Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lissu agusia urafiki wake na Msigwa, amtaja Mbowe

Mchungaji Peter Msigwa katika picha ya pamoja na Makamu Mwenyekiti Chadema Bara, Tundu Lissu. Picha na Maktaba

Dar es Salaam. Licha ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, Tundu Lissu kukiri Mchungaji Peter Msigwa ni rafiki yake, amesema atakabiliana na kada huyo baada ya kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM).

Lissu amesema hayo leo Alhamisi Desemba 12, 2024 wakati akijibu swali la waandishi wa habari aliloulizwa kuwa Mchungaji Msigwa ni rafiki yake na kada huyo wa zamani wa Chadema tangu ahamie CCM amekuwa anakishambulia chama hicho na y eye hajamkana hadharani.

Katika mkutano huo, Lissu ametangaza nia yake ya kuwania uenyekiti wa Chadema akitaja sababu mbalimbali ikiwemo mazingira ya siasa ya hivi sasa yanamhitaji mtu kama yeye kukiongoza chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Katika majibu yake Lissu amesema: “Niliwahi kukana hadharani siku moja. Sikuwahi kufanya hivyo jamani? Akajibiwa na wafuasi wake ‘umewahi’. Nilisema hivi, ,kwa vile umehamia huko (CCM), itabidi tukabiliane, nakumbuka nilisema maneno haya’.”

Mbali na hilo, Lissu amesema amewahi kutamka kwamba maneno yanayozungumzwa na Mchungaji Msigwa yajibiwe.

Pamoja na hayo, amesisitiza mbunge huyo wa zamani wa Iringi Mjini alikuwa rafiki yake na kuwa huo ndiyo ukweli.

“Nitasema hakuwa rafiki kwa sababu amekimbilia CCM? Nilisema kuondoka kwake kumeniuma sana, kwa sababu najua… amehamia huko, kama rafiki yake nimeumia sana, kuna marafiki zake wengi wanaojifanya hawakuwa naye, hivi sasa.

“Kwa nini nasema alikuwa rafiki yangu. Wakati naenda Nairobi (Kenya), niliambiwa alishikilia chupa ya damu na mwenyekiti (Mbowe) anaangaika na mtungi wa gesi. Sasa mnataka nisemeje kwa watu wa aina hiyo? Nimtukane au niseme hajawahi kuwa na maana yoyote, haiwezekani. Kuondoka kwake kumetuumiza wengi,” amesema Lissu.

Lissu alikuwa anasimualia kisa cha Septemba 7, 2019, aliposhambuliwa kwa risasi katika makazi yake mjini Dodoma na baada ya kupatiwa huduma za awali katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, usiku wa siku hiyohiyo alipelekwa Nairobi kwa matibabu, safari ambayo alisindikizwa na watu kadhaa wakiwemo Mbowe na Msigwa.

Lissu amesema panmoja na Mchungaji Msigwa kutimkia CCM, atatafuta namna ya kukabiliana na mjumbe huyo wa zamani wa kamati kuu.

Juni 30, 2024, Mchungaji Msigwa aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, alitangaza kukihama chama hicho na kujiunga na CCM baada ya kushindwa uchaguzi wa kutetea nafasi hiyo.

Tangu tetesi za Lissu kutaka kutangaza nia yake kuwania uenyekiti katika uchaguzi unaotarajia kufanyika mapema mwakani, kumeibuka minyukano miongoni mwa makada wa Chadema, huku Mchungaji Msigwa akidaiwa kuwa na mkono wake.

Mchungaji Msigwa anaelezwa yuko nyuma ya mkakati wa Lissu kuchuana na Mbowe na ndiye alikuwa anawapigia simu baadhi ya watu kuwashawishi kumuunga mkono.

Mbunge huyo wa zamani wa Iringa Mjini (2010-2020), inaelezwa anapanga mikakati hiyo na baadhi ya wajumbe wengine wa kamati kuu, ambao ni marafiki zake kuwa ikiwezekana mbele ya safari wakajiunge naye CCM.

Wiki iliyopita Mwananchi lilipomtafuta Mchungaji Msigwa juu ya kuhushishwa kwake na mipango hiyo, alisema: "Wanaosema hivyo hawajielewi. Mimi nimfanyie kampeni Lissu kwa masilahi gani? Nipo chama tawala, kwa hiyo yeyote kati yao, ni hasimu wangu kisiasa.

“Nimfanyie Lissu kampeni ili iweje? Ni watu waliokosa hoja na wameshindwa kumtetea mwenyekiti wao aliyedumu muda mrefu, kwa hiyo wanatafuta mtu wa kumfia. Hayo ni matatizo yao wasinihusishe mimi,” alisema Mchungaji Msigwa.


Bega kwa bega na Mbowe

Katika hatua nyingine, Lissu amesema yupo upande wa mwenyekiti wake, Mbowe katika kuhakikisha wanalinda utamaduni wa chama hicho wa kubadilishana uongozi kwa kutumia chaguzi huru na haki.

“Nimekuwa na mwenyekiti 'side by side' kwa miaka 20, hii inapaswa kukwambia kitu fulani. Nafikiri hicho kitu kinachotokana na miaka 20, sidhani kama kuna mtu anaweza kusema nimekuwa chawa wa mwenyekiti kwa miaka 20, kwa sababu sijawahi kuwa chawa,” amesema Lissu akishangiliwa na washiriki wa mkutano huo.

“Lakini nimekuwa upande wake kwa miaka 20, hata sasa hivi nipo upande wake pia katika kuhakikisha tunalinda utamaduni wa chama chetu wa kubadilisha uongozi kwa kutumia chaguzi huru na haki. Niamini hata yeye (Mbowe) yupo upande wangu,” amesema Lissu.


Walichokisema makada

Baadhi ya makada waliohudhuria mkutano wa Lissu wamesema hotuba ya kiongozi hiyo imekuwa nzuri na imeonyesha namna bora ya uongozi unavyotakiwa katika kuongoza taasisi.

“Hotuba yake imeonyesha uhai wa chama kwa siku za usoni, hakuwa na ubaguzi wala upendeleo katika maelezo yake. Maelezo yake yalijaa misingi na miiko ya uongozi, alichokizungumza kimedhihirisha ukweli, matumaini yangu akifanikiwa chama kitasonga mbele,” amesema Alfred Majira, mwenyekiti wa Chadema Kata ya Sinza.

Kada mwingine Shakira Masoud kutoka Tabora, amesisitiza viongozi kuelewana wakati huu wanapoelekea katika uchaguzi mkuu wa chama hicho ili kuepusha mpasuko.

“Amezungumza vizuri kwa sababu katiba inaruhusu, kikubwa uchaguzi uwe huru na haki basi,” alisema Masoud.