LHRC, THDRC yawashtaki Kamanda Mambosasa, AG sakata la Tito Magoti

Muktasari:
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam nchini Tanzania inamshikiliwa ofisa elimu kwa umma wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magito tangu Ijumaa ya Desemba 20, 2019 kwa uchunguzi pamoja na wenzake watatu.
Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) nchini Tanzania wamefungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania kulitaka jeshi la polisi limpeleke mahakamani ofisa wa LHRC, Tito Magoti.
Magoti anashikiliwa na Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam tangu Ijumaa iliyopita ya Desemba 20, 2019 baada ya kumkamata akiwa Mwenge jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amekaririwa na Mwananchi akisema inamshikiliwa Magoti na wenzake watatu kwa uchunguzi wa tuhuma za makosa ya jinai inayowakabilia.
Hata hivyo, Mambosasa hajawahi kubainisha ni kituo gani ambacho Magoti anashikiliwa.
Leo Jumatatu Desemba 23, 2019, LHRC, THDRC na familia ya magoti wamezungumza na waandishi wa habari wakilaani kitendo cha polisi kuendelea kumshikilia pasina kumfikisha mahakamani.
Washtakiwa katika kesi hiyo iliyofunguliwa jana Jumapili na LHRC, THDRC kwa njia ya mtandao ni Kamanda wa Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa na Mwanasheria mkuu wa Serikali ya Tanzania (AG), Profesa Adelardus Kilagi.
Mkurugenzi Mtendaji LHRC, Anna Henga amesema wamechukua uamuzi huo baada ya jeshi la polisi kukaa kimya bila kuweka wazi kituo gani cha polisi alipo mfanyakazi mwenzao.
“Imekuwa ni tabia inayozidi kukuwa nchini kwa vyombo vya usalama wa raia kukamata watuhumiwa kisirisiri kisha kubaki nao muda mrefu bila ndugu zao kuwa na taarifa,” amesema Anna
Amesema tamko la jeshi la polisi linalodai kuhusika na ukamatwaji wa Magoti linauthibitishia umma kuwa wanamshikilia ofisa huyo lakini hawaruhusu wakili wala mwajiri wake kumwona na kusimamia mahojiano yake.
“Ikumbukwe jeshi la polisi halina mamlaka ya kumshikilia mtuhumiwa zaidi ya masaa 24 bila kumwachia kwa dhamana ya polisi au kumfikisha mahakamani, haki ya dhamana ni haki ya kikatiba ambayo raia yoyote anayo endapo kosa alilotenda linadhaminika,” amesema.
Kwa upande wake Mratibu wa THRDC, Onesmo Ole Ngurumwa amesema kesi hiyo ilifunguliwa jana Jumapili kwa njia ya mtandao.
“Tumewasilisha hati ya dharura katika mahakama kuu kulitaka jeshi la polisi wampatie dhamana Magoti tunatoa siku moja ya leo kama watashindwa kufanya hivyo tutaendelea na kesi,” amesema