicho pia ndiye alikuwa akinishika mkono na kuniingiza katika siasa za kitaifa. Ni yeye aliyeniambia kazi ya ukatibu basi, sasa ni kuunda tume ya urais ya mwafaka na napaswa kwenda katika tume hiyo licha ya mimi kukataa na kusema wapelekwe wengine.

Lakini baadaye vilevile ulipokuja uchaguzi wa chama na kwa mara ya mwanzo niligombea nafasi za uongozi mwaka 2004 akawa na msukumo mkubwa wa kunifanya niwe Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na haki za binadamu wa chama na hatimaye nikagombea uwakilishi baada ya maridhiano ya mwaka 2009 na 2010, na kazi nyingi ambazo tumezifanya kwa pamoja.

Kwa hivyo, naweza kusema kuwa yeye kwangu mimi ni zaidi ya mzee, ni zaidi ya kiongozi, ni zaidi ya Maalim katika shughuli zangu. Hivyo ndivyo ninavyomkumbuka Maalim Seif katika safari ya kisiasa. Maalim Seif huwezi kumtia hila hata kwa nukta ndogo katika ufisadi licha ya kuwa katika madaraka na nafasi za juu kwa muda mrefu sana.

Kuna jambo ambalo Maalim Seif mwenyewe alilitaja katika kitabu chake alichokiandika kinachokusanya kumbukumbu za maisha yake na maisha ya Comrade Ali Sultan.

Alitaja kadhia ambayo hata mimi binafsi nakumbuka kuwa aliwahi kunieleza, na hata akikaa na jamaa wengine alikuwa anaizungumzia ambayo iliwashangaza wengi.

Mwaka 1987 alikuwa waziri kiongozi, alifanya ziara katika nchi za mashariki ya mbali akiitafutia Zanzibar uhusiano wa kiuchumi.


na ndio safari yake ya mwanzo kufika Singapore.

Lakini safari ile pia ilimpeleka katika nchi (Kisiwa) ya Brunei. Baada ya kukutana na mfalme wa Brunei katika Hijja Makkah, Saudi Arabia.

Katika ziara ile, kama tunavyojua Mfalme wa Brunei alitajwa kuwa ni mtu tajiri zaidi kuliko watu wote duniani kwa miaka ile, alimtunuku Maalim zawadi binafsi ya dola milioni tatu na alimwambia kuwa hii ni zawadi yako binafsi. Lakini aliporudi fedha zile Maalim Seif aliziingiza katika akaunti ya serikali katika hazina ya Zanzibar.

Alisema kuwa Mfalme wa Brunei hamjui bali alimtambua kama Waziri Kiongozi wa Zanzibar. Kwahivyo fedha zile haziwezi kuwa ni zawadi yake binafsi na hawezi kuzikubali. Hakujitajirisha. Alikuwa ni kiongozi kwa zaidi ya miaka arobaini.

Hata nyumba za kuishi hana, amebakia kuishi katika nyumba za kukodi. Lakini nyumba yake moja ya Pemba ilibidi ijengwe na kumalizwa na marafiki zake kwasababu ilikuwa inamshinda kujenga.

Hakuwahi hata kujishughulisha kumiliki gari isipokuwa gari alizopewa na chama kutumia kwa ajili ya kazi zake, Lakini alipoondoka katika nafasi ya uwaziri kiongozi kulikuwa na jaribio kubwa la kutaka kumchafua.

Kuliundwa tume ya kwenda kukagua nyaraka zote katika ofisi za waziri kiongozi kutafuta wapi labda kulikuwa na marupurupu au masurufu aliyoshindwa kurejesha matumizi yake, wakati alikuwa Maalim Seif hata posho za safari alizokuwa akipewa, akirudi hurejesha stakbadhi za matumizi na fedha zilizobakia huzirudisha katika akaunti ya serikali.

Mwisho katika hilo ambalo nataka kulitoa mfano vile vile, wengi hawajalijua kwasababu sijui kama aliwahi kumhadithia mwingine. Katika safari binafsi mara moja alikuwa anakwenda Dubai na alipofika pale alikuwa amechukua mkoba (briefcase) yake, lakini akajitokeza mfanyabiashara mmoja mwenye asili ya kiasia ambaye alikuwa ana mkoba uliofanana na wake.

Wakati wa kupitisha katika mashine ya ukaguzi kila mmoja akachukua wa mwenzake bila ya kujua. Maalim alinihadithia, alipofikia katika nyumba aliyofikia akalifungua na kukuta limejaa fedha, akajua kwamba sio lake. Jambo hili likamfadhaisha sana.

Alichokifanya katika begi lile ni kutafuta mawasiliano ya yule mwenye begi. Alipoyapata akampigia simu na kumwambia nadhani wewe umechukua begi langu, na yule mtu kwa mshituko akamwambia ni kweli. Alishangaa kuwa mtu alichukua begi lenye fedha na anataka kumrejeshea mwenyewe.

Hakumwambia njoo pahala fulani uje unifuate bali alimwambia kuwa atasogea na vijana wake nusu njia na yeye aende nusu njia ili warudishiane mabegi yao. Huyo ndiye Maalim Seif ambaye wengi walishindwa kumfahamu.

Imeandikwa Na Ismail Jussa