Prime
Laini za simu zawakamatisha watuhumiwa mauaji ya Bilionea Msuya

Maelezo hayo ya ungamo yaliyosomwa mahakamani na shahidi wa 10, Sajenti Atway Omar, yalieleza hatua kwa hatua namna bilionea Msuya alivyotoka Arusha, hadi anauawa eneo la Orkalili mijohoroni wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.
Leo tunakuletea ushahidi wa namna Jeshi la Polisi kitengo cha makosa ya kimtandao (Cyber Crime), kilivyotumia mawasiliano ya mwisho ya bilionea Msuya kuwapata watuhumiwa wa mauaji hayo.
Shahidi wa 11 wa upande wa mashtaka ni Koplo Selemani Mwaipopo kutoka divisheni ya uchunguzi wa makosa ya kimtandao ambaye mwaka 2013 wakati mauaji yanatokea alikuwa anafanya kazi Ofisi ya RCO Kilimanjaro.
Siku ya tukio la mauaji ya mfanyabiashara huyo, RCO Kilimanjaro, Ramadhan Ng’anzi alimjulisha juu ya mauaji hayo na kwamba ameunda timu tatu, moja ikiwa ya masuala ya makosa ya kimtandao na yeye akatakiwa kuiongoza.
Timu zote tatu zilikuwa chini ya Inspekta Samwel Maimu na walipofika eneo la tukio na kukusanya vifaa, na yeye akiwa mtaalamu wa masuala ya elektroniki, alipata simu aina ya Samsung, Iphone na Ipad moja.
Nini kilikutwa kwenye simu
“Tuliporudi ofisini kwa RCO tuliongezewa nguvu ya kachero Constebo William ambaye ni mtaalamu wa Cyber Crime kutoka makao makuu ya polisi. Tulimuunganisha kwa lengo la kuchunguza simu za marehemu,” alisema.
“Baada ya kuungana na William, tulianza kuchunguza simu za marehemu tulizozipata eneo la tukio na tulifanikiwa kuondoa password (nywila) ya simu ya Iphone na baadaye kuchunguza mawasiliano ya namba yake ya Vodacom”
“Kwa kuwa tayari tulikuwa tumeondoa password, tuliangalia simu zote zilizokuwa zimeingia na alizopiga pamoja na SMS (meseji) na tulikutana na namba 0682405323 ambayo ilikuwa ikimwelekeza kwenda eneo la tukio,” alieleza.
“Tulifuatilia usajili wa namba hiyo na kugundua imesajiliwa kwa jina la Motii Moongululu na ilisajiliwa Kituo cha Mabasi ya Arusha, siku moja kabla ya tukio. Tulibaini namba zingine nne na zote zilisajiliwa eneo hilo hilo moja kwa majina ya Kimasai”
Washukiwa walivyokamatwa
“Tulienda eneo hilo (stendi) pamoja na timu ya operesheni ikiongozwa na Inspekta Samwel na tulifanikiwa kumkamata Hamisa ambaye alisema hizo namba zilisajiliwa na mtu wanayemfahamu anaitwa Masai au Adam.
“Alitupatia namba za Adam tukafuatilia location (eneo alipo) na kugundua alikuwa Mirerani na tuliielekeza timu ya ukamataji ambayo ilifanikiwa kumkamata. Yeye akasema alisajili line hizo kwa maelekezo ya Mussa Mangu (mshtakiwa wa tatu).
“Alitupa namba ya Mussa na kwa kushirikiana na mtoa huduma (za mtandao) tulifanikiwa kufahamu location (eneo) aliyopo na wakati huo ilisoma KIA. Tulifanikiwa kumkamata baada ya kumpigia na kukubaliana kukutana naye Arusha,” alieleza shahidi huyo.
