Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Latra yapunguza faini makosa ya barabarani kwa asilimia 40

Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihezile (wa pili kushoto) akizungumza na Watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa aridhini (LATRA), alipotembelea Banda la Mamlaka hiyo kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa (sabasaba), jijini Dar es Salaam leo July6 2026. Picha na Said Powa

Muktasari:

  • Faini za makosa ya barabarani zimepunguzwa kutoka Sh250, 000 hadi Sh150, 000 ili kuboresha utoaji wa huduma na dereva anayefanya kosa kwa mara ya kwanza anaonywa kupitia mfumo wa kielektroniki badala ya adhabu.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) imepunguza faini za makosa ya barabarani kwa magari ya usafiri wa umma kwa asilimia 40 kutoka Sh250, 000 hadi Sh150,000.

Hiyo imeenda sambamba na kuanzisha mfumo wa kutoa onyo kwa madereva wanaofanya kosa kwa mara ya kwanza, kufuatia malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa madereva kuhusu ukubwa wa adhabu hizo.

Hatua hizo mpya zilizoanza kutumika Julai 1, 2026 zilitangazwa na Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Suluo amesema mamlaka hiyo ilifanya mapitio ya adhabu hizo baada ya kupokea malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa madereva na waendesha huduma za usafiri waliodai faini za awali zilikuwa kubwa kupita kiasi.

“Mwaka jana tulipokuwa hapa Sabasaba, tulisikiliza malalamiko ya madereva waliokuwa wakisema Latra inatoza faini kubwa sana. Tumezifanyia marekebisho na kuanzia Julai 1, 2026 zimeanza kutumika.

Suluo amesema madereva watakaofanya kosa kwa mara ya kwanza licha ya kupewa onyo, kosa hilo likirekodiwa katika mfumo wa kidijitali wa ufuatiliaji na adhabu itatolewa endapo dereva atarudia kosa hilo.

Amesema maboresho hayo ni sehemu ya marekebisho ya kanuni za usafiri wa barabarani yanayolenga kuhamasisha uzingatiaji wa sheria kuhakikisha utekelezaji wa haki.

“Mfumo huu mpya unatupa uwezo wa kuhifadhi kumbukumbu za kila kosa la barabarani linalofanywa na dereva. Hii inatusaidia kufuatilia utii wa sheria na kubaini wanaorudia makossa, badala ya kuwaadhibu vikali madereva kwa kosa la kwanza,” amesema.

Kwa mujibu wa Suluo, kipaumbele cha sasa cha Latra ni kutoa elimu kwa madereva na waendesha huduma za usafiri kuhusu kanuni hizo zilizoboreshwa kabla ya kuimarisha zaidi utekelezaji wake.

Amesema mamlaka hiyo inaamini kuwa uelewa na utii wa sheria vitachangia kwa ufanisi zaidi katika kuimarisha usalama barabarani kuliko kutumia adhabu pekee.

Suluo pia aliwataka madereva na wananchi wanaotembelea Maonesho ya Sabasaba kufika katika banda la Latra ili kujifunza zaidi kuhusu huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo, mifumo yake ya kidijitali pamoja na kanuni mpya za usafiri wa barabarani.

Mmoja wa madereva wa daladala jijini Dar es Salaam, Hamisi Mwakalinga amesema uamuzi wa Latra kupunguza faini ni nafuu kwa madereva wengi ambao walikuwa wakilalamikia ukubwa wa adhabu hizo.

“Faini ya Sh250,000 ilikuwa kubwa sana kwa madereva wengi, hasa kwa anayefanya kazi ya kuingiza fedha za kila siku. Kupunguzwa hadi Sh150,000 ni hatua nzuri na itapunguza mzigo kwa waendeshaji wa usafiri wa umma,” amesema.

Akizungumzia mfumo wa kutoa onyo kwa kosa la kwanza, amesema utawapa madereva nafasi ya kujirekebisha kabla ya kuadhibiwa, ingawa alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kuhusu kanuni mpya ili kuhakikisha madereva wote wanazielewa na kuzifuata.

“Si kila kosa hutokana na uzembe; wakati mwingine dereva anaweza kukosea bila kukusudia. Mfumo wa onyo utasaidia madereva kujifunza kutokana na makosa yao, lakini elimu iendelee kutolewa ili kila mtu ajue wajibu wake na sheria zinazomwongoza,” amesema.