Wamiliki wa malori walaani mgomo wa madereva

Muktasari:

Vyama vya wasafirishaji ambavyo ni, Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA), Chama cha wamiliki wa maroli wadogo na wa kati (TAMSTOA) na Chama cha Wasafirishaji Tanzania (TAT)  wamelaani mgomo wa madereva ulioanza Juli 25, 2022.

Dar es Salaam. Vyama vya wasafirishaji pamoja na wamiliki wa malori nchini Tanzania vinalaani mgomo uliofanywa na madereva wa malori katika mpaka wa Tunduma, mkoani Songwe.

 Vyama hivyo ni, Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA), Chama cha wamiliki wa maroli wadogo na wa kati (TAMSTOA) na Chama cha Wasafirishaji Tanzania (TAT) ambao leo Ijumaa, Julai 29, 2022, wamezungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Tamstoa, Chuki Shabani ametoa wito kwa madereva kuachana na migomo hiyo kwani dereva atakayebainika kugoma au kuhatarisha usalama kwa kuvuruga amani, kuleta usumbufu na uharibifu wa mali atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe.

"Siku zote tunaamini katika meza ya mazungumzo kutatua migogoro na si vinginevyo, sisi kama vyama vya wasafirishaji Tanzania tunaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa Serikali kuhakikisha migomo hii isiyo halali inadhibitiwa na kupatiwa suluhisho la haraka," amesema

Pia, amesema wanaunga mkono juhudi za Serikali kwa kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa ikiwani pamoja na kuwapatia madereva mikataba ya ajira pamoja na haki zao za msingi.

Wamiliki hao wamejitokeza kulaani mgomo huo ulioanza Julai 25, 2022 ambapo madereva walikuwa wakidai mambo mbalimbali ikiwemo kuboreshewa mazingira ya kazi zao kwa kupata mikataba ya ajira.

Hivi karibuni Ofisi ya Waziri mkuu, kazi, ajira vijana na watu wenye ulemavu ilieleza kushughulikia malalamiko na hoja za wafanyakazi madereva, kabla ya Vyama vya wafanyakazi wa sekta ya mawasiliano na uchukuzi vya COTWU (T) na TAROTWU kuishukuru kwa hatua hiyo na kuwasihi madereva kutojiingiza katika migomo wakati utatuzi wa hoja zao ukiendelea.

Naibu Katibu mkuu wa COTWU (T), Musa Mwakalinga hivi karibuni alisema katika hoja hizo, Serikali imeshughulikia hoja nane na nyingine nne wanatarajia zitaendelea kushughulikiwa.

Hoja hizo mfumo wa upakiaji wa mafuta depo, malipo ya madereva wanaosafirisha sumu, malipo kuhusu ushushaji mzigo na utaratibu wa ushushaji wa vimiminika na gesi.

"Hoja ambazo Serikali imezishughulikia ni pamoja na mikataba ya ajira ya madereva isimamiwe na Serikali au chama cha wafanyakazi na sio sasa inakuwa ni ya dereva na tajiri.”

“Mishahara ipitie benki na itolewe kwa wakati, wakatiwe bima na NSSF iliyohai sanjari na wastaafu kupata penseni, magari yafungwe spidi gavana na si VTS na dereva akifia nje ya nchi Serikali ichukue hatua kuhakikisha anarudishwa nchini kwa maziko,” alisema