“Hiyo ilikuwa tarehe 10.08.2013. Baada ya kumkamata tulimkabidhi kwa timu ya mahojiano halafu tarehe 11.08.2013 Inspekta Samwel alitupa namba za watuhumiwa wengine. Zilikuwa ni za mtandao wa Airtel, Vodacom na Tigo”
“Majina yao yalikuwa Sadik (Mohamed-mshtakiwa wa sita), Karim (Kihundwa- mshtakiwa wa tano), Jalila (Zuberi-mshtakiwa wa nne), Ally (Mjeshi- mshtakiwa wa 7) na Shahibu (Jumanne au Mredii-mshtakiwa wa pili),” alieleza shahidi huyo.
Polisi walipekua hadi Kondoa
“Jalila na Ally walisomeka wako Babati, Kareem na Sadiki walisomeka wako Dar es Salaam na Shaibu alisomeka yuko Mirerani. Tarehe 16.08.2013 tuliielekeza timu ya ukamataji wakaenda Mirerani na kufanikiwa kumkamata Shaibu,” alisema.
“Tuliendelea kufuatilia na tulifika hadi Kondoa ambapo tulifanikiwa kumkamata Jalila akiwa Guest House (nyumba ya wageni) ila hatukufanikiwa kumpata Ally kwa sababu wakati huo simu yake ilikuwa inasomeka yuko Mwanza.
“Chini ya uongozi wa Inspekta Samwel na mimi, tulikwenda Dar es Salaam lakini namba ya Sadik ilikuwa imezimwa. Tulipoweka mtego wa kumkamata Karim ilishindikana kwa sababu alikuwa anawasiana na watu wachache sana.
“Tuliendelea kuifuatilia namba ya Karim na siku iliyofuata ilionekana anasafiri uelekeo wa Dodoma. Tuliendelea kumfuatilia lakini tulipofika Dodoma alisomeka yuko Tabora na uelekeo ulisomeka Kaliua. Tulikwenda hadi huko Kaliua.
Shahidi huyo aliyekuwa akitoa ushahidi wake kwa kuongozwa na wakili wa Serikali, Lucy Kyusa, alisema baada ya kuweka mitego walifanikiwa kumkamata Karim na Sadick. Tulirudi nao hadi kituo cha Polisi cha Kaliua,” alieleza.
“Baadaye tulirudi na watuhumiwa hao Moshi na kuwakabidhi kwa timu ya mahojiano. Tuliendelea kumtafuta Ally ambaye alikuwa anabadili namba anayotumia lakini handset (simu) ilikuwa ni ile ile.
Simu yamkamatisha Kigoma
“Hii ilitufanya tuchukue muda mrefu kumfuatilia hadi tarehe 02. 10. 2013 alipoweka laini ambayo ndio alikuwa akiitumia mara kwa mara. Namba iliendelea kuhama hama na tulifuatilia hadi ikatufikisha Kigoma tarehe 04. 10. 2013.
“Tulihisi atakuwa anasafiri, hivyo tulitoka hotelini na kwenda Kituo cha Mabasi Kigoma. Inspekta Samwel alitwambia tuipige hiyo namba tuone kama itaita, tulipopiga tuliona mtu amepokea simu huku akisema “hallo, haloo sikusikii”.
“Hapo ndipo Inspekta Samweli alishuka kwenye gari na kwenda kumkamata. Alipokuwa anakamatwa akasema aahh, jamani mmenifuata mpaka huku, naingia kwenye gari. Aliingia kwa hiyari kwenye gari tukaenda Kituo cha Polisi Kigoma.
“Tarehe 16. 08. 2013 nilimkamata mtu anaitwa Shaibu. Baada ya kumkamata, timu ya ukamataji ilimpeleka Kituo cha Polisi Mirerani. Nakumbuka tukiwa hapo Inspekta Samweli aliniagiza nimwandike maelezo ya onyo,” alieleza shahidi.
