Lipumba atoa neno la faraja vigogo CUF kukimbilia ACT-Wazalendo

Kiongozi wa Chama cha ACT wazalendo Zitto Kabwe akiwasili wilaya ya Micheweni Mkoa wa kaskazini Pemba jana, wakati wa ziara yake ya siku tatu kisiwani humo. Picha na Muhammed Khamis

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Zitto, viongozi wa CUF waliojiunga na ACT ni wa wilaya zote kumi na moja za Zanzibar, viongozi wa majimbo 54 na kata 101.

Dar/Pemba. Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ametoa neno la faraja baada ya viongozi wengi wa chama hicho kuhamia ACT-Wazalendo kuungana na Maalim Seif Sharif Hamad.

Akizungumza na Mwananchi jana, Profesa Lipumba alisema orodha ya viongozi wa CUF wanaotajwa kuhamia ACT iliyotolewa na kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe ni propaganda, huku akiahidi kuwa atakapoanza ziara kisiwani Pemba ataweka wazi kila kitu.

Tangu Maalim Seif ambaye alikuwa katibu mkuu wa CUF kujiunga ACT Machi 18 mwaka huu, kumekuwa na wimbi kubwa la viongozi wa CUF na baadhi ya wanachama kuanzia ngazi za chini hadi juu kuhamia chama hicho.

“Si kweli wanaosema kuwa asilimia 90 ya viongozi wa matawi ya CUF wamehamia ACT. Hizo ni propaganda za Maalim Seif,” alisema Lipumba.

Viongozi hao wamejiunga na ACT tangu Zitto na Maalim Seif walipoanza ziara ya siku nne kisiwani Zanzibar iliyomalizika jana, wakianzia Unguja na baadaye Pemba.

Kwa mujibu wa Zitto, viongozi wa CUF waliojiunga na ACT ni wa wilaya zote kumi na moja za Zanzibar, viongozi wa majimbo 54 na kata 101.

Wengine ni viongozi wa matawi 675 ambao Zitto alisema wameshusha bendera za CUF na kupandisha za ACT huku wengine wakisubiri bendera zaidi ili waziweke katika matawi yao.

Katika ziara ya viongozi hao, Mwananchi ilishuhudia wenyeviti wa wilaya zote nne za Pemba, makatibu wao na wajumbe wa kamati za utendaji na viongozi wa jumuiya za vijana wakikabidhiwa kadi. Miongoni mwao ni Juma Muhunzi, baba mzazi wa makamu mwenyekiti wa CUF, Abassi Juma Muhunzi.

Katika maelezo yake, Profesa Lipumba ambaye kitaaluma ni mchumi alisema, “wanafanya hivi ili kuaminika na Wazanzibari kuwa CUF haina kitu kwa sasa jambo ambalo si la kweli. Tutalithibitisha hili kupitia ziara na vikao vyetu tutakavyovifanya siku chache zijazo.”

Alisema kinachofanywa na Maalim Seif ni kama mbio za sakafuni ambazo zitafikia ukingoni, “hatuna hofu na ziara hiyo ambayo baadhi ya wanachama na viongozi wa CUF wanatangaza kukihama chama chetu.”

Profesa Lipumba alisema yeye na viongozi wenzake wamepanga kufanya ziara na vikao kwenye ofisi za CUF zilizopo Unguja na Pemba na watawaeleza Wazanzibari ukweli wa kinachoendelea baada ya Maalim Seif kuhama.

“Tunajipanga na tutakwenda kuzungumza na wanachama wetu na tutakuwa na mpango mkakati maalumu wa kuimarisha CUF kuhakikisha inakuwa imara Pemba na Unguja. Lengo letu ni kuleta umoja wa kitaifa Zanzibar na kuondoa uongo unaoenezwa Seif.”

Kauli kama hiyo ilitolewa na katibu mkuu wake ambaye alisema siku yoyote kuanzia leo viongozi wa CUF wataanza ziara Zanzibar kukagua matawi ya chama hicho na kuwaeleza wanachama wao juu ya kinachoendelea.

“Waliojiunga CUF ni viongozi wa chama katika ngazi mbalimbali na sio wanachama wa kawaida ambao naamini wapo wengi kuliko waliotoka,” alisema.

Alibainisha kuwa wanaohamia ACT wanafanya hivyo kwa shinikizo la Maalim Seif na hawafanyi kwa mapenzi yao

Wanachama wapya walonga

Aliyekuwa mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Micheweni, Rashid Khalid alisema kazi iliyopo sasa ni kuiimarisha ACT ili chama hicho kiweze kuibuka na ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Katibu wa zamani wa CUF Wilaya ya Chakechake, Saleh Nassor Juma ambaye sasa ni kaimu katibu wa ACT wa wilaya hiyo alisema kazi ya kuandikisha wanachama imemalizika na atahakikisha kila aliyekuwa CUF anajiunga na chama hicho.

“Mfano tangu ilipoanza ziara hii ni ngumu kuona bendera ya CUF ikipepea, hii ni ishara kuwa wananchi wameamua,” alisema Juma.

Zitto, Maalim wamaliza ziara

Akizungumza katika siku ya mwisho ya ziara hiyo, Zitto aliwataka wakazi wa Pemba kutambua kuwa shughuli za harakati si za siku moja, zinahitaji ujasiri na kuwataka kutovunjika moyo ili mambo wanayoyahitaji yaweze kupatikana.

Maalim Seif aliwataka wananchi kuwa watulivu wanapodai haki yao, akibainisha kuwa huenda walipohamia wakakumbana na hujuma alizodai zilitokea wakati akiwa CUF, hasa kila unapoelekea uchaguzi, akitolea mfano ule wa mwaka 2015.