Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Latra yaingilia kati mgomo wa madereva wa malori

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa tangazo la mpango wa mgomo huo, huduma za usafirishaji wa mizigo kupitia malori zinatarajiwa kusitishwa kuanzia Julai mosi, 2026, saa 12:00 asubuhi.

Dar es Salaam. Hatimaye Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) imeingilia kati vuguvugu la baadhi ya madereva wa malori wanaotishia kusitisha shughuli za usafirishaji wa mizigo mikoani na nje ya nchi kuanzia Julai mosi, 2026, wakishinikiza kutatuliwa kwa changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Madereva hao wametangaza kusudio la kugoma kuanzia saa 12:00 asubuhi ya tarehe hiyo, wakieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuishinikiza Serikali kushughulikia madai yao yanayohusu masilahi, mazingira ya kazi pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya barabara ili kupunguza ajali.

Kwa mujibu wa tangazo lililosambazwa katika makundi ya WhatsApp wiki mbili zilizopita, likiwa na kaulimbiu isemayo, “Sauti ya dereva isikike, haki yetu itendeke,” huduma za usafirishaji wa mizigo kwa malori zinatarajiwa kusitishwa endapo hakutafikiwa makubaliano.

Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa kikao cha mazungumzo kati ya Serikali na wadau wa sekta hiyo kinatarajiwa kufanyika kesho, Jumatatu, Juni 15, 2026, jijini Dar es Salaam, kikihusisha vyama vya madereva wa malori, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) na Kikosi cha Usalama Barabarani.

Kikao hicho kinatajwa kuja siku 12 baada ya Latra kueleza kuwa iko tayari kufanya mazungumzo na madereva ili kusikiliza na kushughulikia changamoto zilizo ndani ya mamlaka yake.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu kuhusu sakata hilo jana Jumamosi, Kaimu Ofisa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa Latra, Fungo Augustus, amesema mamlaka hiyo ipo tayari kusikiliza hoja za madereva na kuchukua hatua kwa yale yaliyo ndani ya majukumu yake.

Amesema baadhi ya makundi yanayojitambulisha kama madereva hayajatambulika rasmi, lakini akaongeza kuwa watafanya jitihada za kuwasiliana nao ili kuwasikiliza, huku akibainisha kuwa baadhi ya hoja zinahusu taasisi nyingine za Serikali.

Hata hivyo, alipozungumza tena jana Jumamosi, Juni 13, 2026, Fungo amesema bado hawajafanikiwa kupata ushirikiano kutoka kwa vinara wanaoratibu mpango huo wa mgomo, licha ya jitihada za kuwasiliana nao kwa njia mbalimbali, ikiwamo simu.

“Tumejitahidi kuwatafuta wanaohamasisha mgomo huo ili kujua madai yao, lakini hatujapata ushirikiano. Kuna wanaojibu kuwa bado wapo Congo,” amesema.

Kuhusu kikao kinachotarajiwa, amesema wamepokea taarifa za mkutano huo na kwamba watahudhuria pamoja na Kikosi cha Usalama Barabarani, ambacho mara nyingi huandaa mikutano ya wadau wa sekta hiyo.

Kwa upande wao, viongozi wa vyama vya madereva wamesema wamepokea mwaliko wa kikao hicho, ingawa wameeleza kuwa ajenda kamili bado haijaainishwa wazi.

Katibu wa Chama cha Wafanyakazi Madereva Tanzania (Tadwu), Ally Kimaro, amesema wamepokea mwaliko wa kushiriki kikao hicho kitakachofanyika Dar es Salaam, lakini hakuwa na uhakika kama suala la mgomo litakuwa miongoni mwa mada zitakazojadiliwa.

“Tumepokea mwaliko wa mkutano wa Jumatatu, lakini sina uhakika kama mgomo utazungumziwa. Mwaliko unasema ni masuala ya uadilifu na rushwa,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Malori Tanzania (Chawamata), Nuhu Mgodo, amesema wamepokea barua ya mwaliko huo, lakini akasisitiza kuwa si utaratibu kutoa maelezo ya ndani ya kikao kabla ya kufanyika.

Kwa upande mwingine, Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Uchukuzi Tanzania (COTWU-T) kimesema ni vigumu kutoa msimamo kuhusu mgomo huo kwa kuwa walioutangaza hawatambuliki kama wanachama wao.

Naibu Katibu Mkuu wa COTWU-T, Musa Mwakalinga, amesema bado kuna changamoto ya uungwaji mkono mdogo wa madereva kujiunga na vyama rasmi, hali inayodhoofisha nguvu ya pamoja ya kutetea haki zao.

Amesema, kwa mujibu wa taratibu za kazi na uhusiano kazini, mgomo unatakiwa kutangazwa na vyama vinavyotambuliwa kisheria baada ya mazungumzo kushindikana.

Hata hivyo, amesema chama hicho kinatarajia kuwasilisha baadhi ya madai ya madereva kwa Waziri Mkuu, yakiwamo yale ya mikataba ya ajira na suala la msongamano wa magari barabarani.

Katika tangazo hilo la mgomo, madereva wamewasilisha madai saba, yakiwamo kuongeza kima cha chini cha mshahara kutoka Sh350,000 hadi Sh1 milioni kwa mwezi.

Mengine ni kurahisisha masharti ya uhuishaji wa leseni, kuondoa baadhi ya masharti kwa madereva wenye uzoefu wa zaidi ya miaka 15, na kupunguza gharama za mafunzo ya leseni zinazofikia Sh375,000.

Pia, wanataka Bandari Kavu (ICD) zilizopo Dar es Salaam zihamishiwe Kwala, kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara, kuimarishwa kwa mfumo wa kushughulikia changamoto za madereva kwa wakati, pamoja na kuhoji uwepo wa maofisa wa Latra barabarani na msingi wa baadhi ya shughuli zao za ukaguzi.