Shahidi huyo alisema alitafuta chumba kimojawapo katika kituo hicho kwa ajili ya kufanya mahojiano hayo, nikamchukua mtuhumiwa mahabusu na kumweleza haki zake lakini akasema yuko tayari kutoa maelezo bila wakili wala ndugu.
“Baada ya hapo nilimtaka anisimulie namna alivyohusika katika hilo tukio na nini anakifahamu kuhusu tuhuma zinazomkabili. Katika maelezo hayo alikiri kuhusika kumuua Erasto Msuya. Alikuwa na afya njema hata tulipomaliza kuandika.
Ubishani wa maelezo
Shahidi huyo aliomba kutoa maelezo hayo kama kielelezo, lakini upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Majura Magafu aliyemtetea, ukisema mteja wake anasema Agosti 16, 2013 hakuwahi kuandika maelezo na alikuwa hajakamatwa.
“Anachokumbuka ni kuwa tarehe 18. 8. 2013 ndio aliteswa na kulazimishwa kuweka sahihi kwenye maelezo ambayo hayajui. Hiyo statement aliyolazimishwa kusaini na kuweka dole gumba hakusomewa wala hajui maudhui yake,” alisema.
“Anasema baada ya kuteswa sana na kuchomwa sehemu mbalimbali za mwili wake bila hata polisi kuhofu kama angeweza kufa kituoni, Agosti 21. 08. 2013 alipewa PF3 na kupelekwa hospitali ya Mawenzi kwa matibabu,” alidai wakili.
“Aliendelea na matibabu akiwa gereza la Karanga na baada ya madaktari katika gereza hilo kuona afya yake inadhoofu, alipewa rufaa kwenda hospitali ya Rufaa ya KCMC. Hizi ndio sababu zetu kwa nini tunapinga maelezo haya,” alisisitiza.
Akijibu hoja hiyo, Wakili mwandamizi wa Serikali, Abdalah Chavulla alisema kwa vile utoaji wa hiyari wa maelezo hayo unatiliwa shaka, msimamo wa sheria unataka kufanyike kesi ndani ya kesi ili kuthibitisha kile kinacholalamikiwa.
Jaji Salma Maghimbi aliyesikiliza kesi hiyo, alikubaliana na hoja hizo na kuamuru kusikilizwa kwa kesi ndani ya kesi, ingawa hata hivyo baada ya usikilizwaji kukamilika, mahakama ilikataa maelezo hayo yasipokelewe.
Akijibu maswali ya dodoso kutoka kwa Wakili Hudson Ndusyepo aliyemtetea mshtakiwa wa kwanza, Sharifu Mohamed, shahidi huyo alisema katika kufuatilia watuhumiwa hao, walikuwa wakitumia magari mawili tofauti tofauti ya polisi.
Kwa upande wa maswali ya wakili Majura Magafu, shahidi huyo alisema hakumbuki mwili wa bilionea Msuya uliondolewa saa ngapi eneo la tukio ila aliuona ukiondolewa kwa kuwa wakati huo yeye alikuwa kwenye gari.
Kuhusiana na usajili wa laini za simu, Shahidi huyo alisema wakala aliyezisajili aliwaeleza kuwa zilisajiliwa kwa majina ya Motii Mongulu, Motii Lilia na Motii Siria na laini hizo hazikusajiliwa kwa kutumia kitambulisho chochote cha mmiliki.
Akijibu maswali ya Wakili Emmanuel Safari, alisema mtu aliyekuwa akikusanya vielelezo ni Inspekta Samwel na kwamba ndiye aliyekusanya simu eneo la tukio ila hawezi kukumbuka ni wapi hasa simu hizo zilipatikana katika eneo la tukio.
Akijibu swali maswali ya wakili John Lundu, shahidi huyo alisema simu za marehemu ndizo zilizowasaidia kubaini namba aliyokuwa akiwasiliana nayo kumwelekeza kwenda kwenye eneo ambalo baadaye ndipo aliuawa.